::::::::
Serikali imeendelea kufanya uwekezaji mkubwa katika ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya elimu pamoja na kuongeza fursa za masomo katika ngazi mbalimbali. Miongoni mwa hatua hizo ni kuongezeka kwa bajeti ya mikopo ya elimu ya juu kutoka Sh. bilioni 464 mwaka 2020/21 hadi Sh. bilioni 926.7 mwaka 2025/26.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Disemba 10, 2025 jijini Dar es Salaam, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema kuwa hatua hizo zinalenga kuwawezesha vijana kumudu kikamilifu mahitaji na changamoto za soko la ajira la karne ya 21.
Ameeleza kuwa Serikali inaendelea kutoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi waliofanya vizuri katika fani za sayansi, teknolojia, uhandisi, Hisabati, TEHAMA na sayansi ya nyuklia kupitia programu za Samia Scholarship na Samia Scholarship Extended.
Aidha, katika kutekeleza Mpango wa Samia Scholarship Extended DS/AI+, vijana 50 watakaosomea fani za Data Sayansi ikiwemo Akili Unde wanaendelea na maandalizi katika Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST) Arusha, kabla ya kwenda kusoma nje ya nchi.
Kuhusu elimu ya ufundi, Waziri Mkenda amesema Serikali imejenga vyuo vipya vya VETA katika mikoa ya Geita, Simiyu, Njombe na Rukwa, huku ujenzi wa Chuo cha VETA cha Mkoa wa Songwe pamoja na vyuo 64 vya wilaya ukiendelea nchini.
Pia amebainisha kuwa ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi (Polytechnics) Mkoani Dodoma umekamilika, na sasa inajiandaa kuanza ujenzi wa vyuo hivyo katika Mikoa ya Mwanza, Kigoma, Mtwara, Morogoro na Zanzibar.