Mwaka 2025 umekuwa mgumu kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kutokana na mashambulizi makali ya ndani na nje kilichoyapata, jambo ambalo wachambuzi wa siasa wanaeleza kuwa wamepitishwa kwenye “tanuri la moto”.
Tofauti na vyama vingine vya upinzani, Chadema kimejipambanua kama chama kikuu cha upinzani ambacho kina uwezo wa kutoa ushindani mkubwa dhidi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kwenye chaguzi zote.
Miaka ya hivi karibuni, chama hicho kimekuwa kikikumbana na mashambulizi kila msimu wa uchaguzi ambapo wagombea wake wengi wameenguliwa kwenye chaguzi za serikali za mitaa za mwaka 2019 na 2024 pamoja na uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
Katika uchaguzi wa mwaka huu, Chadema kiliazimia kutoshiriki uchaguzi huo huku kikishinikiza kuzuia uchaguzi kufanyika hadi pale mabadiliko ya msingi kwenye mfumo wa uchaguzi ikiwemo Tume ya Uchaguzi yatakapofanyika.
Hata hivyo, mwaka 2025 unaelekea ukingoni huku chama hicho kikiwa na kesi mahakamani na viongozi wake wakisimamishwa huku kukiwa na zuio la kutumia mali za chama kutokana na shauri lililo mahakamani.
Katika makala haya, Mwananchi linaangazia mfululizo wa mashambulizi ya ndani na nje dhidi ya Chadema tangu chama hicho kilipopata uongozi mpya kabla ya kuanza kwa songombingo hizo zinazolenga kukiua au kukidhoofisha chama hicho.
Mashambulizi dhidi ya Chadema yalianza muda mfupi baada ya kumalizika kwa uchaguzi wa ndani, Januari 21, 2025, kati ya aliyekuwa mwenyekiti, Freeman Mbowe na makamu wake, Tundu Lissu ambaye alishinda uchaguzi huo kwa tofauti ndogo ya kura.
Baada ya ushindi huo, Lissu alianza kazi kwa kusimamia azimio la Kamati Kuu ya Chadema la kuzuia uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025 usifanye kupitia kampeni yao ya ‘No reforms, no election’ (bila mabadiliko, hakuna uchaguzi).
Lissu na viongozi wengine waandamizi wa chama hicho walianza kuzunguka nchi nzima na kukutana na makundi tofauti ya wadau kueleza maana ya kaulimbiu yao na dhamira ya kutaka uchaguzi mkuu usifanyike hadi pale mabadiliko ya msingi yatakapofanyika.
Aprili 19, 2025, akiwa katika ziara yake Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Lissu alikamatwa na Jeshi la Polisi na kupelekwa Dar es Salaam ambapo alifunguliwa kesi ya uhaini na uchochezi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Baadaye, shauri hilo lilihamishiwa Mahakama Kuu ya Tanzania ambako inaendelea hadi sasa huku kiongozi huyo wa Chadema akiendelea kushikiliwa mahabusu katika gereza la Ukonga wakati kesi hiyo ikiendelea.
Kukamatwa kwa kiongozi huyo wa chama kwa takribani miezi minane sasa kunatajwa kukipunguzia nguvu chama hicho kwani yeye ndiyo amebeba dira ya chama na sauti yake ina mamlaka katika utekelezaji wake tofauti na wengine.
Februari 18, 2025, katika hali isiyotarajiwa, kada wa Chadema, Lebrus Mchome, alimwandikia barua Msajili wa Vyama vya Siasa akilalamikia uteuzi wa viongozi wa kamati kuu na sekretarieti, uliofanywa na Baraza Kuu analodai akidi haikukamilika Januari 22, 2025.
Aprili 8, 2025, Mchome aliandika barua nyingine kwa Msajili, akisisitiza kuhusu barua yake ya awali, akitaka uongozi wa juu wa Chadema kubatilishwa kwa sababu haukuchaguliwa kihalali kwa sababu akidi haikutimia kwenye kikao cha Baraza kuu lililowathibitisha viongozi hao.
Viongozi wanaolalamikiwa ni Katibu Mkuu, John Mnyika, Amani Golugwa (Naibu Katibu Mkuu – Bara) na Ally Ibrahim Juma (Naibu Katibu Mkuu – Zanzibar.
Pia, aliwataja wajumbe wa kamati kuu walioteuliwa na Lissu na kuidhinishwa na Baraza Kuu – Godbless Lema, Rose Mayemba, Salma Kasanzu, Hafidh Ally Saleh na Dk Rugemeleza Nshala.
Hata hivyo, Machi 25, 2025 akifungua mafunzo ya uongozi kwa viongozi wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha) na Baraza la Vijana Chadema (Bavicha) Kanda ya Kusini, Mnyika alisema kikao cha baraza kuu cha Januari 22, 2025 kilifuata utaratibu unaotakiwa.
Alisema akidi iliyotumika ni asilimia 50 ya wajumbe, kwa kuwa kikao hicho hakikuwa cha kiuchaguzi wala kupitisha sera wala katiba, ambacho uhitaji akidi ya asilimia 75 ya wajumbe.
Hata hivyo, maelezo hayo hayakuwa utetezi mbele ya Msajili aliiandikia barua Chadema akiitaka imjibu Mchome. Pia, aliiandikia Chadema barua akiitaka ikajieleze kwake kuhusu tuhuma zilizoibuliwa na Mchome, jambo ambalo walilifanya na akawataka waitishe kikao kingine na kuwaidhinisha upya.
Katika hatua nyingine, wajumbe wa bodi ya wadhamini walifungua shauri mahakamani akiishitaji Bodi ya Wadhamini ya Chadema pamoja na Katibu Mkuu kwa madai kwamba hakuna mgawanyo sawa wa mali za chama kati ya Zanzibar na Bara.
Kesi hiyo ya madai namba 8323 ya mwaka 2025 ilifunguliwa na Makamu Mwenyekiti mstaafu wa Chadema, Said Issa Mohamed na wajumbe wawili wa Bodi ya Wadhamini wa Chadema kutoka Zanzibar, Ahmed Rashid Khamis na Maulida Anna Komu.
Wadai wanadai kumekuwa na mgawanyo usio sawa wa mali za chama na rasilimali za kifedha kati ya Tanzania Zanzibar na Tanzania Bara, kinyume na Sheria ya Vyama vya Siasa na Katiba ya chama hicho.
Hatima ya uhalali wa kesi ya mgogoro huo wa rasilimali usio sawa kati ya Tanzania Bara na Zanzibar inayokikabili Chadema, sasa itajulikana Februari 2026, Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam itakapoamua pingamizi dhidi ya kesi hiyo.
Katika mwendelezo wa sintofahamu hiyo, Msajili alichukua hatua ya kuwasimamisha wanaojifanya kuwa ni viongozi kufanya shughuli za kisiasa kwa mujibu wa kifungu cha 21E cha sheria ya vyama vya siasa.
Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa iliwasihi wananchi, wadau mamlaka na taasisi zote za Serikali na binafsi, kutowapa ushirikiano na huduma viongozi wa Chadema kwa kuwa haiwatambui.
Mbali na hilo, Ofisi ya Msajili iliamua kusitisha kuwapa ruzuku Chadema hadi watakapotekeleza maelekezo ya Msajili, kwa sababu chama hicho hakina viongozi wanaoweza kusimamia mapato, matumizi na mrejesho wa fedha hizo za umma.
Viongozi wanaolalamikiwa na msajili na kuamua kuwaweka kando hadi Baraza Kuu jingine litakapoitishwa ni Katibu Mkuu, John Mnyika, Amani Golugwa (Naibu Katibu Mkuu – Bara) na Ally Ibrahim Juma (Naibu Katibu Mkuu – Zanzibar).
Wengine ni wajumbe wa kamati huu Godbless Lema, Rose Mayemba, Salma Kasanzu, Hafidh Ally Saleh pamoja na Dk Rugemeleza Nshala, ambaye aliteuliwa kuwa mwanasheria mkuu wa chama hicho.
Pigo jingine ambalo Chadema kimelipata mwaka huu ni kukimbiwa na makada wake hasa waliokuwa viongozi waandamizi, waliotimkia Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Mei 7, 2025, kwa kile walichodai kuwa ni kutafuta mustakabali wao kisiasa.
Mgawanyiko huo ulianza baada ya Mbowe kushindwa kwenye uchaguzi wa chama wa Januari 21, 2025. Baadhi ya viongozi waliokuwa wakimuunga mkono walidai kutengwa na uongozi mpya, hivyo wakaamua kukihama chama hicho.
Viongozi hao, walioongoza kundi la G55, ni pamoja na Salum Mwalimu ambaye sasa ndiyo Katibu Mkuu wa Chaumma, Benson Kigaila (Naibu Katibu Mkuu – Bara wa Chaumma), John Mrema (Mkurugenzi wa Mawasiliano) na Julius Mwita aliyekuwa katibu wa Sekretarieti ya Chadema.
Viongozi hao pamoja na wanachama wengine walikihama chama chao na kwenda Chaumma huku wakieleza kwamba uamuzi huo umechochewa na viongozi wapya kuwatenga kwa sababu walikuwa upande wa Mbowe wakati wa uchaguzi wa ndani.
Licha ya kwamba uongozi mpya uliwapuuza uamuzi wa makada hao kukihama Chadema, ni wazi kwamba hilo lilikuwa pigo kwa chama hicho kwani kiliwapoteza wanachama ambao wameweza kukisaidia kupiga hatua mbele.
Kaimu Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika anasema mwaka huu umekuwa kifungo cha kisiasa na kidemokrasia siyo tu kwa Chadema, bali kwa nchi nzima kwani demokrasia imefungwa na uchaguzi kuporwa.
“Huu ni mwaka ambao Watanzania tumeendelea kupoteza fursa ya kufanya mabadiliko ya kikatiba na kisheria ili kuwezesha nchi kuwa na chaguzi huru na za haki. Umekuwa ni mwaka wa giza na kilele cha giza hilo ni mauaji ya Oktoba 29, 2025,” anasema Mnyika.
Hata hivyo, Mnyika anasema wamefarijika mwaka huu kuona mapambano ya kudai haki yamevuka mipaka ya kichama ya Chadema pekee bali yamekuwa ni mapambano ya wananchi kutafuta haki.
Mnyika anasema asasi za kiraia, taasisi za dini, kundi la vijana (Gen Z), wote wanaimba wimbo wa haki, jambo ambalo linawapa faraja ya kwamba sasa umma wa Watanzania umeamka katika kudai haki zao.
Kiongozi huyo wa Chadema anasema nguvu sasa zielekezwe katika kutafuta mabadiliko ya Katiba, kutaka Chadema iwe taasisi huru ili kiendelee kupigania demokrasia na haki za wananchi, kuhakikisha uchaguzi mkuu unarudiwa ili wananchi wachague viongozi wanaowataka.
“Haukuwa mwaka wa Chadema peke yake kuumia, ulikuwa ni mwaka wa Watanzania kuumia, kwa hiyo tunapotoka kwenye hayo maumivu, madhila na madhara, halipaswi kuwa jambo la Chadema peke yake, linapaswa kuwa jambo la wadau wote,” anasema.
