Kijana adaiwa kumbaka, kumjeruhi bibi yake

Mbozi. Obadia Mpenzu (22), mkazi wa Kitongoji cha Majimoto, Kijiji cha Nanyala, wilayani Mbozi, mkoani Songwe anashikiliwa na Jeshi la Polisi akituhumiwa kumbaka na kumjeruhi bibi yake mwenye miaka 80.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Augustino Senga, amekiri kumshikilia mtuhumiwa.

Akizungumza na Mwananchi, Mwenyekiti wa Kijiji cha Nanyala, Maneno Mwambunga, amesema tukio hilo lililotokea usiku wa Desemba 8, 2025.

Amesema mtuhumiwa alitekeleza tukio hilo la ukatili baada ya kufika nyumbani kwa bibi yake saa nne usiku wa Desemba 8, wakati mume wa bibi huyo akiwa kilabuni.

Mwambunga amesema baada ya tukio hilo, mtuhumiwa alikimbilia kusikojulikana.

Amesema uongozi wa kijiji ulianzisha msako uliodumu hadi saa tano asubuhi ya Desemba 9, 2025, mtuhumiwa alipokamatwa akiwa amejificha porini.

“Mtuhumiwa alikutwa akiwa amejificha porini na afya yake ilionekana kuwa dhaifu, akitapika. Inadaiwa alikuwa amekunywa sumu kwa lengo la kujitoa uhai kwa kujutia kitendo alichofanya,” amesema.

Amesema mtuhumiwa alipelekwa Kituo cha Afya Nanyala kabla ya kukabidhiwa polisi kwa hatua zaidi.

Kamanda Senga amesema afya ya mtuhumiwa inaendelea vizuri baada ya kupatiwa matibabu na uchunguzi utakapokamilika atafikishwa kwenye vyombo vya sheria.