KIUNGO Moussa Balla Conte wa Yanga, ametumiwa salamu nzito kutoka kwa kocha wake wa zamani, Alexander Dos Santos ambazo kama atazitumia anaweza kurudisha heshima ndani ya mabingwa hao wa soka nchini.
Santos, kocha Mreno aliyefanya kazi na Conte akiwa CS Sfaxien ya Tunisia, ameliambia Mwanaspoti, kuwa Conte sio mchezaji anayetakiwa kukubali kirahisi kwamba hawezi kuichezea Yanga, kwani ana kipaji kikubwa, ila anachotakiwa ni kupigana vita hiyo na atashinda.
Samtos anayeinoa kwa sasa AS FAR Rabat ya Morocco alisema Conte anatakiwa kufanyia kazi ubora ambao wenzake anaoshindana nao namba wanamzidi kisha kuongeza ratiba binafsi ya mazoezi ili aweze kurudisha nafasi.
Kocha huyo raia wa Ureno, alisema Conte ni kiungo wa kisasa ambaye kama atajipanga sawasawa na kurudisha nafasi yake, Yanga itapata makubwa zikiwemo pasi zake za mbali na uwezo wa kukaba kwa nguvu.
“Ukiniambia Conte hawezi, nitachelewa kukukubalia, huyu ni mtu niliyefanya naye kazi…nadhani amepitia mwanzo mgumu tu, nilipata nafasi ya kuongea naye nilipokuja hapo Tanzania, lakini haikuwa sana ila nilimuuliza kwanini hachezi,” alisema Santos na kuongeza:
“Kitu ninachofahamu ni kwamba Conte ni kiungo mzuri anajua kupiga pasi, pia anajua kukaba, kama ameonekana hawezi Yanga nadhani ni suala la kujiamini tu na akifanikiwa kuwa na ratiba ngumu na kali ya mazoezi binafsi anaweza kurudi katika kiwango alichonacho.
“Kwa viungo wanaocheza Yanga mbele ya mabeki wa kati, yale yote Conte anaweza kuyafanya sijajua ni kipi kimemkuta hadi anakuwa katika hali ile, lakini anaweza kurudisha ubora, makocha wake wanaweza kuongea naye na wakamjenga.”