KONA YA MALOTO: Tanzania inamhitaji Mungu

Yupo mtu, kwa kutafsiri kichwa cha makala, anaweza kuuliza: “Lini Watanzania hawakumhitaji Mungu zaidi?” Jawabu ni kwamba hiyo ni lugha ya picha, kujenga tafsiri kuwa muktadha ulio mbele unazidi uwezo wa kawaida wa binadamu.

Mbona ni mengi huambizana kuwa “yapo juu ya uwezo wetu?” Basi ndivyo ilivyo. Mungu anahitajika wakati wote, ila zipo nyakati huhitajika zaidi, maana bila yeye, wanadamu hawawezi kuvuka.

Ule wakati wa Nuhu na Safina lake, Mungu alihitajika zaidi ili kumwezesha Nuhu kubaki salama na watu wazuri, wenye hofu ya Mungu, kisha jeuri, wabishi na waasi waangamie.

Zama za Luttu, Mungu alihitajika zaidi ili watu waovu wapate adhabu inayostahili kwa kugeuzwa miamba ya chumvi. Mungu alihitajika zaidi kumwezesha Musa kuvuka Bahari ya Sham kwa kuigawa katikati kupitia fimbo ya maajabu ili yeye na wana wa Israel wasikamatwe na Firauni.

Tanzania inahitaji Mungu zaidi kipindi hiki. Si kwa matendo makubwa kama Yona kuishi kwenye tumbo la samaki au Mtume Muhammad na swahaba wake, Aboubaqar Swidiq kuokolewa na buibiui mbele ya makafir, walipokuwa wanakimbia Mecca kwenda Medina, Mungu anayehitajika kwa

Watanzania ni kwa ajili ya upatanisho. Dhahiri, hili limekuwa juu ya uwezo wa wanadamu.

Ndani ya mitandao ya kijamii, hoja na mitazamo vimebeba hisia na matarajio ya lazima kuliko Utanzania. Inatakiwa ndani ya mitandao ya kijamii, kuwepo na hisia za Utanzania kuliko misimamo ya kulazimisha.

Hoja za mitandao ya kijamii, kwa upande mmoja, ni kutaka Rais Samia Suluhu Hassan, aondoke madarakani. Wanajadili kwa shinikizo na msisitizo utadhani kumwondoa Rais madarakani ni kama kubadili chaneli ya televisheni. Unabonyeza namba kwa rimoti, unahamia mpya.

Matamko, ushabiki na misimamo yenye shinikizo la kumng’oa Rais madarakani, tena Rais mwenyewe ana utii kamili wa dola, ni Amiri Jeshi Mkuu anayepokea utii wa vyombo vyote, kuondoka kwake haiwezi kuwa rahisi. Wanamapinduzi wa mitandaoni wanatakiwa watambue hilo.

Angalau wangefahamu kuwa kumtoa madarakani Rais anayepokea utii kamili wa vyombo vya dola, inatakiwa kazi kubwa kufanyika kwa kushawishi vyombo vitambue usahihi wao kwa Rais hafai. Ushawishi wao uzingatie kuwa vyombo vina macho na mikono kuliko hisia na maoni ya mitandaoni.

Rais anaongoza majesho ambayo yote, kila moja lina kitengo cha intelijensia. Rais anaongoza Idara ya Usalama wa Taifa, ambayo ukiacha ulinzi wa viongozi, majukumu yake mengine yote ni ya kiintelijensia kwa asilimia 100.

Sasa, vyombo hivi vinajua mengi, tena yenye ushahidi kuliko wanaohamasisha maoni mitandaoni.

watu huamini kwamba hoja za mitandaoni nyingi zinatoka kwenye vyombo. Kama ingekuwa kweli, basi tungeshuhudia mengi yenye ushahidi mitandaoni. Hata hivyo, mitandaoni kuna shutuma, tuhuma na hisia kuliko ushahidi.

Vyombo gani vinavyotoa hayo?

Kuna jambo kubwa halipo sawa. Jambo hilo ni mwamko wa kutaka mapinduzi kwa hisia na tuhuma zisizo na ushahidi. Jambo hilo ni kutofahamu hatari ya kushinikiza mapinduzi ya kiraia dhidi ya Rais mwenye mamlaka na utii kamili wa kidola.

Jaribio lolote la kumng’oa ni kukaribisha mapambano baina raia na majeshi. Je, hapo nani anahitajika zaidi? Ni Mungu tu!

Wasiojua hatari ya mapinduzi ya Rais mwenye mamlaka kamili ya kidola, anayepokea utii wa asilimia 100 wa vyombo vya ulinzi na usalama, ndiyo wanaoshangaa watu kupoteza maisha Oktoba 29, 2025.

Udhibiti wa uasi wa watu wanaovamia mali za watu na kupora. Kuharibu mali za watu na za umma. Wenye lengo la kusimamisha shughuli za nchi. Wanaopayuka Rais atoke. Udhibiti wake lazima utaongozwa na nguvu nyingi. Matumizi yoyote makubwa ya kijeshi, huleta matokeo ya vifo.

Rais Samia ametaka yawepo maridhiano. Wito huo unakataliwa na wanamapinduzi wa mitandaoni. Rais Samia ameahidi kupatikana kwa Katiba Mpya kabla hajaondoka madarakani.

Hilo haliwatulizi wanamapinduzi wa mitandaoni. Rais Samia ameunda Tume ya Uchunguzi kwa ajili ya matukio ya Oktoba 29, 2025, nayo hawaitaki.

Jumuiya ya Madola iliteua Kamati ya Upatanishi, ambayo kiongozi wake ni Rais wa zamani wa Malawi, Lazarus Chakwera, nayo pia wanamapinduzi wa mitandaoni walisema hawaitaki. Jiulize sasa, kipi ambacho wanakitaka? Je, ni kweli sauti zao kwamba Rais Samia aachie ngazi, aking’atuka watatulia?

Vipi Rais Samia akitangaza kuachia ngazi, wao wakaleta visa vipya? Inatakiwa kujiuliza maswali mengi dhidi ya wanamapinduzi wa mitandaoni.

Mpaka sasa kiini cha vuguvugu lao hakijawa wazi. Wanamtaja Rais Samia, wakati huohuo wanamzunguzia Rais mstaafu, Jakaya Kijwete, ambaye aliachia ngazi miaka 10 iliyopita.

Vyombo vinajua kuwa kumsema Kikwete ndiye anaongoza nchi ni uongo mkubwa. Je, chuki inayopandikizwa kwa wananchi kuhusu Kikwete, na kumshushia hadhi Rais Samia, ambayo vyombo vinajua zaidi ukweli wake. Je, vyombo vinaweza kukaa kimya kuacha nchi ivurugike kwa simulizi za utunzi mitandaoni?

Hatari nyingine kubwa ni kuwa jumuiya za ndani na nje zinakaririshwa kwamba vuguvugu la sasa dhidi ya Serikali linaletwa na vijana kundi rika la Generation Z (Gen Z). Hata hivyo, vinara (ringleaders), wanaohamasisha vuguvugu, hawapo kundi rika la Gen Z. Ni watu wazima. Tena, asilimia kuwa wapo nje ya nchi, na hawakushiriki kimwili Oktoba 29.

Ringleaders wa vuguvugu linaloitwa la Gen Z Tanzania, wataendelea kuhamasisha ghasia kwa sababu hawakukutana na madhara ya moja kwa moja Oktoba 29. Wapo salama. Kaz yao ni kuhamasisha tu.

Vijana wanajenga chuki. Wanaingia barabarani. Wanachoma nchi yao.

Ona sasa, chokochoko zimeleta hadi udini. Zinachokonoa tunu ya nchi, Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, ulioleta Tanzania. Ni kitu kikubwa mno kisichoonekana. Ni hofu, utayari wa Katiba Mpya unaweza kufifishwa na mifarakano. Maridhiano yakashindikana kwa sababu ya chuki. Mungu ndiye anahitajika zaidi.