Mbeya. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia Marry Timotheo, kwa tuhuma za mauaji ya mtoto wake, Scola Mwaba, kisha kutupa mwili wake shambani jirani na nyumba anayoishi.
Mwamba (10) alikuwa mwanafunzi wa darasa la nne katika Shule ya Msingi Ngonde.
Tukio la mauji linadaiwa kutokea jana Desemba 9, 2025 saa 6:30 mchana katika Kijiji cha Garijemb, Kata na Tarafa ya Tembela, wilayani Mbeya.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga katika taarifa kwa umma leo Desemba 10, amesema mtuhumiwa anadaiwa kumshambulia kwa kitu kizito kichwani mtoto wake kwa kile kinachoelezwa kuwa amezidi utukutu.
“Tukio hilo linadaiwa kutokea Desemba 9, baada ya mama mzazi wa marehemu kumuadhibu kwa kumpiga na kitu kizito kichwani kwa madai ya kuzidi utukutu, kisha mwili wake kutupwa shambani jirani na nyumba wanayoishi,” amesema.
Amesema jeshi hilo pia linamshikilia Sharifa Nzalanje, ambaye ni jirani wa mtuhumiwa akidaiwa kushirik tukio hilo.
Kamanda Kuzaga amesema uchunguzi wa awali umebaini chanzo cha tukio hilo ni kujichukulia sheria mkononi kwa kumuadhibu mwanaye kwa kumpiga hadi kufa.
“Baada ya kubaini amefariki dunia mama mzazi kwa kushirikiana na jirani yake walikwenda kutupa mwili wake shambani,” amesema.
Amesema watuhumiwa wanaendelea kushikiliwa na upelelezi ukikamilika hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Kamanda Kuzaga ametoa wito kwa wazazi na walezi kuacha kujichukulia sheria mkononi kwa kuadhibu watoto, badala yake watoe adhabu za kuwarekebisha kwa kuwafundisha mienendo ya maadili mema.
Katika hatua nyingine ameitaka jamii kuwa mabalozi wa kutoa taarifa za wazazi na walezi wanaofanya vitendo vya ukatili dhidi ya watoto ili hatua za kisheria zichukuliwe ili kuepuka madhara yanayoweza kuwapata, ikiwamo kupoteza maisha au ulemavu wa kudumu.
Mkazi wa Izumbwe wilayani Mbeya, Fredy Daniel ameiomba Serikali kutoa elimu ya athari za kisaikolojia kwa wanawake, akieleza wengi wao huingiza watoto kwenye chuki za migogoro ya wenza wao na kuleta madhara.
“Tunashuhudia migogoro ya wazazi kuchangia watoto kutwishwa mizigo kwa kuadhibiwa pasipo sababu. Tuombe elimu itolewe kuanzia ngazi za serikali za vijiji ili kuokoa kizazi cha baadaye,” amesema.
