BAADA ya kukosekana uwanjani kwa msimu mmoja, beki wa kati wa Pamba Jiji, Abdulmajid Mangalo ameonekana kurejea kwa kasi mpya uwanjani akiisaidia timu hiyo kuvuna pointi 12, huku akitoa mwelekeo wa chama hilo katika Ligi Kuu Bara.
Mangalo aliyewahi kutesa na timu kadhaa ikiwamo Biashara United na Singida Black Stars, alijikuta nje ya uwanja kufuatia jeraha la goti lililomfanya kutoonekana uwanjani baada ya kufanyiwa upasuaji.
Msimu huu mchezaji huyo ameibukia Pamba Jiji ya jijini Mwanza, ambapo tayari amecheza mechi tano sawa na dakika 450 na kusaidia timu hiyo kushinda michezo mitatu na sare mbili, na kuiweka katika nafasi ya tatu kwenye msimamo ikiwa na pointi 16.
Katika michezo hiyo, Pamba Jiji imefungwa bao moja na kufunga manane ikionyesha kuwa na ukuta imara chini ya nahodha huyo wa zamani wa Biashara United na kujiweka katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi.
Mangalo ameliambia Mwanaspoti kuwa, licha ya kupotea msimu mzima, lakini hajapoteza chochote kwa kuwa aliamua kukaa nje kwa ushauri wa watalaamu ili anaporejea uwanjani aweze kuendeleza makali yake.
Alisema kwa mwanzo huo alioonyesha ni sehemu ya mwendelezo wa ubora wake na matarajio yake ni kuiona Pamba Jiji ikiendelea kufanya vizuri kwa kutoruhusu mabao.
“Zilikuja ofa nyingi, ila niliamua kuzitema kwa kuwa sikutaka kuchukua cha mtu halafu niende kukaa benchi. Nilifuata maelekezo ya madaktari kuhakikisha napumzika ili nikirejea uwanjani nifanye vizuri,” alisema.
“Kwa maana hiyo haya ni matokeo ya uvumilivu wangu. Nashukuru tunashirikiana vyema wachezaji kila mmoja anatimiza wajibu wake kuipambania Pamba Jiji. Tunataka nafasi nne mwisho wa ligi.”