Marufuku magari binafsi, bodaboda barabara za mwendokasi

Dar es Salaam. Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart) umepiga marufuku vyombo vyote vya moto isipokuwa mabasi ya ‘mwendokasi’ kutumia miundombinu ya mabasi yaendayo haraka kuanzia leo Jumatano, Desemba 10, 2025.

Marufuku hiyo imetangazwa leo Jumatano na Dart kupitia taarifa kwa umma ya Kitengo cha Mawasiliano cha Uhusiano kwa Umma Dart.

“Dart inasisitiza vibali vyote vilivyowahi kutolewa vimesitishwa kuanzia Desemba 10, 2025,” imeeleza taarifa hiyo na kuongeza:

“Doria na udhibiti vitaimarishwa ili kuhakikisha agizo hili linazingatiwa. Hatua za kisheria zitachukuliwa kwa yoyote atakayekiuka agizo hilo.”

Marufuku hiyo imetangazwa kipindi ambacho kumekuwa na vyombo vya moto hususan magari ya Serikali na bodaboda kupita kwenye barabara hizo.

Novemba 25, 2025, Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega alitoa ruhusa kwa magari ya abiria kuanza kutumia barabara ya mwendokasi awamu ya tatu inayoanzia katikati ya jiji la Dar es Salaam kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere hadi Gongo la Mboto kwa lengo la kupunguza msongamano wa magari katika barabara hiyo ya Nyerere.

Ulega alitoa ruhusa baada ya kukagua utekelezaji wa mradi huo ambao umekamilika kujengwa kwa asilimia 100 na kusisitiza umuhimu wa barabara hiyo kuendelea kutumika hadi hapo mtoa huduma kwa ajili ya kuleta mabasi katika barabara hiyo atapopatikana.