Mashauri 15 ACT Wazalendo yatajwa mahakamani leo

Unguja. Mashauri 15 kati ya 17 ya Unguja yametajwa katika Mahakama Kuu ya Zanzibar yanayopinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 29, mwaka huu huku mashauri mawili ya Jimbo la Makunduchi na Kiembesamaki kutajwa kati ya Desemba 14 au 15.Β 

Mashauri hayo yamefunguliwa na wanachama 15 wa Chama cha ACT Wazalendo na waliokuwa wagombea wa nafasi za ujumbe wa Baraza la Wawakilishi kwenye uchaguzi Mkuu dhidi ya wasimamizi wa uchaguzi wa majimbo 15 na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar.

Mashauri hayo, yametajwa leo Jumanne Desemba 10, 2025 mbele ya Naibu Mrajisi Faraji Shomar Juma katika Mahakama hiyo iliyopo Tunguu, Mkoa wa Kusini Unguja.

Akitoa maombi mahakamani hapo, Wakili kutoka upande wa walalamikaji, Rajab Abdallah Rajab wameiomba mahakama kupitia majibu ya mashauri yaliyoletwa upande wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, kwani mashauri hayo yalikuja leo asubuhi kwa ajili ya kutajwa.Β 

Hivyo, hawajapata nafasi ya kuyapitia majibu hayo kwa lengo la kuendelea na mambo mengine ya kisheria mahakamani hapo.

Kabla Mahakama kuridhia ombi hilo, Wakili kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar,Β  Mbarouk Suleiman Othman alikubali kutoa majibu hayo na kutoa angalizo, kuwa majibu hayo yasitumike kupitia pingamizi ambazo tayari zimewasilishwa katika utetezi wao.

“Mheshimiwa Naibu Mrajisi, Sisi hatuna tatizo na kupewa majibu hayo lakini tunaomba wasije wakayatumia kupitia pingamizi tulizowasilisha,” amesema Mbarouk

Akitoa ufafanuzi wa hilo,Β Wakili Rajab amesema wanachohitaji ni kupitia majibu ya Serikali ili kutoa majibu yao (walalamikaji) ndipo mashauri yaendelee.

Hivyo, Mahakama imejiridhisha kuwa upande wa wajibu na wamekabidhiwa nyaraka za kufungulia kesi kwa mujibu wa sheria.

Pia, Mahakama imeagiza kuwa walete maombi ili kupatiwa nakala za majibu hayo yaliyowasilishwa na wajibu maombi pamoja na hati za kiapo kinzani.

Kwa hivyo, Naibu Mrajisi ameahirisha mashauri hayo hadi Desemba 18, 2025 saa 3:00 asubuhi kwa ajili ya kutajwa tena.

Naibu Mrajisi amesema katika tarehe hiyo, walalamikaji wataitaarifu mahakama kama wanakusudia kuwasilisha majibu kwa majibu yalioletwa ya wajibu maombi au hatua nyengine za kimahakama zinaweza kuendelea ikiwemo kesi hiyo kupangiwa Jaji.Β 

Akizungumza nje ya Mahakama, Mwanasheria Mkuu wa Chama hicho, Omar Said Shaaban amesema timu yao ya mawakili inazingatia ratiba na taratibu zote zilizowekwa na Mahakama.

Β “Hadi kufikia sasa tunaridhishwa na hatua zinazoendelea na tunatumia muda huu wa kuahirishwa kwa mashauri kujiandaa kwa hatua zinazofuata za kisheria,” amesema Omar.

Ameeleza kuwa, kwa kuwa mashauri hayo yapo rasmi mikononi mwa mahakama, hawatatoa maoni kuhusu ushahidi au kiini cha kesi kwenye vyombo vya habari hivyo wameomba wananchi kuheshimu utaratibu wa sheria.

Katika uchunguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 29, Chama hicho kilishinda majimbo 10 na Chama cha Mapinduzi (CCM) kikishinda majimbo 40 kati ya 50 yaliyopo Zanzibar.

Chama hicho kilifungua mashauri 25 ya kupinga matokeo hayo, 17 Unguja na nane Pemba huku mashauri mawili ya jimbo la Makunduchi na Kiembesamaki kutajwa kati ya Desemba 14 au 15.

Majimbo ambayo wameyafungulia kesi ni Malindi, Amani, Nungwi, Kijini, Bumbwini, Chaani, Mpendae, Kiembesamaki, MwanaKwerekwe, Tumbatu, Makunduchi, Pangawe, Chumbuni, Mwera, Mtoni, Welezo na Kikwajuni.