Maxime aanza na watano Mbeya City, wamo Awesu, Chasambi kutoka Simba

Baada ya kutua kikosini, Kocha Mkuu wa Mbeya City, Mecky Maxime ameanza kazi ya kusuka upya timu hiyo akihitaji huduma ya wachezaji watano wakiwamo mastaa wawili kutoka Simba ili kurejesha ari, morali na nguvu mpya.

Wachezaji hao ni Awesu Awesu na Ladack Chasambi ambao wameombwa kwa mkopo na imeelezwa tayari pande zote zimeshakubaliana na mastaa hao kutua jijini Mbeya kuanza majukumu mapya baada ya kukosa nafasi ya uhakika huko walipo.

Maxime amejiunga na timu hiyo akichukua mikoba ya mtangulizi wake Malale Hamsini aliyesitishiwa mkataba ikiwa saa chache baada ya kupoteza mechi dhidi ya Namungo.

Kipigo hicho kilikuwa ni mwendelezo wa matokeo yasiyo ridhisha baada ya awali kufungwa dhidi ya Coastal Union, Mashujaa na sare mbele ya JKT Tanzania na kipigo kwa Tanzania Prisons.

Maxime aliyewahi kuzinoa timu kadhaa ikiwamo Kagera Sugar, Mtibwa Sugar, Dodoma Jiji na Ihefu, alitambulishwa siku chache baada ya kikosi hicho kupigwa 3-0 na Simba katika mechi ya Ligi Kuu Bara iliyochezwa Desemba 7, 2025 kwenye uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Salaam.

Kwa sasa timu hiyo iliyopo nafasi ya 13 katika msimamo wa Ligi Kuu Bara ikikusanya pointi nane baada ya mechi 10, ipo mapumziko kwa takribani siku kumi, ambapo inatarajia kurejea kambini mwishoni mwa mwezi Desemba kujiandaa na mwendelezo wa Ligi Kuu kuwafuata Mtibwa Sugar, Januari 22, 2026.

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Mbeya City, John Jerome amesema tayari wamepokea ripoti ya Maxime ikipendekeza mahitaji ya wachezaji takribani watano ili kuongeza nguvu kikosini haswa tunapoelekea dirisha dogo la usajili litakalofunguliwa Januari Mosi, 2026

Amesema baada ya kupokea ripoti hiyo, uongozi umeanza kuifanyia kazi, akieleza kuwa wapo tayari kuvunja kibubu kuhakikisha wachezaji waliotajwa wanapatikana na kuvaa uzi wa City, akieleza matokeo yaliyopita hayajawafurahisha.

“Amehitaji kuongeza nguvu maeneo matatu, beki, kiungo na straika, lakini amewataja mastaa anaowataka na sisi uongozi tunafanyia kazi ripoti hiyo ili kufikia malengo.

“Ni kweli wachezaji wanaohitajika wote wana mikataba na timu zao, kinachoenda kufanyika ni kuvunja kibubu kuwapata nyota hao ambao tunaamini wataturejeshea heshima yetu kuanzia mechi zijazo,” amesema Jerome.