Mtazamo tofauti vyama vya siasa, sherehe za Uhuru

Dar es Salaam. Wakati ACT Wazalendo na CUF, vikidai maadhimisho ya kusheherekea miaka 64 ya Uhuru wa Tanganyika hayakuwa huru, kutokana na ulinzi kuimarishwa kila kona, baadhi ya vyama vya upinzani vimesifu ulinzi na usalama kutimiza wajibu wao.

Desemba 9 ya kila mwaka, Tanzania BaraΒ  inasheherekea Uhuru wake, lakini jana ilikuwa tofauti kwa Watanzania kusalia katika makazi yao. Utofauti huo ulichochewa na kauli ya Serikali kuwataka wananchi washerehekee sikukuu hiyo kwa kutulia majumbani mwao.

Pia, Serikali iliwataka wananchi kusalia kwenye makazi yao, kama hawatalazimika kwenda kwenye shughuli zao, amri iliyotokana na vuruguvugu kwa kile kilichoitwa maandamano yasiyo na ukomo.

Maandamano hayo yaliyopangwa kupitia mitandao ya kijamii, ni mwendelezo wa yale yaliyofanyika Oktoba 29, wakati wa uchaguzi na kuzua vurugu, zilizosababisha vifo vya watu, wengine kujeruhiwa na mali za umma na za watu binafsi kuharibiwa.

Katika taarifa yake kwa umma, Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo (bara),Isihaka Mchinjita ameeleza kuwa Desemba 9, ilikuwa siku ya kusherehekea miaka 64 ya Uhuru wa Tanganyika, lakini hakukuwa na uhuru kwa Watanzania kutokana na hatua zilizochukuliwa na vyombo vya dola.

β€œHakika siku ambayo ilipaswa kuashiria uhuru lakini Watanzania hawakuwa huru kufuatia hatua zilizochukuliwa na dola kudhibiti uwezekano wa kutokea maandamano yaliyotangazwa na wanaharakati.”

Katika taaarifa hiyo, Mchinjita amedai kuwa maandamano ya amani yaliyopangwa yalilenga kudaiΒ  haki kwa waathiriwa wa ghasia baada ya uchaguzi na uwajibikaji kwa waliohusika. Hata hivyo, Serikali ilipiga marufuku.

Desemba 5,2025 polisi ilipiga marufuku maandamano hayo ikidai yamekosa sifa za kisheria kufanyika kwa mujibu wa Katiba. Kama hiyo haitoshi leo Jumatano, Desemba 10, polisi imewaonya wanaopanga kufanya maandamano hayo kwa mara nyingine baada ya kushindikana jana.

Wakati Mchinjita akieleza hayo, Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Bara, Magdalena Sakaya amesema ni kweli jana ilikuwa siku ya Uhuru wa Tanganyika, lakini Watanzania waliambiwa wakae kwenye makazi yao.

β€œKila sehemu kulikuwa na vyombo vya ulinzi na usalama, huku wanajeshi, kule polisi barabarani, ni kweli watu walinyimwa uhuru, siku ya Uhuru. Kila mmoja alidhibitiwa alipo, sasa huwezi kumaliza tatizo…,” amesema Sakaya.

Sakaya amesema Serikali haikuwa sawa ilichokifanya jana badala yake, ilipaswa kuwaacha watu kuandamana, lakini kwa kufuata taratibu zote pasipo kubeba silaha zozote zikiwemo za jadi.

β€œNingekuwa na mamlaka, ningeruhusu maandamano hayo yawepo na polisi iwalinde, lakini waandamanaji wasibebe silaha ya aina yoyote ila wabebe mabango, Polisi ingewalinda waandamane hadi wanakotaka kwenda ili kusikiliza madai yao,” ameeleza.

Sakaya ambaye ni mbunge wa zamani wa Kaliua mkoani Tabora, amesema hatua hiyo ingesaidia kutuliza presha ya watu kitaifa, lakini pia ingewezesha viongozi kusikiliza ujumbe watu walioandamana na Taifa lingetulia.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Ada -Tadea, Juma Ali Khatib amewapongeza Watanzania kwa utulivu walionyesha jana wakati wa maadhimisho ya miaka 64 ya Uhuru wa Tanganyika, sambamba na kutii maelekezo ya Serikali ya kutotoka kwenye makazi yao.

β€œHatua zilizochukuliwa na Serikali zilikuwa sahihi na mwafaka kwa mustakabali wa kuimarisha ulinzi na usalama. Nawapongeza Watanzania wakiwemo vijana wameelewa hakuna jambo zuri kama amani, bila kuvisahau vyombo vya ulinzi na usalama kutimizi wajibu wao,”

β€œNiwaombe Watanzania tuendelee kushikamana na kwa maslahi mapana ya nchi yetu, katika miaka 64 Tanzania imepiga hatua kubwa sana. Tulikotoka, hapa tulipo kuna maendelea makubwa, kiuchumi, kisiasa na kielimu,” amesema Khatib.

Khatib amewataka Watanzania kufungua macho na kuendelea kuwa wazalendo, kushikamana na Serikali hasa katika kipindi hiki kinachopaswa kuilinda Tanzania kwa nguvu zote.

β€œKilichofanyika jana (Desemba 9), kimetokana na tishio lililokuwapo la maandamano, hivyo Serikali imetimiza wajibu wake,” ameeleza.

Naye Mwenyekiti wa DP, Abdul Mluya amesema kilichofanyika jana (Desemba 9) ni kuimarisha ulinzi kwa Watanzania kutokana na tishio la vurugu zilizopangwa kufanyika siku ya maadhimisho ya kusherehekea miaka 64 ya Uhuru wa Tanganyika.

β€œNi kitu kizuri watu kushehekea sikukuu na familia yako nyumbani kutokana na mazingira yaliyokuwapo, maana yale yaliyopangwa hayakuwa maandamano ni vurugu, kwa sababu aliyekuwa akiyaratibu hajulikani wala anuani yake,”amesema Mluya.

Katika taarifa hiyo, ACT Wazalendo imerejea maelezo yake ya kuikataa Tume ya Kuchunguza vurugu za Oktoba 29, inayoongozwa na Jaji Othman Chande ikidai kutokuwa na imani nayo.

Mbali na hilo, chama hicho kikuu cha upinzani Zanzibar kimehimiza kuanza upya kwa mchakato wa Katiba mpya ili kuunda mfumo unaohakikisha demokrasia ya kweli, ulinzi wa haki za watu na uwajibikaji.

β€œACT Wazalendo inasimama na Watanzania katika mapambano haya. Hatutanyamaza na tunawaomba wananchi, asasi za kiraia, na washirika wa kimataifa kujiunga ili kuijenga Tanzania huru na yenye demokrasia,” amesema Mchinjita.