BAADA ya kuikanda Singida Black Stars kwa mabao 3-1 wachezaji wa TRA United wamepewa siku 10 za kupumzika kabla ya kurudi kujiandaa na mechi zijazo za Ligi Kuu Bara, Kombe la FA na Kombe la Mapinduzi 2026.
Kocha mkuu wa timu hiyo, Etienne Ndayiragije amewapa wachezaji hao mapumziko ya siku 10 akiwataka warudi kambini Desemba 17.
Ndayiragije aliyejiunga na kikosi hicho ameiongoza katika mechi nne akianza na ushindi dhidi ya Tanzania Prisons wa bao 1-0, vipigo viwili kutoka kwa JKT Tanzania 1-0 na Mtibwa Sugar iliyowalaza 2-1 na kushinda mabao 3-1 dhidi ya Singida Black Stars.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ndayiragije amesema Nwametoa mapumziko ya siku chache kutokana na kuwa katika ratiba ya kushiriki mashindano ya Mapinduzi Cup 2026 itakayofanyika Zanzibar, ni sehemu ya kuendelea kujenga timu bora na ya ushindani.
βNafikiri sababu kubwa ya kurudisha haraka timu kambini ni kutokana na ratiba iliyo mbele yetu tumepata mwaliko wa kushiriki michuano ya Mapinduzi 2026. Naamini hii itasaidia kujenga kikosi chetu kwa ajili ya kuendana na kasi ya ligi,β amesema Ndayiragije na kuongeza:
βNimefurahia kupata hii nafasi sikuwa na muda mrefu wa kukaa na timu, hivyo kupitia haya mashindano naamini nitaweza kutambua ubora na upungufu wa wachezaji sambamba na kusawazisha mapema kabla ya kurudi katika ligi, kwani ni ngumu na yenye ushindani.β
Ndayiragije amesema anatambua umuhimu wa hayo mashindano hasa timu hiyo ikiwa imetoka kupata matokeo yataendeleza hali ya ushindani kwa wachezaji wake ambao anabainisha angewaacha waende mapumziko angekuwa na mtihani wa kuanza upya.
βHaya mashindano ni fursa kwangu kama kocha, pia kwa wachezaji kuendelea kujijenga katika hali ya ushindani nina kila sababu ya kuyatumia vizuri kutengeneza timu imara na shindani ligi msimu huu ni ngumu.β
