HADI sasa kuna timu mbili tu zimesalia hazijapoteza mechi hata moja katika Ligi Kuu Bara ambazo ni Azam na Yanga, lakini kocha wa watetezi wa Ligi hiyi, Yanga kuna maagizo ameyatoa kwa mastaa wa kikosi hicho.
Kocha Pedro Goncalves amekutana na wachezaji akawapongeza kwa ukomavu mkubwa waliouonyesha katika mechi sita wakishinda nne na kutoa sare moja.
Baada ya kupongeza kwa kiwangi hicho, Pedro ameliambia Mwanaspoti, wachezaji ambao hawajaitwa timu za taifa wakiwemo Pacome Zouzoua na Mamadou Doumbia watapumzika kwa siku saba tu kuanzia jana.
Pedro amesema, wachezaji hao watakwenda kukaa na familia zao na kupumzika kabisa kabla ya kurudi kazini kuanza hesabu mpya za kuendelea na ligi mwakani.
“Nina furaha sana na wachezaji wangu kwa muda ambao nimekuwa nao, naridhika na namna wanavyoonyesha kuwa washindani katika mechi tulizocheza hadi sasa,” amesema Pedro na kuongeza:
“Tutakuwa na makundi mawili sasa, wale waliopata bahati ya kuitwa timu za taifa, tunawatakia kila la kheri huko na hawa ambao wamebaki katika timu kwa sasa.
“Hawa waliobaki tumewapa mapumziko ya siku saba wakakae na familia zao na kutafuta nguvu mpya ili tukirudi tujipange sawasawa.
“Ukweli ni kwamba hizi mechi tatu za Ligi ya ndani, zimetuonyesha kwamba Ligi ni ngumu tunatakiwa kuwa makini zaidi, lakini kuna ugumu katika mashindano ya Afrika, lakini ndio maana ya timu kubwa kama Yanga lazima kila mchezo tutafute ushindi kwa nguvu zote,” amesema Pedro raia wa Ureno.
Kocha huyo aliyeiongoza timu hiyo katika mechi sita za mashindano zikiwamo mbili za makundi ya Ligi ya Mabingwa na nne za Ligi Kuu, tangu pale alipoajiriwa Oktoba kuchukua nafasi ya Romain Folz, ameongeza kwa muda ambao ligi itasimama, watapata nafasi ya kuingiza mbinu mpya kikosini kutokana na kukosa muda hapo kabla wa kufanya hivyo.
“Wakati tunafika hapa tulikuta timu bado ipo katika mashindano, ilikuwa ngumu kidogo kubadilisha mambo mengi, lakini tutajaribu kufanya kitu tofauti kidogo kwa muda huu tutakaoupata,” amesema.
Yanga itarudia tena uwanjani Januari, mwakani, kwa mechi mbili za Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly ya Misri na Ligi Kuu Bara iliyosimama kupisha Fainali za Kombe la Maraifa ya Afrika (Afcon) 2025 zitakazofanyikia Morocco kuanzia Desemba 21 hadi Januari 18, mwakani.
Tanzania ni kati ya timu 24 zilizopo katika fainali hizo za 35 ikipangwa kundi mika na Tunisia, Nigeria na Uganda na kwa kikosi cha awali cha Taifa Stars, Yanga imetoa wachezaji saba ambao ni; Ibrahim Bacca, Israel Mwenda, Dickson Job, Bakar Mwamnyeto, Mudathir Yahya na Offen Chikola.
