Jumatano, Papa Leo wa XIV ametoa wito wa kusitisha mara moja mapigano yaliyoshika kasi upya katika mpaka wa Thailand na Cambodia, ambako mapigano ya hivi karibuni yamesababisha vifo wakiwemo raia na kuwalazimu maelfu kukimbia makazi yao.
Akihutubia waumini waliokusanyika kwa ajili ya mkusanyiko kuelekea sherehe za mwisho ya mwaka leo Jumatano Desemba 10, 2025, Papa ameeleza masikitiko yake kutokana na taarifa zinazoripotiwa kutoka eneo hilo.
“Nimesikitishwa na habari za kurejea kwa mapigano katika mpaka wa Thailand na Cambodia. Kumekuwa na vifo, wakiwemo raia, na maelfu ya watu wamelazimika kuyakimbia makazi yao. Nawaombea na kuwaunga mkono kwa sala watu hawa wapendwa.”
Ghasia hizo ni mwendelezo wa mzozo wa mpaka wa miongo kadhaa, ambapo maeneo yanayogombewa hasa yale yanayozunguka maeneo ya kihistoria na ya kitamaduni kama vile maeneo ya hekalu, yamekuwa chanzo cha mapigano ya mara kwa mara kati ya mataifa hayo mawili. Ingawa jitihada za awali za usuluhishi na diplomasia za kikanda ziliwahi kufanyika ili kutuliza hali ya mpakani, makubaliano ya kusitisha mapigano mara nyingi yamekuwa dhaifu na hivyo kuziacha jamii za eneo hilo zikiathirika tena na tena.
Historia na kiini cha mgogoro
Mgogoro wa mpaka kati ya Cambodia na Thailand ni wa kieneo kati ya nchi hizo mbili kuhusu maeneo kadhaa ya mpaka wanaoshirikiana. Mgogoro huo ulianza miaka ya 1950, muda mfupi baada ya Cambodia kupata uhuru kutoka kwa Ufaransa na awali ulijikita kwenye umiliki wa hekalu la Preah Vihear.
Kesi hiyo iliwasilishwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ), ambayo mwaka 1962 ilitoa uamuzi kwa faida ya Cambodia.
Hata hivyo, suala hilo halikufutwa moja kwa moja, kwani sehemu za mpaka kati ya nchi hizo hazijawahi kupimwa na kuainishwa kwa pamoja.
Mgogoro huo ulitulia kwa miongo kadhaa, hasa kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Cambodia, lakini uliibuka tena mwaka 2008, baada ya Cambodia kupendekeza hekalu hilo liingizwe kwenye orodha ya urithi wa Dunia ya Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (Unesco), hatua iliyosabisha maandamano ya raia wa Thailand waliopinga serikali yao kuhusu suala hilo.
Mapigano hayo yalisababisha ombi kwa ICJ kufafanua uamuzi wa 1962 na mwaka 2013, mahakama ilitoa tafsiri mpya.
Katika awamu hiyo ya mzozo, kulijitokeza pia migogoro juu ya maeneo mengine ya mpaka, ikiwemo yale yanayozunguka mahekalu ya kale ya Khmer kama vile Prasat Ta Muen Thom na Prasat Ta Krabey.