Dar es Salaam. Wakati wadau wa elimu wakionesha wasiwasi kuhusu maandalizi ya madarasa mawili yatakayohitimu elimu ya msingi mwaka 2027 na kutakiwa kujiunga na sekondari mwaka 2028, Serikali kupitia Wizara ya Elimu imeeleza kuwa inaendelea kuweka mikakati mbalimbali kuhakikisha hilo linafanyika kwa ufanisi.
Kufuatia utekelezaji wa sera mpya ya elimu, elimu msingi sasa itakuwa miaka sita hivyo wanafunzi walioanza darasa la kwanza mwaka 2022 wanatarajiwa kumaliza mwaka 2027 sambamba na wale walioanza mwaka 2021.
Hali hiyo iliibua wasiwasi wa wadau wa elimu kwamba huenda kukawa na mrundikano mkubwa wa wanafunzi katika shule za sekondari endapo Serikali haitafanya maandalizi ya kutosha kuwachukua wanafunzi wote.
Akizungumza leo Jumatano Desemba 10, wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema wizara imeanza maandalizi ikiwemo kuweka mikakati mbalimbali kuhakikisha wanafunzi wote watakaohitimu shule za msingi wanakwenda sekondari.
“Iwe ni kwenye mkondo wa jumla au mkondo wa amali tunaendelea kufanya maandalizi kuhakikisha wanafunzi wote wanajiunga na sekondari. Tumeshaandaa andiko tukiweka mikakati mbalimbali ya kufanikisha hilo.
“Tunaendelea kuangalia uwezekano wa kushirikiana na sekta binafsi hata wao wachukue wanafunzi wengine kwa gharama nafuu, pia tunaweza kuvitumia vyuo vya Veta kama shule za amali kwa sababu suala hili litakuwa kwa mwaka mmoja tu,”.
Wakati waziri akieleza hayo baadhi ya wadau wa elimu wamesema kuwa utekelezaji wa mabadiliko ya sera unahitaji maandalizi ya miundombinu, walimu na rasilimali za kutosha ili kuepusha changamoto zinazoweza kujitokeza.
Bernard Bahati ambaye ni mwalimu mstaafu , amesema Serikali inatakiwa kuanza mara moja kutathmini uwezo wa shule zilizopo na kupanga upanuzi utakaohakikisha kila mtoto anapata nafasi na hilo linapaswa kufanyika haraka iwezekanavyo kabla na sio kusubiri 2028.
“Tusisubiri hadi 2028 ndipo tuchukue hatua. Uhitaji wa madarasa, walimu na vifaa utaongezeka maradufu. Serikali inapaswa kufanya tathmini ya kina sasa ili kuepusha msongamano ambao tayari tunaushuhudia katika baadhi ya shule,” amesema.
Kwa upande wake Scholastica Mchome, amesema changamoto siyo tu madarasa, bali pia uwiano wa mwalimu kwa mwanafunzi ambao tayari unaonekana kuwa mkubwa katika maeneo mengi.
“Kwa idadi hii, bila kuajiri walimu wa kutosha, ubora wa elimu unaweza kushuka. Tusiweke nguvu yote kwenye miundombinu tukasahau walimu,” amesema.
Katika hatua nyingine Profesa Mkenda ameeleza fursa mbalimbali ndani ya sekta ya elimu ambazo zinazotolewa kwa vijana na kulitaka kundi hilo kuzichangamkia ili kupata matokeo chanya.
Amesema Serikali inaendelea kutengeneza mazingira wezeshi kuhakikisha vijana wa Kitanzania wanazitumia fursa zinazofungamana na sekta ya elimu kwa kile inachoamini elimu ndiyo nyenzo kuu ya ukombozi wa kifikra.
Amezitaja miongoni mwa fursa hizo ni kuanzishwa kwa mkondo wa amali ambao utawawezesha vijana kupata ujuzi watakaoweza kuutumia kujiajiri au kuajiriwa.
Nyingine ni fursa za ufadhili wa masomo kupitia Samia Schorlaship kwa wanafunzi wanaopata ufaulu wa juu kwenye masomo ya sayansi ja ufadhili wa masomo kwenye eneo la teknolojia.
Amesema hatua hiyo inalenga kuongeza chachu ya ubunifu kwa vijana ili kwenda sawa na kasi ya maendeleo ya teknolojia inayokua kila kukicha.
“Tumeona hili suala la akili unde tunahitaji vijana wetu wengi wabobee kwenye teknolojia, ndiyo maana tumetoa ufadhili na tumeanza na vijana 50 ambao watakwenda nje ya nchi kujifunza masuala ya teknolojia kwa undani.
“Pia, mikopo ya elimu ya juu nayo imeongezeka, mwaka 2020/2021 bajeti ilikuwa Sh 464 bilioni na sasa imefikia Sh916.7 bilioni hii yote ni katika kuhakikisha vijana wanaofika elimu ya juu wanasoma katika mazingira wezeshi,” amesema.
Kuhusu suala la mdondoko wa wanafunzi Profesa Mkenda amekiri kuwa hilo ni tatizo kubwa na wizara yake inalifanyia kazi ikijiandaa kutengeneza mfumo wa kuwafuatilia wanafunzi wote wanaondikishwa.
“Hili ni tatizo kubwa na hatupaswi kuliangalia kwa udogo, tunaendelea kufanya tafiti kujua wanaenda wapi lakini tunataka kutengeneza mfumo unganisho ambapo mwanafunzi atapewa namba kuanzia anavyoandikishwa hadi anapotoka kwenye mfumo wa elimu, tutakuwa tunamfuatilia kujua alipo,” amesema
