Unguja. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imesema kwa sasa lugha ya Kiswahili inapaswa kuwa katika mfumo wa kidijitali na utafiti wa kisayansi ili kuendana na kasi ya teknolojia.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, amesema hayo leo Jumanne Desemba 10, 2025 alipomwakilisha Rais Hussen Ali Mwinyi katika ufunguzi wa kongamano la tisa la Kiswahili la kimataifa, lililofanyika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la zamani, Kikwajuni Unguja.
Amesema katika kipindi hiki cha mapinduzi ya viwanda ambacho teknolojia inaongoza katika ufatiliaji wa maarifa ni muhimu lugha hiyo itengenezewe mazingira mazuri kwa lengo la kuiongezea hadhi duniani kama ilivyo lugha nyingine.
“Serikali imedhamiria kukuza lugha ya Kiswahili kwa kushirikiana na taasisi binafsi kwa kufanya mashindano, makongamano na matamasha ya Kiswahili kama kivutio cha utalii wa kiutamaduni utakaoifanya Zanzibar kuwa kitovu cha Kiswahili duniani,” amesema.
Katika kufikia lengo hilo, ameagiza Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo kujikita katika kufanya ubunifu kwa kushirikiana na mabaraza ya Kiswahili.
Amesema hayo yataifanya lugha hiyo kukua kwa kasi na kuhakikisha Kiswahili kinakuwa rasilimali ya maendeleo ya Zanzibar.
Vilevile, amewataka washiriki wa kongamano hilo kuwa mabalozi wazuri wa kukitangaza Kiswahili popote walipo kwa kuzihimiza familia, wanafunzi na jumuiya za Serikali na binafsi kujua thamani yake.
Waziri wa wizara hiyo, Riziki Pembe Juma, amesema makongamano hayo yanaunda jukwaa la kitaifa na kimataifa kuchochea mijadala, kutengeneza sera na kuibua mwelekeo mpya wa ukuzaji wa lugha hiyo.
Amesema kongamano hilo linaakisi ukubwa wa nafasi ya Kiswahili katika zama za maendeleo ya sayansi na teknolojia, ufunguaji wa masoko, ujenzi wa jamii zenye maarifa na kupanuka kwa diplomasia ya kimataifa.
Waziri amesema matarajio ya kongamano hilo kupitia mijadala ya kitaaluma itakayofanyika itatoa mapendekezo yatakayoisaidia Serikali na taasisi zake kuimarisha sera, mbinu na mikakati ya kukuza lugha hiyo katika elimu, mawasiliano, biashara na nyanja za kimataifa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Kiswahili Zanzibar (Bakiza), Dk Saade Said Mbarouk, amesema kongamano hilo limekuwa daraja la kuwakutanisha wataalamu kutoka duniani na watunga sera ambao watawasilisha tafiti na mikakati ya kuimarisha Kiswahili katika nyanja za elimu, sayansi na maendeleo endelevu.
Amesema baraza hilo limepata mafanikio makubwa ikiwemo kuanzishwa jarida maalumu la kongamano linalolenga kukuza utafiti, ubunifu na mawasiliano miongoni mwa wataalamu wa Kiswahili.
Dk Saade amesema, jukwaa hilo linaandika historia mpya iliyobeba sauti ya vijana na watafiti chipukizi wanaotaka kuona lugha hiyo inapenya katika sayansi, uchumi na utamaduni wa kidunia.