Sowah abanwa, yupo hatarini kufungoni

SIMBA kwa sasa inaugulia maumivu ya kipigo kutoka kwa Azam FC, lakini wakati wowote huenda maumivuΒ  yanaweza kuongezeka kupitia mshambuliaji wake, Jonathan Sowah.

Iko hivi. Wakati Simba inacheza dhidi ya Azam Desemba 7, 2025 na kukubali kipigo cha mabao 2-0, Sowah dakika ya 90+6 katika mechi ikiwa mwishoni alimpiga kiwiko kiungo wa Azam, Himid Mao.

Hata hivyo, Sowah aliyeingia kipindi cha pili dakika ya 84 akichukua nafasi ya kiungo Alassane Kante, tukio lake la kumgonga hadi kumwangusha Himid halikuonwa na mwamuzi Abdallah Mwinyimkuu ambaye alipuliza vilimbi ya kumaliza mechi hiyo.

Video mbalimbali zimeanza kutembea mitandaoni zikimuonyesha mshambuliaji huyo akifanya tukio hilo likiwaamsha mabosi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na hata wale wa Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB).

Taarifa kutoka kwa mmoja wa mabosi wa Bodi ya Ligi zilizoifikia Mwanaspoti zimedai Sowah ni ngumu kupona kwenye tukio hilo.

β€œTumeziona hizo video fupi, lile ni kosa kwa mujibu wa kanuni na mbaya zaidi ameonekana akikataa hata kumpa β€˜fair play’ (kuonyesha uungwana) mchezaji mwenzake huku akitoka baada ya mwamuzi kumaliza mechi,” amesema bosi huyo.

β€œNadhani kikao kinachofuata cha Kamati ya Usimamizi wa Ligi kitatoa uamuzi kwa kuliangalia lile tukio ila kwangu mimi haikuwa sawa kabisa alichofanya.”

Kama akibainika kutenda kosa hilo, Sowah anaweza kufungiwa mechi tano na kupigwa faini ya Sh1 milioni.

Kanuni ya 41:21 kuhusu udhibiti wa wachezaji inasema: “Mchezaji atakayethibitika na kupatikana na hatia ya kumpiga mchezaji mwenzake isivyo kawaida au kwa kutumia nguvu kubwa kuliko kawaida/kupiga au kupigana mwamuzi, kijana wa mpira (ball kids) au ofisa, mhudumu mwingine wa mchezo atasimama kushiriki michezo isiyopungua mitano au kufungiwa kati ya miezi mitatu mpaka mwaka mmoja na faini isiyopungua shilingi milioni moja bila ya kujali kutokuchukuliwa hatua au hatua yoyote iliyochukuliwa na mwamuzi uwanjani na kwa mazingatio ya kanuni ya (41,5,3).”

Adhabu hiyo msimu huu imewakuta beki wa Yanga, Ibrahim Abdullah β€˜Bacca’  na wachezaji wawili wa Mbeya City, Daudi Mwaipola na Vitalis Mayanga kutokana na makosa kama hayo uwanjani.

Endapo Sowah atakutana na hatia na kufungiwa itakuwa ni mara ya pili baada ya kufanya kosa kama hilo msimu uliopita, katika Fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) dhidi ya Yanga na kuonyeshwa kadi nyekundu iliyomkosesha mechi za awali msimu huu, alipohamia Simba.