Tanzania yaeleza inavyotumia maarifa ya asili, sayansi kulinda bahari ikolojia za pwani

Nairobi. Tanzania imeeleza hatua inazochukua kulinda rasilimali za pwani na mifumo ya ikolojia ya bahari kama miamba ya matumbawe na maeneo oevu.

Akizungumza leo Jumatano, Desemba 10, 2025 katika mkutano wa pembeni uliojadili, ulinzi wa rasilimali za pwani na bahari, kwenye kikao cha saba cha Baraza la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEA-7), Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Cyprian Luhemeja, amesema Tanzania imeelekeza nguvu katika kuimarisha haki za jamii, usimamizi shirikishi na kuhakikisha kunakuwepo na mgawanyo wa faida wenye usawa katika miradi ya uhifadhi.

“Mageuzi tunayofanya si ya kiikolojia pekee. Tunataka kuhakikisha jamii za pwani, hususan wanawake, vijana na makundi mengine, wanashiriki kikamilifu katika maamuzi, usimamizi na mgawanyo sawa wa rasilimali,” amesema.

Akieleza hatua zinachochukuliwa na Serikali, Luhemeja amesema wanahakikisha kuimarisha haki za kijamii na mifumo ya usimamizi shirikishi kupitia upanuzi na uimarishaji wa Kamati za Usimamizi wa Fukwe (BMUs) na vikundi shirikishi vya uvuvi.

“Serikali inahakikisha uongozi wa BMUs unajumuisha wanawake, vijana na makundi madogo, huku wanajamii wakipatiwa mafunzo ya utawala bora, usimamizi wa fedha, utatuzi wa migogoro na kuunganishwa na watafiti pamoja na mamlaka za kitaifa” amefafanua.

Pia, ametaja mgawanyo sawa wa rasilimali na faida kwa ujumuishaji na kusaidia wanawake wanaojihusisha na kilimo cha mwani, uongezaji thamani na upatikanaji wa masoko.

“Tunahakikisha ushiriki jumuishi katika upangaji wa maendeleo ya maeneo ya pwani na kukuza usawa kielimu na ujenzi wa uwezo, ikihusisha mafunzo ya ufuatiliaji wa rasilimali, uendeshaji boti, ramani dijitali, utalii ikolojia na ujasiriamali,” amesema.

Aidha, Luhemeja amesema, Tanzania inaunganisha masuala ya mabadiliko ya tabianchi na ulinzi wa jamii katika programu hizo.

“Tunapowawezesha wananchi na kuchanganya sayansi na maarifa ya asili, tunaimarisha ustahimilivu wa tabianchi na kulinda mazingira yetu.”

Umuhimu wa kuhalalisha maarifa ya asili

Mshauri wa UNEP katika masuala ya jamii asilia na ikolojia za pwani, Chris Poonian, amesema uhifadhi wa miamba ya matumbawe hauwezi kufanikiwa ikiwa maarifa ya asili yataachwa pembeni.

“Uhifadhi wa haki na wenye ufanisi lazima uweke ujumuishe elimu za asili,” amesema, akibainisha kuwa tafiti zimeonyesha mbinu za jadi si mila tu, bali ndio msingi wa usimamizi endelevu wa miamba ya matumbawe kwa maelfu ya miaka duniani kote.

Hata hivyo, aliongeza kuwa mbinu hizo mara nyingi hazitambuliwi kwenye mifumo ya sheria.

Poonian amesisitiza haja ya kuzitambua rasmi katika sheria za nchi, kuzihusisha mamlaka za asili katika usimamizi wa bahari, na kuhakikisha ridhaa ya wazi, huru na ya awali kwa maamuzi yanayohusu maji ya mababu.

Akuzungumzia umuhimu wa elimu na maarifa asili, Mkurugenzi wa Kitengo cha Ikolojia wa UN Environment, Susan Gardner, ametoa mifano ya kimataifa ikiwemo Canada, ambako vikosi vya moto vya watu wa asili vinafanya kazi kwa pamoja na idara za moto za kisasa kufufua mbinu za kitamaduni za kukabiliana na moto, zikisaidiwa na teknolojia kama satelaiti.

“Ujumbe ni mmoja. Maarifa ya asili ni muhimu na tunapata matokeo mazuri zaidi tunapoyaunganisha na sayansi,” amesema.

Ushahidi kutoka kwa vijana

Mwanabiolojia wa bahari na mwakilishi wa vijana kutoka jamii ya asili ya Guna Yala nchini Panama, Susania Avila Misselis, ameeleza jinsi vijana wanavyounganisha hekima za mababu na sayansi ya kisasa.

Amesema, “wasichana wa Guna wanaongoza usimamizi wa jamii, ubia wa kisayansi na elimu ya uhifadhi, wakitumia mbinu za jadi sambamba na ufuatiliaji wa kisasa chini ya maji na uchambuzi wa afya ya matumbawe.”