Tuhuma za uchawi zawaponza watatu, wahukumiwa kunyongwa

Arusha. Hasira hasara. Ni kauli inayoakisi kilichowakuta wakazi watatu wa Murongo, wilayani Kyerwa, Mkoa wa Kagera, baada ya mmoja wao kumtuhumu Jenester Petro kutohudhuria maziko ya mtoto wake kwa kuwa ni mchawi.

Nyumba ya Petro ilibomolewa na kuchomwa moto, kisha akapigwa hadi kufa na mwili wake kuteketezwa kwa petroli.

Mahakama Kuu Masjala Ndogo Bukoba imewahukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa washtakiwa watatu wa mauaji hayo ambao ni Roida Emmanuel, Saverina Wilbard na Kemilembe Barakwea.

Jaji Lilian Itemba, aliyesikiliza kesi ya mauaji dhidi ya washtakiwa, alitoa hukumu hiyo Novemba 27, 2025 na nakala yake kupakiwa kwenye mtandao wa Mahakama.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili katika kesi hiyo, mahakama iliwatia hatiani washtakiwa na kuwahukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa.

Ilidaiwa mahakamani kuwa Petro alishukiwa kuwa mchawi, moja ya sababu za tuhuma hizo ikiwa ni kutohudhuria maziko ya mtoto wa jirani yake (mshtakiwa wa kwanza).

Kutokana na hilo, nyumba yake ilibomolewa na kuchomwa moto.

Ilidaiwa baada ya Petro kutokea, alifukuzwa na kupigwa hadi kufa, kisha mwili wake ukamwagiwa petroli na kuchomwa moto.

Siku chache baadaye, washtakiwa wote watatu walikamatwa na kushtakiwa kwa kosa la mauaji kinyume cha kifungu cha 196 na 197 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu.

Wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo, upande wa Jamhuri uliwasilisha mashahidi watano na kielelezo kimoja.

Mauaji hayo yanadaiwa kutokea Juni 21, 2024 katika Kijiji cha Murongo.

Mahakama ilielezwa kuwa Jenester Petro alikuwa akiishi kitongoji kimoja na mshtakiwa wa kwanza (Roida) na nyumba zao zilikuwa jirani.

Ilielezwa kuwa mtoto wa kiume wa Roida aitwaye Daniel (17) alipofariki dunia, Petro hakuhudhuria maziko, akatuhumiwa kuwa ndiye aliyemuua.

Shahidi wa tatu na wa nne, Judith Faustin na Zawadi Simon, walidai kuwa baada ya maziko Juni 20, 2024, wakiwa na washtakiwa wa pili na wa tatu, walikusanyika nyumbani kwa Roida kumfariji na kusaidia kupika na kuosha vyombo.

Walidai wakiwa huko, washtakiwa hao watatu walianza kupanga njama ya kumuua Petro.

Shahidi wa tatu alidai hawakuchukulia mipango hiyo kwa uzito, wakiamini jambo hilo lisingeweza kutokea kwa urahisi.

Walidai siku iliyofuata usiku, Petro alirudi nyumbani kwake. Washtakiwa walipomwona, walimfukuza na kumshambulia kwa vipande vya kuni zilizotumika awali kupikia kwenye mazishi.

Alidai walimpiga nyuma ya kichwa na sehemu nyingine za mwili hadi akaanguka na kupoteza maisha. Mwili wake ulichomwa kwa kutumia makaa ya moto uliotumika kupikia pamoja na majani ya maharage.

Alidai kwa kushinikizwa na mshtakiwa wa tatu, Roida alimtaka mtoto wake akalete petroli ambayo waliimwaga juu ya maiti, na kwa hofu kubwa mashuhuda walikimbia na kuondoka eneo hilo.

Shahidi huyo wa tatu alidai kwenda kuripoti tukio hilo kwa mumewe aliyekuwa katika kituo chake cha biashara.

Taarifa ikatolewa kwa mwenyekiti wa kitongoji, Nickson Simon, Juni 22, 2024.

Shahidi wa tano, askari G8268 Sajenti Asifiwe, na maofisa wengine wa polisi walitembelea eneo la tukio wakiwa na daktari Dickson Machalo (shahidi wa kwanza wa Jamhuri).

Dk Machalo alieleza aliufanyia uchunguzi mwili wa marehemu uliokutwa nje, jirani na nyumba yake iliyoungua, ukiwa umezungukwa na majivu.

Alidai mikono yote miwili haikuwepo, huku sehemu ya nyama ikiwamo ya makalio ikiwa imebaki.

Shahidi wa tano alidai alipata taarifa kutoka kwa chanzo cha siri kuwa kijijini hapo kuna mashahidi wengine walioshuhudia tukio hilo, lakini waliogopa kutoa ushahidi kwa kuwa walitishwa, hivyo akawapata wawili pekee.

Alidai aliwakamata washtakiwa wote watatu waliokuwa wamekimbia kijiji hicho.

Mshtakiwa wa kwanza alikana kuhusika na mauaji, akieleza kuwa Juni 18 alifiwa na mwanaye ambaye walimzika siku iliyofuata.

Alisema wanakikundi wenzake walibaki naye kumfariji na kwamba Juni 22 alipata taarifa za kifo cha Petro.

Aliieleza mahakama kuwa majirani zake watatu—shahidi wa tatu, wa nne, Violeta, Zawadi na Salina, walikuwa wametuma maombi ya kujiunga na chama chake ambacho anahudumu kama mwenyekiti, lakini walikataliwa kwa kutokidhi vigezo.

Alidai ushahidi wa mashahidi wa tatu na wa nne ulitokana na hasira ya kunyimwa kujiunga na kikundi hicho.

Alidai Julai 25, 2024, wakati maofisa wa polisi walipovunja mlango wa nyumba yake, hakuwa ametoroka. Aliiomba mahakama imuachie huru akihofia mali zake zilizoibwa katika uvamizi huo.

Mshtakiwa wa pili alidai baada ya kujulishwa na mchungaji wake kuwa Daniel amefariki dunia, alisafiri hadi Murongo kuhudhuria mazishi. Baada ya maziko alikwenda nyumbani. Alikana kuwafahamu washtakiwa wenzake, akidai alikamatwa sokoni Isingiro.

Mshtakiwa wa tatu alidai kwenda nyumbani kwa mshtakiwa wa kwanza kuhudhuria mazishi ya Daniel, na baada ya matanga Juni 19 alikusanya sahani za kikundi na Juni 20 alirejea nyumbani kwake.

Alidai hakuwahi kurudi katika eneo hilo hadi Juni 22 alipokuwa akivuna shambani kwake, mtoto wake alimwarifu kuwa Petro amefariki dunia.

Alieleza kuwa alikwenda kuomboleza kifo chake ambako alikamatwa akijiandaa kuondoka.

Mshtakiwa huyo alidai hakuwahi kujaribu kutoroka na hakuwafahamu washtakiwa wa kwanza na wa pili hadi walipokutana gerezani.

Jaji Itemba amesema amezingatia ushahidi wa shahidi wa tatu na wa nne waliodai kuwatambua washtakiwa eneo la tukio, huku akirejea mashauri mbalimbali ya Mahakama ya Rufaa kuhusu ushahidi wa utambuzi wa washtakiwa eneo la tukio.

Amesema mashahidi hao walieleza kuwa walikuwa wamesimama karibu na eneo la tukio, hatua tano hadi 10 kutoka upande wa pili wa barabara, wakiangalia watuhumiwa wakimshambulia na kumuua Petro.

Amesema mahakama haitilii shaka utambuzi wa washtakiwa eneo la tukio.

“Nimezingatia hoja za pande zote, mawakili wa utetezi wameeleza kuwa kuna mkanganyiko wa muda wa tukio. Nimeona hilo na nadhani ni dogo kwa sababu mashahidi wote wawili wanarejelea siku moja, na ukinzani wao ni mdogo kati ya saa za jioni,” amesema na kuongeza:

“Ushahidi unaonesha kuwa washtakiwa walimvamia marehemu kwa vipande vya kuni na kumpiga kichwani, ambayo ni sehemu nyeti. Ikiwa haitoshi, waliuchoma moto mwili wake.”

Jaji amesema: “Vitendo hivi bila shaka vinaonesha kuwa washtakiwa walikuwa na nia mbaya, walikuwa na nia moja siyo tu ya kumdhuru marehemu bali kumuua.”

Jaji Itemba baada ya kupitia ushahidi wa pande zote mbili, alihitimisha kwa kueleza kuwa upande wa mashtaka umethibitisha kesi kwa kiwango kinachotakiwa kisheria, hivyo mahakama imewatia hatiani washtakiwa wote watatu na kuwahukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa.