Dar es Salaam. Wananchi na wachambuzi wa siasa na jamii wamesema utulivu ulioonekana Jumanne Desemba 9, 2025 unapaswa kuendelezwa ili kuimarisha ulinzi na usalama wa Taifa.
Kauli zao zinakuja siku moja baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani, George Simbachawene, kutoa wito wa kutunza amani wakati Tanzania ikiadhimisha miaka 64 ya Uhuru wa Tanganyika.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti leo Jumatano Desemba 10,2025 wananchi na wachambuzi hao wamesema tukio la Oktoba 29, 2025 limeonyesha umuhimu wa kutafuta ufumbuzi wa tofauti za kisiasa kwa njia zisizoleta vurugu.
Kwa mujibu wao, maandamano licha ya kuwa na uhalali wa kikatiba, hayapaswi kutumika kama mbinu ya kwanza ya kudai haki, wakisisitiza umuhimu wa kuwasilisha malalamiko yaliyopo kwa Tume ya Kuchunguza Vurugu za Oktoba 29.
Vurugu zilizotokea siku hiyo ulipofanyika uchaguzi mkuu zilisababisha uharibifu wa mali za umma na binafsi pamoja na vifo.
Mkazi wa jijini Dar es Salaam, Joseph Clement, amesema utulivu ni jambo muhimu kwa shughuli za kiuchumi na maisha ya kila siku, akieleza kuwa matukio ya vurugu huathiri watu wengi wanaotegemea kipato cha kila siku.
βNiwasihi wanaopanga kufanya maandamano, waache kwa sababu siyo njia sahihi na si utamaduni wetu Watanzania. Kilichotokea Oktoba 29, ni funzo kubwa kwetu, kiliharibu maisha ya Watanzania, tujiepusha na mtego wa maandamano mwingine unaoapangwa,β amesema.
Mchambuzi wa siasa na jamii, Kiama Mwaimu, amesema hatua ya wananchi kutoshiriki maandamano yaliyokuwa yakihimizwa katika mitandao ya kijamii ni ishara kuwa sehemu kubwa ya jamii inapendelea njia zinazolinda utulivu.
Hata hivyo, amesema jukumu la kudhibiti viashiria vya uvunjifu wa amani linabaki kwa vyombo vya ulinzi ambavyo vimeuimarisha maeneo mbalimbali nchini.
Amewashauri wananchi wenye malalamiko kuyawasilisha mbele ya Tume, akisema mchakato huo unaweza kusaidia kutengeneza mapendekezo yatakayoshughulikia changamoto zilizojitokeza.
βTume ikipata maoni ya kutosha itatoa ushauri mzuri kwa Serikali wenye lengo la kutatua changamoto zilizopo. Tume inaruhusu kupokea maoni, kuzungumza na watu, kama wana dukuduku wapeleke huko, si sahihi kufanya maandamano yanayosababisha vurugu na kuleta adha kwa wasiokuwa na hatia,β amesema na kuongeza:
βKuna wengine wao riziki zao hadi watoke kwenda kutafuta ndio maisha yao, sasa kukiwa na vurugu kama za Oktoba 29, hawa wataishi vipi? Hata mimi nina mawazo yangu nikionana na Tume nitayaeleza.β
Mchambuzi mwingine, Ali Makame, amesema maandamano ni haki ya kisheria, lakini yanatakiwa kuandaliwa kwa kufuata utaratibu unaohitaji taarifa kwa Jeshi la Polisi, ikiwemo kueleza barabara zitakazotumika na waandaaji wanao wajibika.
Amesema matukio ya Oktoba 29 yameonyesha kuwa kutokuwa na mpangilio au kutoonekana kwa waandaaji huongeza hatari ya uvunjifu wa amani na athari kwa wananchi.
Makame amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa Tume ya Uchunguzi, akisema taarifa na maoni ya wananchi ndiyo msingi wa uchambuzi na mapendekezo yatakayotolewa.
βWatanzania wenzangu amani na umoja uliopo haukujengwa kirahisi, zilifanyika jitihada kubwa. Amani ikipotea kuirejesha ni ngumu sana, yaliyotokea Oktoba 29 tusiyaruhusu tena, siyo ustaarabu wetu,β amesema.
Amesema: βHata kama tuna kasoro na mapungufu yetu tutumie njia sahihi ili kueleza changamoto hizo ili kuyafikia maendeleo kamili. Tuimarishe umoja na tuthamini nembo yetu ya umoja.β
