Unguja. Takwimu kutoka Zanzibar zinaonyesha kuwa visiwa hivyo vilipokea watalii wa kimataifa 72,833 katika kipindi cha Novemba 2025, ikiwa ni ongezeko la asilimia 8.6 ikilinganishwa na wageni 67,049 waliowasili kipindi kama hicho mwaka jana.
Hiyo ni kwa mujibu wa Tume ya Utalii Zanzibar kwa kushirikiana na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali zilizotolewa juzi Desemba 8, 2025.
Taarifa mpya ya utalii inaonyesha kupungua kwa asilimia 16 kutoka wasafiri 86,740 waliowasili Oktoba 2025, hali inayodhihirisha mzunguko wa misimu ya utalii visiwani wakati kilele cha msimu wa juu kikianza kupungua.
Wasafiri kutoka Ulaya waliendelea kutawala soko, wakiweka asilimia 73.1 ya wote waliowasili Novemba.
Italia iliongoza kwa asilimia 12.2 ya wageni wote, ikifuatiwa na Ujerumani (asilimia 7.7) na Ufaransa (asilimia 7.4), huku Japan ikiwa na idadi ndogo zaidi ya asilimia 0.1.
Masoko yanayochipukia ikiwemo Poland, India, Urusi, Israel, China na Ukraine yalionesha kupungua kidogo kwa asilimia 1.1 ikilinganishwa na takwimu za Oktoba.
Usafiri wa anga uliendelea kuwa njia kuu ya watalii kuingia Zanzibar, kwa asilimia 93.7 ya wote waliowasili kupitia uwanja wa ndege Novemba. Kati ya hao, abiria 54,263 waliwasili kwa ndege za kimataifa, huku 13,960 wakitua kwa safari za ndani ya nchi.
Kwa upande mwingine, wasafiri 4,610 pekee waliingia visiwani kwa njia ya bahari, ambapo wanne tu walikuwa watalii waliowasili kwa meli kubwa za kitalii.
Wasafiri wa likizo waliendelea kuipa nguvu sekta hiyo, huku watalii 72,433 (asilimia 99.5) wakitembelea visiwa hivyo kwa madhumuni ya mapumziko.
Ni asilimia 0.4 tu waliokwenda kuwatembelea ndugu na jamaa, huku asilimia 0.1 wakiwasili kwa sababu nyinginezo.
Kwa upande wa rika, wenye umri kati ya miaka 15β64 walichangia sehemu kubwa ya watalii waliowasili visiwani hapo kwa asilimia 87.7, wakifuatia wazee (miaka 65 na kuendelea) kwa asilimia 8.2, na watoto kwa asilimia 4.1.
Jumla ya vitanda 884,430 vilikuwa vinapatikana mwezi huo, huku 601,266 vikiuzwa, sawa na asilimia 68 ya matumizi (occupancy rate).
Kuhusu muda wa kukaa taarifa inaonyesha kuwa watalii hao walikaa wastani wa siku nane, ambapo asilimia 32.8 walichagua kukaa kwa muda wa wiki moja.
