WAZIRI wa Maji, Juma Aweso, ameagiza mgawanyo wa maji kutoka Chanzo cha Ruvu ufanyike kwa usawa, huku akisisitiza maji hayo yahifadhiwe.
Hayo ameyasema wakati akizungumza leo Desemba 10, 2025, katika ziara yake kwenye Mtambo wa Kuzalisha Maji wa Ruvu Juu uliopo Mlandizi, Kibaha mkoani Pwani, Waziri Aweso amesema mgawanyo wa maji lazima uendane na kiwango halisi kinachozalishwa na kiwe na uwiano unaozingatia mahitaji ya wakazi wote wanaotegemea chanzo hicho.
“Mgawo wa maji ufanyike kwa usawa. Kiwango kidogo tulichonacho kigawiwe bila upendeleo ili kila eneo lipate huduma kadri inavyowezekana,” amesema Aweso.
Amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha kuwa, licha ya changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa na kupungua kwa maji kwenye vyanzo, huduma ya majisafi inaendelea kuwafikia wananchi bila maeneo mengine kuachwa nyuma.
Aidha, Waziri Aweso ametoa rai kwa wakazi wa Dar es Salaam na Pwani kuendelea kuhifadhi maji, akibainisha kuwa kipindi hiki ni cha mpito na kwamba mvua zinatarajiwa kuanza kurejea katika maeneo mengi, hatua itakayoboresha kiwango cha uzalishaji wa maji kwenye mtambo huo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Wami–Ruvu, Elibariki Joseph Mashi, alieleza kwa kina chanzo cha upungufu wa maji na hatua zilizochukuliwa kurejesha kiwango cha maji kwenye vyanzo.
Amwsema bonde hilo ndilo linalohudumia mikoa ya Pwani, Dar es Salaam na baadhi ya maeneo ya Morogoro kupitia mito muhimu inayotegemewa katika uzalishaji wa maji. Hata hivyo, mvua za vuli za mwaka huu zilikuwa chache kuliko ilivyotarajiwa, hali iliyosababisha kupungua kwa kiwango cha maji katika vyanzo.
“Kama taasisi, jukumu letu ni kufuatilia vyanzo vya maji na kubaini changamoto zinazosababisha kupungua kwa maji. Tumekuwa tukifanya doria, na tumesisitisha shughuli zote zisizo za matumizi ya majumbani zilizokuwa zikichangia kupoteza maji. Baada ya hatua hizi, kiwango cha maji kimeanza kuongezeka,” amesema Mmasi
Mkurugenzi huyo amebainisha kuwa moja ya changamoto kuu ilikuwa mgawanyiko wa mkondo wa mto, ambapo maji yalikuwa yanaingia katika mikondo midogo midogo na hivyo kupunguza kiasi kinachofika kwenye vituo vya uzalishaji wa maji.
“Mto unaposhuka maji, huwa kuna wakati unahama mkondo wake. Tulichokifanya ni kuzuia mikondo yote midogo na kuelekeza maji kwenye mkondo mmoja. Hatua hii imehakikisha maji yanatiririka moja kwa moja kuelekea maeneo ya uzalishaji kwa ajili ya Dar es Salaam,” alifafanua.
Amesema juhudi hizo zimeanza kuonyesha mafanikio na kwamba wananchi wanapaswa kuwa na matumaini kuwa hali itarejea katika utulivu katika kipindi kifupi kijacho. Wakati huohuo aliwataka wananchi wanaoishi karibu na vyanzo vya maji kutunza mazingira ya maeneo hayo na kuendelea kushirikiana na mamlaka.
“Tumetoa rai kwa wananchi kuwa wastahimilivu na kushirikiana nasi kutunza vyanzo hivi. Maeneo yaliyopoteza maji tumeyadhibiti, na maji yanayotiririka sasa yanatumika kwa matumizi ya majumbani pekee, ambayo ndiyo kipaumbele chetu hivi sasa,” amesema.