Aliyeua mke, mtoto ahukumiwa kunyongwa

Arusha. Ni mauaji ya kutisha. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya Hamis Shija, kuhukumiwa adhabu ya kunyongwa hadi kufa baada ya kukutwa na hatia ya kuwaua mkewe, Diana John na mtoto wao, Yakobo Hamis.

Ilidaiwa mahakamani kuwa Hamis alimuua mkewe aliyekuwa mjamzito kwa kumchinja kwa kutumia panga, baadaye kutumia wembe kukata tumbo lake na kutoa watoto wawili ambapo alidai kuambiwa na mganga kuwa mkewe anamroga na ndiye chanzo cha yeye kushindwa kutajirika.

Ilidaiwa kuwa mmoja wa watoto aliowatoa tumboni kwa mkewe, alimkata viungo na kuviweka kwenye sufuria na kuvichemsha, kisha akamuua mtoto wake, Yakobo Hamis kwa kumchinja.

Mauaji hayo ya kutisha yalitokea Januari 28, 2024 (ambapo alimuua mkewe) na Januari 29, 2024 alimuua mwanaye katika kijiji cha Misangi, Kata ya Uyogo wilayani Urambo, Tabora.

Jaji Zaiban Mango aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo ya mauaji, amesema baada ya kupitia ushahidi wa pande zote mbili, Mahakama imemkuta Hamis na hatia na kumuhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa.

Hamis alishtakiwa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Tabora, makosa aliyodaiwa kutenda kinyume na kifungu cha 196 na 197 cha Kanuni ya Adhabu.

Upande wa mashtaka ulieleza kuwa Diana na mshtakiwa walikuwa mke na mume na Yakobo alikuwa miongoni mwa watoto waliopata katika ndoa yao.

Upande wa mashtaka, ulikuwa na mashahidi 12 na vielelezo vitano huku mshtakiwa akiwa shahidi pekee wa utetezi.

Upande wa mashtaka, ulieleza kuwa vifo vya watu hao havikuwa vya asili ambapo mashahidi wote 12 waliopata fursa ya kuona miili hiyo walitoa ushahidi kuwa marehemu wote walikuwa na majeraha ya kukatwa.

Upande wa mashtaka uliieleza Mahakama kuwa hakuna shahidi aliyeshuhudia mauaji hayo ila mshtakiwa alihusishwa na mauaji hayo kutokana na ushahidi wa kimazingira,  pamoja na mshtakiwa mwenyewe kukiri.

Shahidi wa pili, Elisha Paulo alidai Januari 27, 2024 akiwa nyumbani na mshtakiwa (ambaye ni baba yake wa kambo) na marehemu mama yake, Sumbu na Yakobo (marehemu kwa sasa), walipata chakula cha mchana kilichokuwa kimeandaliwa na ndugu yake (Dotto).

Alisema baada ya chakula cha mchana, Dotto aliondoka na kurejea kwa bibi yao alikokuwa akiishi.

Alisema kuwa nyumba yao ilikuwa na chumba kimoja na varanda ambapo mshtakiwa, mkewe na Yakobo walikuwa wakilala chumbani huku yeye na Sumbu wakilala kwenye varanda.

Alieleza kuwa kila mshtakiwa anaporudi nyumbani  jioni, alikuwa akimuamsha ili amfungulie mlango na kuwa Januari 27, 2024 mshtakiwa alichelewa kurudi lakini hakumuamsha ili afungue mlango.

Shahidi huyo aliieleza mahakama kuwa Januari 28, 2024 saa za asubuhi, alisikia mtu akikoroma kwenye chumba cha kulala cha mzazi wake na baada ya muda, mshtakiwa alitoka nje ya chumba hicho na kuendelea na shughuli zao za asubuhi ila mama yao hakutoka chumbani.

Aliieleza mahakama kuwa alimtunza ndugu yake (Yakobo) kwa kumlisha, kumwogesha na kumbadilisha nguo akieleza kuwa mshtakiwa aliwaambia wasiingie chumbani kwake.

Shahidi huyo wa pili  na mdogo wake Sumbu, walianza kuwa na mashaka na mama yao alipo kwa vile hakutoka chumbani, na kuwa mshtakiwa aliwaambia kuwa amemuua mama yao baada ya kutokuelewana baina yao.

Alisema jioni mshtakiwa aliwapikia chakula na Yakobo alilala naye kwenye varanda ambapo baadaye mshtakiwa aliingia ndani huku yeye na Sumbu wakiwa nje ya nyumba hiyo na ghafla walisikia sauti mtu akilia ndani ya nyumba, na alipotaka kwenda kuangalia mshtakiwa alimzuia.

Aliieleza mahakama kuwa alipoenda kumuangalia Yakobo hakukumkuta alipokuwa amemlaza aliamua kufungua pazia la chumbani kwa wazazi wake na kumuona Yakobo akiwa amelala kitandani shingo yake ikiwa na jeraha lililokatwa.

Aidha alisema pia aliona kitanda kimesogezwa kidogo na mama yake amelazwa chini na kuwa alitamani kutoroka nyumbani, lakini aliogopa kwamba asipokuwepo mshtakiwa anaweza kumuua Sumbu.

Shahidi huyo alisema alimuona mshtakiwa akichemsha vitu vinavyofanana na vipande vya nyama ya ng’ombe na   alipomaliza kuchemsha vitu vyake, mshtakiwa alimwita na kumtaka ashike chupa ya plastiki ili amwage mafuta aliyoyachota kwenye chupa hiyo.

Aliendelea kueleza kuwa mshtakiwa alimwambia, mafuta ambayo alichimba hayawezi kupatikana kwa urahisi, baadaye alimwita ndani aende kumsaidia  kubeba maiti ya Diana.

Shahidi huyo alieleza kuwa alisita, lakini mshtakiwa akasisitiza amsaidie kuubeba mwili wa Diana ambapo waliubeba hadi kwenye shimo ambalo lilichimbwa katika shamba nje ya nyumba yao na mshtakiwa, alimzika hapo.

Alieleza kuwa waliporudi, mshtakiwa aliwazuia kutoka nje ya nyumba na baadaye aliwasikia wajomba zake Joseph na Masonge wakigonga mlangoni kwao, hawakuweza kujibu kwani mshtakiwa aliwaambia wasimjibu mtu yeyote.

Alieleza shangazi yao naye alikuja na kugonga lakini tena hawakuweza kuitikia, baada ya muda mjomba wao alikwenda tena lakini hawakuweza kuitikia hodi yake, kisha akasikia watu wakisukuma mlango wa nyumba yao. Mshtakiwa aliushika mlango kisha akauacha na kuwakumbatia yeye na Sumbu kwa nguvu.

Shahidi huyo aliieleza Mahakama kuwa mlango uliposukumwa alichukuliwa na mwenyekiti wa kijiji na baadaye yeye na Sumbu wakapelekwa nyumbani kwa babu yao mzaa mama.

Katika utetezi wake, mshtakiwa huyo alisema siku ya tukio hakuwepo nyumbani alikuwa safarini Mnande, Kaliua kuchukua bidhaa na kwa kuwa hakupata bidhaa siku hiyo aliamua kulala huko.

Alisema siku iliyofuata alirejea nyumbani kwake na kuwakuta wanaye wawili,  Sumbu na Elisha na shahidi wa pili na alipowauliza alipo mama yao walisema hawafahamu.

Aliieleza Mahakama kuwa alipoingia chumbani kwake alikuta mwili wa Yakobo na kijusi kilichochemshwa kwenye sufuria ya kupikia na alipata wazo la kwenda kuwajulisha majirani zake,  lakini kabla ya kufika kwa majirani aliona watu wakija huku wakiwa na mapanga.

Alisema kuwa aliogopa pengine watu hao ndio waliomuua mtoto wake Yakobo na mkewe Diana, hivyo ilibidi akimbilie nyumbani kwake na kuwashika wanaye ili kuwalinda na watu hao.

Mshtakiwa huyo alikana kuhusika na mauaji hayo na kukana kuwapeleka polisi mahali alipozikwa Diana, akikana kurekodi maelezo ya ziada.

Jaji amesema ushahidi wa shahidi wa pili unaweka ushahidi wa kimazingira unaoonyesha kuwa mshtakiwa ndiye aliyemuua Diana na Yakobo, ambapo pia alikiri mbele yake kumuua mkewe kutokana na kutokuelewana.

Amesema mbali na kwa shahidi wa pili, mshtakiwa huyo alikiri kwa mashahidi waliokuwa eneo la tukio wakati wa kukamatwa kwake ambapo walidai hakukana kuhusika na vifo hivyo.

Jaji amesema ilidaiwa na shahidi wa 11, H. 875 Koplo Christopher kuwa, mshtakiwa alikiri mbele ya polisi na kwenye maelezo yake ya onyo.

Alisema licha ya maelezo hayo ya onyo ya mshtakiwa kutokusomwa au kuwasilishwa mahakamani hapo katika orodha ya ushahidi wa maandishi wa upande wa mashtaka, badala yake upande wa mashtaka ulitoa maelezo ya ziada ya mshtakiwa huyo kupitia Jaji wa Amani Siriri Mboya ambaye alikuwa shahidi wa tisa kwenye kesi hiyo.

Kwa mujibu wa Mboya, mshtakiwa alikiri kuwaua Diana na Yakobo kwa kuwa aliamini walikuwa wakifanya uchawi na wao ndio chanzo cha masaibu yake.

Alisema katika maelezo hayo mshtakiwa huyo kwa mganga wa kwanza aliyemfahamu kwa jina la Sai, alipoenda kwake alimtaka aende kwa mganga mwingine aitwaye Undala ambapo alipoenda huko alielezwa hawezi kutajirika kamwe hadi mkewe afe, na hata mimba aliyonayo mkewe si kitu bali ni majimaji tu, hivyo alipewa dawa ya kutumia.

Mahakama hiyo ilinukuu sehemu ya ungamo la mshtakiwa ambapo alieleza kuwa: “Ndipo baada ya kurudi nyumbani nikiwa nimepewa dawa na waganga wote wawili ya kupaka na kujifukiza na usiku huo wa Januari 28, 2024, nilitumia dawa zile na nikagundua kuwa ndani ya nyumba mke wangu Diana John na mtoto wangu Yakobo Hamis hawapo ndani wameenda kuloga.

“Alfajiri saa 11 niliwaona wakitokea kuloga, ndipo nikachukua uamuzi wa kumchinja mke wangu Diana John kwa kutumia panga na kisha nikampasua tumbo kwa kutumia wembe ili kuhakiki maneno ya wale waganga kama tumboni kuna maji, ambapo tumboni nilitoa vitoto vichanga viwili,” alinukuliwa na kuongeza.

“Na kimoja nilikifukia kwenye shimo la choo na kingine nilikata mikono na miguu na kuchemsha kwenye sufuria pamoja na kiwiliwili. Na Januari 29, 2024, niliamua kumchinja mtoto wangu Yakobo  kwa sababu naye niliambiwa na mganga kuwa pia ni mchawi anaziba riziki.”

Baada ya kupitia hoja za pande zote mbili Mahakama ilihitimisha kuwa utetezi wa mshtakiwa haukutikisa ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka dhidi yake, hivyo ikamtia hatia kwa mauaji ya mkewe na mwanaye na kumuhukumu kunyongwa hadi kufa.