Chadema yasisitiza miili ya waathirika wa vurugu za Oktoba 29, izikwe kwa heshima

Dar es Salaam. Makamu Mwenyekiti wa Chadema, John Heche ameitaka Serikali kuwasilisha na kukabidhi miili ya watu wote waliouawa kabla, wakati na baada ya 29 Oktoba 2025, ili miili hiyo izikwe kwa heshima.

Kauli ya kiongozi huyo ni msimamo wa chama hicho kuhusu Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29,2025 ambapo yalifanyika maandamano yaliyozaa vurugu katika mikoa mbalimbali, ikiwemo Dar es Salaam, Mwanza, Mara, Mbeya, Geita, Dodoma, Songwe na Arusha.

Novemba mwaka huu akizungumza na waandishi wa habari, msemaji wa Serikali, Gerson Msigwa akijibu swali la mwandishi wa habari kuhusu malalamiko ya wananchi kutoona miili ya ndugu zao tangu Oktoba 29, amesema kwa wale wote ambao ndugu zao hawaonekani waende polisi.

“Katika hatua hii nitoe wito, sehemu sahihi ni kwenda polisi, polisi wao ndio wenye uwezo wa kufanya jitihada kujua walipo na kama kutakuwa na maelekezo mengine, haya ni matukio yaliyotokea wakati wa vurugu,”alisema.

Msigwa alisema Tume ya kuchunguza matukio ya vurugu za Oktoba 29 itakapokamilisha kazi zake taarifa nyingi zaidi zitajulikana.

 Heche amesema, “tunasisitiza kuwasilishwa na kukabidhiwa kwa familia zao miili ya wote waliouawa kabla, wakati na baada ya  Oktoba 29,2025, ili hatimaye miili hiyo izikwe kwa heshima na desturi za Tanzania,”amesema.

Pia katika hatua nyingine, Heche ametaka kukomeshwa mara moja kwa operesheni zote za utekaji, mateso, mauaji na upotezaji wa raia, na Watanzania waliopotea kwa kutekwa waachiwe huru.

Mbali na hayo amesema Chadema inataka uchunguzi wa utakaofanywa na tume huru inayoaminika yenye wajumbe wa ndani na nje ya nchi, ili kubaini ukweli wa idadi ya mauaji haya, makaburi ya halaiki na kuwajibishwa kwa wote waliohusika.

Hata hivyo, akiwaondoa wananchi hofu kuhusu tume iliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan, Desemba mosi mwaka huu, katika mkutano wake na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Tume ya Uchunguzi wa Matukio ya Uvunjifu wa Amani wakati na baada ya uchaguzi mkuu Oktoba 29, 2025, Jaji Mkuu mstaafu, Othman Chande alisema anajua utendaji wa tume hiyo utapimwa kitaifa na kimataifa, hivyo imejikita kuzingatia Watanzania wanataka nini.

Alisema mambo waliyobaini, Watanzania wanataka uchunguzi ufanyike kikamilifu, uwazi na ushahidi utakaochukuliwa uwe unaotumika iwapo italazimika kufikia hatua hiyo katika muhimili wa kisheria.

“Tunataka tufanye kazi kikamilifu, kwa kiwango kwa sababu tunajua tutapimwa kwa viwango, ndani na nje ya nchi, hiyo tunajua. Tusipimwe kabla hatujaanza mtihani, tufanye mtihani mtupe maksi,” alisema.

“Nichukue nafasi hii kwa niaba ya chama chetu kuwapa pole, kuwatia moyo na kuwafariji, yote mliyokuwa mnayapigania ni ya halali na haki, mmepoteza vijana wenu, mmepoteza viungo na wengine wamepoteza mali zao, poleni sana,  na yote hayo yana mwisho na tutashinda kwa pamoja,”amesema.