Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amemteua Fortunatus Magambo kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF).
Kabla ya uteuzi, Magambo alikuwa Mkurugenzi wa Mipango, Uwekezaji na Miradi katika mfuko huo.
Sambamba na Magambo, Rais Samia pia amemteua Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Plasduce Mbossa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).
Taarifa ya uteuzi huo, imetolewa leo, Alhamisi Desemba 11, 2025 na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Bakari Machumu, akirejea taarifa ya Katibu Mkuu Kiongozi, Dk Moses Kusiluka.
Uteuzi wa Magambo, unaziba nafasi iliyoachwa wazi na Dk Rhimo Nyansaho ambaye Novemba 10, 2025, aliteuliwa kuwa mbunge na baadaye Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.
Dk Nyansaho alihudumu katika mfuko huo kuanzia Mei 26, 2025 alipoteuliwa kwa mara ya kwanza, akitokea Benki ya Azania kwa nafasi ya Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara.
Uteuzi wa Mbossa kuwa Mwenyekiti wa bodi ya Tanesco, anarithi mikoba ya Dk Nyansaho ambaye ndiye aliyekuwa na nafasi hiyo hadi uteuzi mpya unafanyika.
Dk Nyansaho ameiongoza bodi ya shirika hilo, kuanzia Desemba mwaka juzi.