Hesabu za Simba zatua kwa kiungo Mrundi

ACHANA na matokeo ya mwisho iliyoyapata dhidi ya Azam FC kwa kukubali kichapo cha mabao 2-0, uongozi wa Simba umeanza mipango ya kuboresha kikosi hicho kimya kimya, ikianza na kiungo Mrundi wa Fountain Gate, Elie Eldinho Mokono.

Simba iliyopoteza mechi tatu ya nne ilizocheza hivi karibuni, zikiwamo mbili za kimataifa na nyingine kama hizo za Ligi Kuu, imedaiwa imeanza mazungumzo na kiungo huyo mshambuliaji ili kuongeza nguvu kikosini.

Kwa sasa Simba katika eneo hilo linaongozwa na Jean Charles Ahoua ambaye ndiye kinara wa mabao msimu uliopita kwa kupachika mabao 16 kambani na msimu huu hajaanza vyema kwani nafasi hiyo anatumika Morice Abraham na Elie Mpanzu ambaye pia hana mwanzo mzuri na hajapachika bao lolote, licha ya kuasisti mara tatu Ligi Kuu.

Chanzo cha kuaminika kutoka Simba kimeliambia Mwanaspoti, viongozi tayari wameanza mazungumzo na Mokono ili kuangalia uwezekano wa kumnasa dirisha lijalo linalotarajiwa kufunguliwa Januari mwaka huu.

“Ni kweli jina la Mokono limetua mezani kwa viongozi, ni mchezaji anayezungumzwa sana sijajua kama wameanza mazungumzo naye, lakini yupo katika listi ya wachezaji wanaoliwa rada na uongozi,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;

“Simba inafanyiwa maboresho maeneo mengi dirisha lijalo, hii ni kutokana na wachezaji wengi kushindwa kuendana na kasi ya ushindani uliopo ligi kuu, tumecheza mechi chache hatujafanya vizuri ndani na hata kimataifa.”

Chanzo hicho kilisema usajili ulianza kufanyiwa kazi na kocha aliyeondoka pia alitoa pendekezo lake ni maeneo gani yanatakiwa kuboreshwa, lakini Seleman Matola ameupa uongozi ripoti yake nini kifanyike.

“Ni kweli Simba inapitia magumu msimu huu kuanzia benchi la ufundi na hata kikosi kukosa mwendelezo wa ubora, hilo viongozi wameliona na wanalifanyia kazi licha ya hayo yote kuna ripoti nzuri juu ya kuboresha kikosi inafanyiwa kazi,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;

“Usajili hata bila ya kocha unafanyika. Mpira ni mchezo wa wazi kila mmoja ameona timu ina shida eneo gani, pia makocha aliyetoka na aliyepo sasa wametoa ripoti zao ni idara gani zina upungufu hivyo yanafanyiwa kazi.”

Katika Ligi Kuu Mokono amekuwa mmoja ya nyota wa kigeni walio tishio kwa viwango walivyonayo na anajua kufunga, kwani msimu uliopita alifunga mabao saba.