KIUNGO wa Azam, Idd Seleman ‘Nado’ amempiku aliyekuwa nyota mwenzie wa kikosi hicho aliyepo Yanga kwa sasa, Prince Dube na mshambuliaji wa zamani wa Simba, Meddie Kagere ya kufunga mabao mengi zaidi katika mechi ya ‘Mzizima Derby’ tangu mwaka 2020.
Bao alilofunga Nado katika ushindi wa timu hiyo wa mabao 2-0 dhidi ya Simba, Desemba 7 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es Salaam, limemfanya kufikisha manne na kuwapiku Kagere na Dube, ambao kila mmoja wao amefunga matatu tangu mwaka 2020.
Nado alianza kufunga bao la kwanza wakati timu hiyo ilipochapwa mabao 3-2, dhidi ya Simba, Machi 4, 2020, akafunga tena katika sare ya 2-2, Februari 7, 2021, huku la tatu akatupia zilipotoka sare ya kufungana kwa bao 1-1, Julai 15, 2021.
Bao la nne lililomfanya avunje rekodi ya kufunga mabao mengi katika Mzizima Derby, ni la ushindi wa kikosi hicho wa 2-0, Desemba 7, 2025, alipofunga la pili dakika ya 88, baada ya Mkongomani Jephte Kitambala kuitanguliza Azam dakika ya 81.
Kwa upande wa mabao ya Kagere, alianza kuyafunga katika ushindi wa Simba wa 3-2, Machi 4, 2020, akafunga zilipotoka sare ya 2-2, Februari 7, 2021, huku la tatu na la mwisho alilifunga wakati miamba hiyo ilipotoka sare ya 1-1, Julai 15, 2021.
Prince Dube ambaye kwa sasa anaichezea Yanga, amefunga pia matatu katika mechi ya Mzizima Derby wakati akiwa na kikosi cha Azam, akianza kwenye ushindi wa timu hiyo wa 1-0, Oktoba 27, 2022, kisha sare ya kufungana 1-1, Februari 21, 2023.
Bao la mwisho la Dube kuifunga Simba akiwa na Azam kabla ya kuhamia Yanga, lilikuwa la sare pia ya kikosi hicho ya bao 1-1, Februari 9, 2024, alilolifunga kunako dakika ya 14, kisha Simba kuchomoa kupitia kwa Clatous Chama dakika ya 90+2.
Hilo lilikuwa ni pambano la 35 kwa Simba na Azam kukutana katika Ligi Kuu tangu 2008, huku rekodi zikiibeba Simba iliyoshinda 15 dhidi ya saba za wapinzani wao na nyingine 13 zikiisha kwa sare, huku Wekundu wakifunga mabao 48 dhidi ya 33 za Wanalambalamba yenye kuvuna pointi 34 katika mechi hizo 35, tofauti na wenzao walikusanya 58 hadi sasa.
