IGP, DPP kortini wakidaiwa kumshikilia waziri mstaafu kinyume cha sheria

Dar es Salaam. Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali (IGP) na wenzake wawiili akiwamo Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) na Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Kanda Maalumu ya Dar es Salaam (ZCO), wamefikishwa mahakamani kwa madai ya kumshikilia Waziri mstaafu, Geofrey Mwambe kinyume cha sheria.

Shauri hilo la maombi namba 289778/2025 limefunguliwa na Mwambe akiwa mwombaji kupitia kwa wakili wake, Hekima Mwasipu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Dar es Salaam, Kisutu jana Desemba 11, 2025  chini ya hati ya dharura.

Mwambe aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji (TIC), mbunge wa Masasi, Mtwara (CCM), Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na Waziri wa Viwanda na Biashara ameshikiliwa na Jeshi la Polisi tangu Desemba 7, 2025.

Kwa mujibu wa hati ya kiapo inayounga mkono maombi hayo, Mwambe alikamatwa katika makazi yake eneo la Tegeta, usiku wa tarehe hiyo na watu waliojitambulisha kuwa,  maofisa wa polisi, akapelekwa Kituo cha Polisi Mbweni, alikohojiwa kwa tuhuma za uchochezi.

Baada ya hapo, alihamishiwa Kituo Kikuu cha Polisi (Central) kwa usimamizi wa mjibu maombi wa tatu (ZCO) alikohojiwa mara ya pili kwa tuhuma za uchochezi kisha  siku hiyo hiyo ya mahojiano alipelekwa mahabusu katika Kituo cha Polisi Kigamboni.

Kutokana na hali hiyo,  wakili wake Mwasipu kwa niaba yake, amefungua shauri hilo dhidi ya IGP, DPP na ZCO,  akiiomba Mahakama iamuru  Mwambe afikishwe mahakamani na  apewe dhamana kwa masharti yatakayowekwa na Mahakama hiyo.

Akizungumza na Mwananchi, wakili wake Hekima Mwasipu amesema wamefungua maombi hayo mahakamani hapo kwa kuwa Mwambe ameshikiliwa kinyume cha sheria bila kupewa dhamana kwa makosa yanayodhaminika.

“Pale kosa analotuhumiwa mtu anayeshikiliwa na Jeshi la Polisi linapokuwa na dhamana, lakini polisi au wanaomshikilia wanakuwa hawataki kutoa dhamana basi unaweza kupeleka maombi kama haya katika Mahakama ya Wilaya au Mahakama ya Hakimu Mkazi kuomba huyo anayeshikiliwa apewe dhamana na Mahakama,” amesema Mwasipu.

“Utaratibu wa kisheria ni kwamba, mtu anapokamatwa anapaswa kufikikishwa mahakamani ndani ya saa 24 lakini mpaka leo (jana) hajapelekwa mahakamani.”

 Wakili Mwasipu amesema kuwa, maombi hayo yamepangwa kusikilizwa Jumatatu, Desemba 15, 2025  saa 3:00 asubuhi na Hakimu Mkazi Mkuu, Hassan Makube.

Wakili Mwasipu amesema kuwa, alifahamishwa na familia yake, kisha alikwenda kuzungumza na Mwambe uso kwa uso katika Kituo cha Polisi Kigamboni alikopelwa baada ya kukamatwa kwa tuhuma za uchochezi.

Amesema alifanya mashauriano na wanaomshikilia kwa ajili ya dhamana, lakini haikuwezekana na wanaendelea kumshikilia, ndio maana wameamua kuchukua njia ya za kisheria ili pate haki yake ya Kikatiba ya kuwa huru.

Hata hivyo, wakili Mwasipu amesema inadaiwa kuwa Mwambe amehamishwa kutoka katika Kituo cha Polisi Kigamboni alikokuwa anashikiliwa na hawajui amepelekwa wapi.

“Leo asubuhi familia ilimpelekea chakula wakaambiwa kuwa hayupo wameshamtoa, sasa mpaka sasa hivi hatujui yuko katika kituo gani cha polisi. Tunazidi kufuatilia pamoja na familia ili kujua amepelekwa kituo gani cha polisi,” amesema wakili Mwasipu.

Wakili Mwasipu amesema wanaendelea kufuatilia ni kwa  nini mpaka sasa anashikiliwa kwa kuwa, kama kulikuwa na sababu za kuendelea kumshikilia zaidi ya muda huo utaratibu wa kisheria unawataka waombe ruhusa mahakamani.

“Lakini hilo halijafanyika. Sasa tunafuatilia kukutana nao (polisi) watuambie ni kwa nini ni zaidi ya saa  24 bado anashikiliwa ili haki yake ya kuwa huru iweze kupatikana,” amesisitiza wakili Mwasipu.