WAKATI mchezo wa kikapu hapa nchini ukizidi kukua kwa kasi, nyota wa timu ya Stein Warriors Jonas Mushi amewataka wachezaji wazawa wa mchezo huo wasiridhike na kiwango walichonacho.
Mushi anayejulikana kwa jina la ‘KD’, amesema cha muhimu zaidi ni wachezaji kuendelea kufanya mazoezi.
Amesema kufanya hivyo kutaleta ushindani mkubwa kati ya wachezaji wazawa na wale wa kigeni katika ligi za Tanzania.
“Bila kufanya hivi, wachezaji wa kigeni wataonekana kuwa bora zaidi katika michezo wanayocheza,” amesema Mushi.
Kwa mujibu wa Mushi, ujio wa wachezaji wa kigeni katika ligi za Tanzania umetokana na ubora wa Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL).
“Kama sisi tuna uwezo wa kupambana na wachezaji wa kigeni wenye uwezo mkubwa katika ligi zetu, basi hata ligi za nje inaonyesha tunaweza kucheza,” amesema Mushi.
Akizungumzia mwamko wa mchezo wa kikapu nchini, amesema umekuwa mkubwa tofauti na miaka ya nyuma.
“Kikapu kwa sasa imekuwa moja ya kazi kama nyingine, ni kutokana na ligi hiyo kuendeshwa na mdhamini,” amesema Mushi.
Hata hivyo, aliomba Shirikisho la Mpira wa Kikapu nchini (TBF) na BD waendelee kutafuta wadhamini watakaoweza kuendelea kuisapoti mchezo huo nchini.
Na kwa wadhamini waliopo, amesema uongozi wa TBF na BD unapaswa kuwapa ushirikiano.
Mushi aliyewahi kuchezea timu ya Atomic ya Comoro, amesema ligi ya Tanzania ina ushindani mkubwa tofauti na ligi ya Comoro.
Amesema utofauti unatokana na timu zilizoko katika ligi za nchini humo kuwa chache.
