Kijana mkora wa miaka 17 alivyomuua mlinzi Lake Oil

Mwanza. Ni tukio linalofikirisha, pale kijana Method Meshack alipotiwa hatiani na Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, kwa kosa la kumuua mlinzi wa kituo cha mafuta cha Lake Oil mkoani Mwanza, alilolitenda akiwa na umri wa miaka 17.

Awali kulijitokeza utata juu ya umri wake halisi wakati akitenda kosa hilo, akiwa pamoja na kundi la majambazi wenzake; kwani aliieleza Mahakama amezaliwa Julai 2007 wakati mama mzazi alisema amezaliwa mwaka 2006.

Jaji Athman Matuma, anasema hebu idhaniwe alizaliwa Januari 1, 2006 kwa kuwa mama hakumbuki tarehe, basi wakati anatenda kosa alikuwa na umri wa miaka 17 na miezi 9, lakini kama alizaliwa Julai 2007 basi alikuwa na miaka 15 na miezi 4.

Kwa vyovyote vile iwavyo na hata akiegemea maelezo ya wawili hao, licha ya mama na mtoto kutofautiana, Jaji Matuma anasema wakati tukio hilo linatokea usiku wa Oktoba 13, 2023, mshtakiwa huyo alikuwa na umri chini ya miaka 18.

Katika hukumu yake aliyoitoa Desemba 8, 2025 na kuwekwa katika tovuti ya Mahakama leo Desemba 11, Jaji Matuma anasema pale unapokosekana ushahidi halisi kutoka upande wa mashtaka, faida ya mashaka anapewa mshtakiwa.

“Hivyo naamua kuwa Method alitenda kosa la mauaji ya kukusudia akiwa na umri wa miaka 17, miezi 9 na siku 13 kwa kuegemea ushahidi wa mama,” anasema Jaji na kunukuu kifungu cha sheria kinachosimamia mkosaji mwenye umri huo.

Jaji anataja kifungu cha 26(2) cha sheria ya Kanuni ya Adhabu kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022 na 2023, kinachosema adhabu ya kifo haiwezi kutamkwa kwa mtu yeyote ambaye wakati akitenda kosa alikuwa na umri chini ya miaka 18.

Hii ni kwa sababu kifungu cha 197 cha sheria hiyo kinatoa adhabu ya kifo kwa mtu ambaye amepatikana na hatia ya kosa la kuua kwa kukusudia, kama Method.

Lakini kifungu hicho cha Kanuni ya Adhabu anachokinukuu Jaji Matuma kinasema “Adhabu ya kifo haitatamkwa au kuandikwa dhidi ya mtu yeyote ambaye, wakati wa kufanya kosa alikuwa chini ya umri wa miaka 18”

Badala ya adhabu ya kifo, kifungu cha 26(2) kinataka mahakama imuhukumu kuwekwa kizuizini wakati wa msamaha wa Rais, na atawajibika kuzuiwa katika sehemu hiyo na chini ya masharti ambayo waziri mwenye dhamana ya sheria atakavyoamuru.

Kutokana na mwongozo huo wa sheria, Jaji alimuhukumu mtiwa hatiani huyo kuwekwa kuzuizini kwa utashi wa Rais kulingana na kifungu hicho cha 26(2) kadri waziri atakavyoamuru, na akiwa kizuizini, atahesabika yuko katika uangalizi halali.

Method alikuwa ameshtakiwa pamoja na Edwin Mchanga aliyekuwa mshtakiwa wa pili, lakini baada ya Jaji kusikiliza ushahidi wa pande pili na kuuchambua kwa kina, aliona mshtakiwa huyo wa pili hakuwa na hatia.

Ushahidi uliomtia hatiani

Kulingana na ushahidi, marehemu Peter Elias maarufu kwa jina la Budeba alikuwa mlinzi katika kituo hicho cha mafuta kilichopo eneo la Nyatukala na usiku wa manane wa mauaji yake, alikuwa na mlinzi mwenzake, Albert Emmanuel.

Emmanuel aliyekuwa shahidi wa pili wa Jamhuri, alieleza wakiwa hapo walivamiwa na majambazi ambao walianza kumkata kwa mapanga mlinzi mwenzake na alipojaribu kusogea ili kumwokoa, naye karibu akatwe mapanga na mmoja wao.

Lakini Method aliyekuwa mshtakiwa wa kwanza alimwokoa asikatwe na panga kwa kuwaambia wenzake “msimuue huyo ni uncle (mjomba) wangu”, wakati alipojaribu kumuokoa mlinzi mwenzake kwa kuwarushia mawe majambazi hao.

Shahidi huyo alieleza kuwa alipata muda wa kuwaangalia majambazi hao kwa vile kituoni hapo kuna taa kali za umeme eneo lote na katika wote, alimtambua Method, kutokana na mwanga huo na kwa kuwa ni mpwa wake tangu utoto wake.

“Ni mtoto wa dada yangu kiukoo na niliposema msimuue huyo ni uncle wangu nikamkazia macho zaidi na kumtambua,”alieleza Emmanuel na ndipo alifanikiwa kutoroka na kukimbilia polisi ambako alitoa taarifa ya tukio hilo.

Huko Polisi alimtaja Method kama miongoni mwa majambazi aliowatambua na aliporudi eneo la tukio hilo lililotokea saa 8:00 usiku akiwa na polisi, walimkuta mlinzi mwenzake amepoteza fahamu na damu zilikuwa zimetapakaa eneo lote.

Walimwahisha hospitali lakini alifariki dunia baadaye.

Shahidi wa kwanza, Dk Simon Gati alieleza alivyoufanyia uchunguzi mwili wa marehemu, na kueleza ulikuwa na majeraha mbalimbali yaliyosababishwa na kukatwa na kitu chenye ncha kali na kufanya avuje damu nyingi.

Koplo Josephat aliyekuwa shahidi wa nne, alieleza siku ya tukio alikuwa zamu na alimpokea shahidi wa pili usiku huo akieleza kuwa wamevamiwa na majambazi na kumtaja mshtakiwa Method kuwa ndiye aliyeweza kumtambua miongoni mwao.

Kwa upande wake, shahidi wa sita, sajenti Michael alieleza namna yeye na maofisa wenzake walivyokwenda eneo la tukio na kuwa baadaye ndiye aliandika maelezo ya onyo ya mshtakiwa wa kwanza, Method Meshack ambaye alikiri kushiriki kosa hilo.

Katika maelezo hayo yaliyopokewa kama kielelezo, Method anaeleza yeye ndiye aliyepewa kazi kwenda kuchunguza eneo la tukio na namna watakavyoingia na watakavyotoroka, na alikwenda katika kituo hicho na pikipiki na kuweka mafuta.

Alifanya hivyo mara kadhaa mchana na usiku na kuweza kusoma ramani ya namna walinzi wa usiku wanavyofanya kazi yao na kulala, na kisha alirudi na kuwapa mrejesho washirika wenzake kuhusu ramani yote ya eneo na katika maelezo anaeleza.

“Tulienda (siku ya tukio) moja kwa moja hadi kwenye bajaji na kumkuta mlinzi mmoja ambaye alikuwa na silaha bunduki ambapo (anamtaja jina), alimvuta na kuanza kumkatakata mapanga na mimi nilisogea hapo nikamkata panga mara moja.”

Hata hivyo, washtakiwa hao walikanusha kuhusika na tukio hilo ambapo Method katika utetezi wake alidai alihojiwa chini ya mateso makali, lakini alikataa katakata kuhusika lakini polisi walimlazimisha kusaini karatasi ambayo haifahamu.

Akaibua madai kuwa kukamatwa kwake kunatokana na chuki baina yake na afande mmoja ambaye alidai alifanya hivyo baada ya kukataa kumpa hongo mwaka 2019 alipomkamata, akiwa na samaki aliokuwa amewabeba katika pikipiki yake.

Katika hukumu yake, alisema kati ya mashahidi sita wa Jamhuri, ni shahidi wa pili ambaye alidai kushuhudia uhalifu huo na kumtambua Method eneo la tukio na kueleza kuwa mshtakiwa huyo hakuwa mgeni machoni kwake, anamfahamu.

Lakini mshtakiwa alikana kufahamiana na shahidi huyo na kufikia hatua ya kumleta mama yake kama shahidi wake namba tatu na kudai shahidi huyo si ndugu yao, lakini Jaji akasema utetezi huo ulikuja mwisho kujaribu kujinasua.

“Shahidi wa pili anamfahamu mshtakiwa kama mpwa wake na wakati wa mashambulizi kulikuwa na mazungumzo baina ya washtakiwa dhidi ya shahidi, pale ambapo mshtakiwa aliwasihi wenzake wasimuue ni mjomba wake.”

“Kwa ushahidi pekee wa shahidi wa pili, kama utaaminika, unatosha kabisa kumuona mshtakiwa ana hatia bila kuungwa mkono na ushahidi mwingine kwa sababu sheria ipo wazi kwa kuthibitisha kosa si lazima waitwe mashahidi wengi.”

“Ushahidi wa shahidi huyo ni wa kuaminika na wala sioni sababu kwa nini shahidi huyo amtungie tukio zito kama hilo mshtakiwa. Alimtaja siku ileile alivyofika polisi na hata shahidi wa nne wa Jamhuri aliyekuwa zamu alithibitisha hili,” alisema.

Jaji alirejea msimamo katika kesi kati ya Marwa Mwita na mwingine, dhidi ya Jamhuri ambapo mahakama ilisema, “Uwezo wa shahidi kumtaja mshukiwa katika hatua za mwanzo ni uthibitisho muhimu wa uhakika wa kuaminika kwake.”

“Badala yake, ushahidi wa utetezi wa mshtakiwa ulikuwa ni wa kujikanganya kiasi cha kufikia mahali kutoa majibu tofauti kwa maswali yanayofanana wakati akiulizwa maswali ya dodoso na kutoa picha kuwa alikuwa akitunga ushahidi.”

“Alijichanganya hadi na shahidi wake mwenyewe namba tatu ambaye ni mama yake mzazi kuhusu umri wake na mwaka aliozaliwa na kudhihirisha kuwa anatunga ushahidi wa utetezi wake, na hivyo ushahidi wake kuonekana ni uongo wa wazi,” alisema Jaji.

Jaji alisema anaona kuwa ushahidi wa shahidi wa pili wa Jamhuri pekee unatosha kumpata na hatia mshtakiwa ingawa unaungwa mkono na sehemu ya vipande vya ushahidi vya mashahidi wengine wa Jamhuri, akiwamo shahidi namba nne.

Ni kutokana na ushahidi huo, Jaji alisema ameridhika kuwa upande wa mashtaka katika kesi hiyo umeweza kuthibitisha mashtaka hayo pasipo kuacha mashaka kwamba Method Meshack ndiye aliyemuua mlinzi huyo kwa nia ovu.

Jaji alisema kulingana na mazingira ya kesi hiyo, mshtakiwa huyo anaonekana na mhalifu mzoefu kwa kuwa alikiri mwenyewe mahakamani kuwa kuna wakati aliwahi kukamatwa na kushtakiwa kwa unyang’anyi wa kutumia silaha.