Dodoma. Ili kuinua kipato cha wakazi wa Dodoma, mkoa huo umetambulisha kilimo kipya cha zao la kibiashara la tufaa (apple) ambapo kila kaya itatakiwa kupanda miche miwili au zaidi kwa ajili ya kujiongezea kipato kupitia zao hilo.
Mti wa tufaa huanza kuzaa matunda unapofikisha miaka miwili ambapo mti mmoja uliotunzwa vizuri una uwezo wa kuzaa matunda 350 kwa wakati mmoja, ambapo heka moja ina uwezo wa kupandwa miti 450 na kutokana na soko la matunda hayo ndani na nje ya nchi mkulima anakuwa amejikomboa kiuchumi.
Akizungumza wakati wa kutiliana saini makubaliano ya kuuziana miche ya matunda hayo na kampuni ya Tamtam Tanzania Limited leo Alhamisi Disemba 11, 2025 Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amesema zao hilo litakuwa ni la kimkakati kati ya mazao mengine yanayolimwa mkoani Dodoma.
Mkoa wa Dodoma umetiliana saini ya kununua miche 6,000 ambayo itasambazwa kwenye halmashauri za wilaya zote ambapo kutakuwa na mashamba darasa ya zao hilo, ili kuwawezesha wakulima na wadau wengine kujifunza kilimo hicho kupitia wataalamu kutoka Wizara ya Kilimo.
Amesema wakati wanafikiria namna ya kuongeza zao lingine la kimkakati mkoani humo ambalo pia litasaidia kuifanya Dodoma kuwa ya kijani walifikia muafaka wa kupendekeza kilimo cha tufaa, ambacho pamoja na kutunza mazingira lakini pia kitakuwa ni chanzo kizuri za mapato ya familia.
Senyamule amesema wameamua kuanzisha kilimo hicho kwa sababu watu wengi huwa wanapanda miti lakini hawaitunzi kwa sababu huwa wanapewa bure hivyo kupelekea miti mingi inayopandwa kwa ajili ya kutunza mazingira kufa, lakini kwa miti ya matufaa ni tofauti kwa sababu inauzwa bei kubwa hivyo hakuna mtu atakayeiacha ikauke.
“Mche mmoja wa matufaa unauzwa Sh12,000 kwa hiyo sidhani kama kuna mtu atakayekubali anunue miti kwa bei kubwa halafu auache ukauke, na kumbuka soko la matunda haya ni kubwa ndani na nje ya nchi hivyo mbali na kutunza mazingira lakini inaongeza kipato cha familia,” amesema Senyamule.
Aidha ameagiza kila kaya mkoani humo kupanda miti miwili ya matofaa ili kutunza mazingira lakini pia kujiongezea kipato pale itakapokuwa na kuanza kuzaa matunda, ambayo bei yake haipungui Sh1,000 kwa moja.
Amesema zipo aina nyingi za matufaa lakini mkoa wa Dodoma utapanda aina tatu ambazo zimefanyiwa utafiti kuwa zinastahimili hali ya hewa ya mkoa huo na tayari zimeshaonyesha mafanikio makubwa kwa wale ambao walipanda kwa ajili ya majaribio.
Amesema mbali na zao hilo la tufaa kuna mazao mengine ya kimkakati ambayo yanalimwa mkoani Dodoma ambayo ni alizeti, mtama pamoja na zabibu ambalo ni zao pekee linalolimwa mkoani Dodoma.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma, Dk Khatibu Kazungu amesema mkoa wa Dodoma umenunua miche 6,000 ya mitofaa yenye thamani ya Sh72 milioni ili kuinua kipato cha mwananchi wa mkoa huo.
Naye mwakilishi wa kampuni ya Tamtam, Gibson Kalyetekela amesema wanazalisha aina zote za miche ya mitofaa na kampuni inanunua matunda yote yatakayozalishwa nchini, hivyo kuondoa hofu ya kukosa soko la zao hilo pindi wakulima watakapohamasishwa na kulima kwa wingi