Kiungo achana mkataba Fountain Gate

KIUNGO mahiri wa Fountain Gate, Abdallah Kulandana ameomba kuvunja mkataba aliosaliwa nao na klabu hiyo wa muda miezi sita  ili aweze kwenda kujaribu changamoto nyingine nje ya timu hiyo, huku akidaiwa anakaribia kutua Mbeya City.

Kulandana ameitumikia Fountain kwa msimu mmoja na nusu,  ameliambia Mwanaspoti ni kweli ameuomba uongozi na tayari ameanza mazungumzo na moja ya timu inayoshiriki Ligi Kuu Bara.

Licha ya kiungo huyo kusita kuweka wazi ni timu gani anayojiandaa kutua, lakini Mwanaspoti linafahamu  mchezaji huyo yupo katika hatua za mwisho kumalizana na Mbeya City kwani mazungumzo ya pande zote mbili yanaenda vizuri.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kulandana alisema ameamua kufanya uamuzi wa kuvunja mkataba na Fountain  kwa lengo la kujaribu changamoto nyingine nje ya timu hiyo na sio kitu kingine.

“Taarifa iliyopo ni kwamba, mazungumzo baina yangu na waajiri wangu hii ni baada ya kuomba kuvunja mkataba uliobaki wa miezi sita ili nitoke na kwenda kuharibu changamoto nyingine nje ya timu hii,” amesema Kulandana na kuongeza;

“Bado hatujafikia muafaka, lakini naamini hadi dirisha dogo linafunguliwa mambo yataenda kama nilivyopanga hakuna kitakachoshindikana ni Suala la makubaliano.”

Mwanaspoti lilipomhoji juu ya mazungumzo na Mbeya City alisema kuna mazungumzo baina yetu ila dili bado halijakamilika mambo yakienda sawa kila kitu kitawekwa wazi kwa sasa bado ni mchezaji wa Fountain Gate.

“Ni kweli kuna mazungumza yanaendelea na Mbeya City, lakini bado hatujafikia makubaliano nafikiri mambo yakienda vizuri kila mmoja atafahamu kupitia mimi au taarifa kutoka kwa viongozi wa timu hiyo.” alisema Kulandana.

Mbeya City iliyomtambulisha kocha mpya, Mecky Maxime aliyedaiwa amependekeza asajiliwe mashine mpya tano wakiwamo Ladack Chasambi na Awesu Awesu kutoka Simba, huku nyota wengine watatu ikifanywa siri na huenda Kulandana ni kati ya hao.