Kizimbani kwa tuhuma za kuvamia, kuiba mali za Sh1.5 bilioni The Voice

Dar es Salaam. Wakazi wawili wa Kinyerezi, Tumaini Moshi(33) na Gaspar Mmari(24) wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kujibu shtaka moja la unyang’anyi wa kutumia silaha na kujipatia vitu mbalimbali vyenye thamani ya Sh1.5 bilion mali ya Klabu ya The Voice Tz Limited.

Washtakiwa hao wanadaiwa kabla ya kutekeleza wizi huo, waliwatishia watu kwa kutumia mawe, fimbo na nondo ili waweze kujipatia vitu hivyo bila kipingamizi.

Moshi na Mmari,  pia wanakabiliwa na kesi nyingine ya uhaini mahakamani hapo, ambapo ipo katika hatua ya kutajwa.

Wamepandishwa kizimbani leo Desemba 11, 2025 na kusomewa shtaka lao na wakili wa Serikali, Frank Rimoy.

Wakili Rimoy ameieleza Mahakama kuwa washtakiwa hao anakabiliwa na kesi ya Jinai namba 28915 ya mwaka 2025 yenye shtaka moja la unyang’anyi wa kutumia silaha.

Rimoy ameieleza mahakama hiyo, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki na kisha kuwasomea mashtaka.

Akiwasomea hati ya mashtaka, Wakili Rimoy alidai Oktoba 29, 2025 eneo la Kinyerezi katika Klabu ya The Voice Tz Limited, washtakiwa kwa pamoja walifanya unyang’anyi wa kutumia silaha na kisha kuiba vitu vilivyokuwepo katika klabu hiyo.

Alidai kuwa siku hiyo ya tukio, Moshi na Mmari wanadaiwa kuiba viti 350 vya mbao na vya plastiki vikiwa na thamani ya Sh150 milioni.

Pia wanadaiwa kuiba vifaa vya ofisi vikiwa na thamani ya Sh40 milioni.

Iliendelea kudaiwa kuwa washtakiwa hao wanadaiwa kuiba runinga ( Tv) 57, zikiwa na thamani ya Sh480 milioni.

“Washtakiwa hao pia wanadaiwa kuiba Music System wenye thamani ya Sh250 milioni  na POS mashine ikiwa na thamani ya Sh80 milioni” alidai Rimoy

Mshtakiwa Tumaini Moshi( wa kwanza kushoto) anayekabiliwa na shtaka la unyang’anyi wa kutumia silaha katika Klabu ya The Voice, akiwa na mshtakiwa mwenzake katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Mahakama iliendelea kuelezwa kuwa washtakiwa hao wanadaiwa kuiba vyombo vya jikoni vyenye thamani ya Sh25 milioni.

“Vile vile, washtakiwa hao wanadaiwa kuiba vifaa vya baa yenye thamani ya Sh15 milioni” alidai.

Pia  wanadaiwa kuiba vinywaji mbalimbali vyenye thamani ya Sh518 milioni, pia wanadaiwa kuiba fedha taslimu Sh16.9 milioni.

Mahakama ilieleza kuwa jumla ya vitu hivyo vilivyoibiwa vina thamani ya Sh1.5 bilioni, mali ya Klabu ya The Voice Tz Limited.

Hata hivyo, kabla ya kutekeleza wizi huo, washtakiwa hao waliwatishia kuwapiga kwa  kutumia mawe, fimbo na nondo, watu watatu ambao ni Jammy Galus, Masoud Ahmed na Benedict Katarunga  ili waweze kupata vitu hivyo bila kikwazo.

Upande wa Jamhuri ulidai kuwa upelelezi haujakamilika na wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Baada ya kusomewa mashtaka yao, hakimu Nyaki aliwaeleza washtakiwa kuwa shtaka linalowakabili halina dhamana kwa mujibu wa sheria, hivyo wataendelea kubaki mahabusu.

Baada ya kueleza hayo, aliahirisha kesi hadi Disemba 22, 2025 kwa ajili ya kutajwa na kuangalia iwapo upelelezi umekamilika.

Hii ni mara ya pili kwa washtakiwa hao kufikishwa Mahakamani hapo, kwani Novemba 7, 2025 walipandishwa kizimbani na wenzao 95 na kusomewa kesi ya uhaini.

Kesi hiyo ya uchunguzi wa awali (PI) namba 26540 ya mwaka 2025 inasikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Hassani Makube imepangwa kutajwa, Desemba 22, 2025.