Kocha Dar City ajivunia mafanikio NBL 2025

BAADA ya timu ya Dar City kutwaa ubingwa wa Ligi ya Taifa ya Mpira wa Kikapu (NBL) 2025, kocha wa timu hiyo Mohamed Mbwana amesema amepitia mengi katika maisha yake lakini anajivunia mafanikio aliyoyapata akiwa na timu hiyo.

Mbwana ambaye pia ni kocha wa timu ya taifa ya Tanzania, amesema alianza kufundisha timu ya Dar City iliyoshiriki Ligi ya Kikapu ya Daraja la Kwanza mwaka 2022.

Anasema anajivunia timu hiyo ilitwaa ubingwa wa Ligi ya Kikapu ya Daraja la Kwanza mwaka huo na mwaka 2023 ilicheza Ligi ya Kikapu ya Mkoa wa Dar es Salaam (BDL), ikatwaa tena ubingwa.

“Kwa kweli sitasahau historia niliyoiweka kwa timu niliyoipandisha daraja na timu hiyo kutwaa ubingwa katika ligi ngumu ya BDL,” amesema Mbwana.

Akizidi kuelezea, amesema mwaka 2023 katika Ligi ya Kikapu ya Taifa (NBL), timu yake ilishika nafasi ya nne, na katika Ligi ya BDL 2024 ikashika nafasi ya tatu.

Baada ya kushika nafasi ya tatu katika Ligi ya BDL, amesema ilishiriki katika Ligi ya Kikapu ya Taifa (NBL), na mwaka huo ikatwaa ubingwa huo.

Mafanikio ya kocha huyo yameendelea mwaka 2025 baada ya timu yake kutwaa ubingwa wa Ligi ya BDL na pia kubeba taji la Ligi ya NBL.

Kwa upande wa mashindano ya kimataifa, akiwa na timu ya Dar City, amesema timu hiyo ilishiriki mashindano ya Road to BAL Elite 16 kundi D.

Mashindano hayo yaliyofanyika kwenye uwanja wa shule ya kimataifa ya IST, Masaki. Katika mashindano hayo amesema ilifuzu baada ya kuishinda timu ya Djabar ya Comoro kwa pointi 102–50 na timu ya Namuwongo Blazers kutoka Uganda kwa pointi 83–70.

Katika mashindano ya Road to BAL Elite 16 yaliyofanyika nchini Kenya, timu yake ilishika nafasi ya tatu baada ya kuishinda timu ya Ferroviario da Beira kutoka Msumbiji kwa pointi 92–77.

Amesema mafanikio hayo ni ya kujivunia na kwamba anapambana kuona anafanikiwa zaidi katika fani yake uya ukocha.