Kocha Msauzi afunguka ishu ya kutua Simba

WAKATI  kocha wa Stellenbosch, Steve Barker  akipewa nafasi kubwa kurithi mikoba ya meneja, Dimitar Pantev huko Msimbazi, raia huyo wa Afrika Kusini amefunguka kuhusu uvumi huo huku akimtaja Fadlu Davids.

Barker, aliyezaliwa Maseru, Lesotho, anatoka katika familia maarufu katika tasnia ya michezo na sanaa. Yeye ni mpwa wa kocha wa zamani wa Bafana Bafana, Clive Barker, aliyoiwezesha Afrika Kusini kutwaa ubingwa wa AFCON 1996, pia akiwa binamu wa mtayarishaji wa filamu, John Barker.

Akizungumzia na Mwanaspoti kuhusu kutajwa kwa jina lake ndani ya Simba, Barker amesema hiyo ni ishara ya kuheshimika kwa kazi anayofanya ndani ya Stellenbosch. Amesema kufanya kwao vizuri msimu uliopita katika michuano ya CAF ikiwa ni mara yao ya kwanza kushiri, anaamini ni moja ya sababu ambazo zimechochea kuwepo kwa hilo.

Alikumbushia namna walivyokutana na Simba katika hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, akisema kwamba wakati huo Simba ilikuwa chini ya Fadlu Davids ambaye kwa sasa ni kocha wa miamba ya soka la Morocco, Raja Casablanca.

“Tulifanya kila tulichoweza, lakini Simba walikuwa bora. Walitupa upinzani mkubwa na ninamheshimu sana Fadlu (Davids) kwa kazi kubwa ambayo aliyofanya,”  amesema kocha huyo ambaye timu hiyo ilipoteza kwa matokeo ya jumla ya bao 1-0.

Pamoja na kuhusishwa na timu hiyo ya Msimbazi, Barker amesema kwa sasa anabaki mtulivu na anazingatia majukumu yake zaidi ndani ya Stellenbosch. Amesema soka ni kazi ya safari na mabadiliko, hivyo ni jambo la kawaida kwa kocha kutajwa hapa na pale.

“Wakati huja na majibu sahihi, tusubiri tuone nini kitatokea, nisingependa kutia neno zaidi kuhusu hilo, naomba niliache kama lilivyo,† amesema kwa kifupi kocha huyo  anayetambulika huko Afrika Kusini kwa kutoa nafasi kwa vijana.

Barker ndiye  aliyempa shavu kijana wa Kitanzania, Ally Msengi kucheza kwa mara ya kwanza Ligi ya Afrika Kusini, 2020. Licha ya kuwa na umri wa miaka 18 wakati huo, Msengi alikuwa akipata nafasi katika kikosi cha kwanza cha Stellenbosch.

Kwa sasa, Stellenbosch inaongoza kundi C katika Kombe la Shirikisho Afrika, ikiwa na pointi nne baada ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya AS Otohô na sare ya 1-1 dhidi ya Singida Black Stars ya Tanzania.

Habari zinaeleza kuwa Simba tayari walifanya mawasiliano ya awali na Barker baada ya timu hiyo kupoteza kwa mabao 2-1  dhidi ya Stade Malien ya Mali katika Ligi ya Mabingwa Afrika, jambo lililofanya mabosi wa Msimbazi waanze kutafuta mbinu mbadala za kuimarisha benchi lao la ufundi ikiwa ni mechi yao ya pili mfululizo kupoteza.

Hata hivyo, Barker si jina pekee kwenye rada ya Simba. Klabu hiyo pia imehusishwa na Mhispania Toni Casano Cantos, kocha aliyeandika rekodi nzuri akiwa na Atletico Luanda ya Angola katika msimu wa 2020/21 ambapo alishinda mechi 37, akatoa sare 20 na kupoteza 12 katika mashindano yote.

Kwa upande wa Stellenbosch, mafanikio yao mengi yamejengwa chini ya falsafa ya Barker ya kujenga timu yenye roho ya ushindani. Moja ya mafanikio makubwa ya klabu hiyo ni kutwaa Carling Knockout Cup 2023, taji lao la kihistoria ambalo lilibadili kabisa hadhi ya Stellies ndani ya soka la Afrika Kusini.

Barker pia amejizolea sifa kwa kuendeleza dira ya klabu ya kukuza na kuibua wachezaji chipukizi. Wachezaji aliowakuza wameendelea kujiimarisha katika timu mbalimbali kubwa nchini humo, jambo lililowafanya wadau wa soka kumwona kama kocha anayeijenga Stellenbosch kuwa na mipango endelevu.

Huku tetesi zikiendelea, bado hakuna taarifa rasmi ikiwa Barker atasogea Msimbazi au ataendelea na Stellenbosch. Hata hivyo, ukubwa wa kile alichokifanya ndani ya klabu hiyo, kuanzia mafanikio ya ndani hadi kimataifa, kunamfanya kuwa mmoja wa makocha wanaotolewa macho kwa sasa barani.