‘Kwa namba ipi?’ Swali muhimu kabla ya kutuma fedha Tanzania

Katika mazingira ya sasa ya Tanzania, ambako huduma za kifedha za kidijitali kupitia simu za mkononi zimeenea na kuwa msingi wa miamala ya kila siku, kuna hatua ndogo lakini muhimu ya kukumbuka kumwuliza mpokeaji, “nitume kwa namba ipi?” kabla ya kufanya muamala.

Kwa kuzingatia tabia za watumiaji huduma fedha kwa simu nchini, Jambo hili ni muhimu ili kufanikisha muamala wako, bila hivyo wewe mtumaji na mpokeaji mnaweza kujikuta katika sintofahamu, au mpokeaji kushindwa kupata fedha hizo licha ya urahisi wa teknolojia.

Jambo hili linatokana na tabia za watumiaji wa huduma wa kifedha katika maisha yetu ya kila siku ya watumiaji. Kwa mfano hata kabla ya huduma hizi kuongezeka, Watanzania walikuwa tayari na tabia fulani ya matumizi ya simu, ambayo kwa namna moja au nyingine huathiri pia namna wanavyotuma na kupokea fedha kwenye mifumo ya kidijitali.

Kwanza, Watanzania wengi hutumia zaidi ya namba moja kwa wakati mmoja, ambazo hutumiwa kwa sababu tofauti, ikiwa ni pamoja na vifurushi vya bei nafuu, promosheni, au mtu anatumia laini fulani ya simu kwa ajili ya upatikanaji wa mtandao. Haishangazi kukuta mtu anatumia laini tofauti kwa intaneti, laini nyingine kwa kupokea pesa, na laini nyingine kwa mawasiliano ya kawaida.

Katika mazingira haya, iwapo unatuma fedha kabla ya kupata uhakika ni rahisi kukosea, mfano umetuma kwa namba ambayo mpokeaji haitumii mara kwa mara, au laini ambayo pengine haipatikani kwa sehemu aliyopo hakuna mtandao wake, changamoto inatokea kuwa hawezi kuzifikia fedha zilizotumwa.

Pili, wapo ambao wana tabia ya kubadili laini za simu mara kwa mara kwa sababu mbalimbali, kama vile kuibiwa simu, kupoteza laini, au kutumia laini fulani kwa matumizi ya muda na kisha kuiacha. Hali hii imezoeleka kiasi kwamba kwenye simu yako unaweza kuwa umehifadhi namba za rafiki yako kwa majina kama Juma 1, Juma 2, au Juma 3.

Endapo mmekubaliana kumtumia fedha bila kuuliza ni ipi anayotumia kwa sasa, unaweza kujikuta umetuma muamala kwenye namba ambayo haiutumii tena. Ndipo anapokwambia, Ayaa!, Hiyo namba niliiacha tangu mwaka jana,

Tatu, wako watumiaji ambao mara kwa mara husahau neno siri la huduma zao za kifedha, jambo ambalo linaweza kutokana na kiwango cha uelewa, mabadiliko ya kifaa, au sababu nyingine za kawaida za matumizi.

Inapotokea mtumiaji amesahau neno siri, anashindwa kupokea fedha mara moja au analazimika kupitia mchakato mrefu wa kurejesha neno siri hilo. Iwapo umetuma fedha bila kuuliza na kuthibitisha namba ambayo anaweza kuitumia kwa wakati huo, unaweza kujikuta muamala umekwama na mpokeaji hawezi kuufikia kwa haraka.

Nne, katika zama hizi za mikopo kupitia huduma za fedha mtandaoni, wapo watumiaji wa huduma za simu za mkononi ambao wana madeni yanayokatwa moja kwa moja pindi tu fedha inapoingia kwenye laini waliyokopea.

Kiasi chochote kinachoingia hutumika mara moja kulipa sehemu ya deni hilo, bila mpokeaji hata kupata nafasi ya kukitumia kwa madhumuni aliyokusudia. Ndio utasikia mara nyengine mtu akitoa tahadhari mapema: “usitume kwa namba hiyo, nadaiwa.” Lakini iwapo hakusema, na wewe hukumuuliza namba sahihi ya kutumia, unaweza kutuma muamala na mpokeaji asiupate.

Ninachokusudia kusema ni kuwa umakini wakati wa kutuma fedha ni sehemu muhimu ya kufanikisha muamala salama. Swali hili dogo, “nitume kwa namba ipi?”, lina mchango mkubwa katika kupunguza makosa ya kimtandao, kuepusha uwezekano wa kutuma fedha kwa namba isiyo sahihi, na kupunguza upotevu wa fedha au usumbufu unaoweza kujitokeza.

Lengo lake si kumsaidia mtu kuepuka kulipa madeni anayodaiwa kupitia mikopo ya mtandaoni, bali kuhakikisha fedha inamfikia mtu anayekusudiwa.