Dar es Salaam. Mwanasiasa mkongwe na waziri wa muda mrefu, Jenista Mhagama, amefariki dunia akiacha historia ya mwanamke mpambanaji, akitokea kwenye kada ya ualimu hadi kuwa waziri katika awamu tofauti za Serikali.
Mhagama, aliyezaliwa Juni 23, 1967, amefariki dunia leo Desemba 11, 2025, ukiwa umepita mwezi mmoja tangu alipoapishwa kuwa Mbunge wa Peramiho (CCM) kwa mara nyingine, tangu alipochaguliwa kwa mara ya kwanza katika jimbo hilo mwaka 2005.
Spika wa Bunge, Mussa Azzan Zungu, ametangaza kifo cha mbunge huyo kupitia taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Spika, akieleza kusikitishwa na kifo hicho kilichotokea leo jijini Dodoma, huku akitoa pole kwa familia, ndugu na jamaa.
“Kwa masikitiko makubwa, naomba kutangaza kifo cha Mbunge wa Peramiho, Jenista Joakim Mhagama, kilichotokea leo Desemba 11, 2025, jijini Dodoma. Natoa pole kwa waheshimiwa wabunge wote, familia ya marehemu, ndugu, jamaa na wananchi wa Jimbo la Peramiho. Mungu awape moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu,” imeeleza taarifa ya Spika.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa Bunge, kwa kushirikiana na familia ya marehemu, inaratibu mipango ya mazishi na taarifa zaidi zitaendelea kutolewa kwa umma.
Safari ya Mhagama ya utumishi wa umma haikuanzia bungeni, bali darasani kama mwalimu, kazi iliyomjengea misingi ya uongozi, uvumilivu na huduma kwa jamii.
Aliwahi kuwa mwalimu wa sekondari na, baadaye, mratibu wa miradi katika Mamlaka ya Ufundi Stadi (Veta) mkoani Ruvuma, kati ya mwaka 1997 na 2000.
Vilevile, aliwahi kuhudumu kama mwalimu katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Songea. Pia aliwahi kuwa Makamu wa Rais wa Chuo cha Ualimu Korogwe.
Mbali na kufanya kazi kama mwalimu kwa nyakati tofauti, Mhagama amewahi kuhudumu kama Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii.
Baada ya kutumikia kwenye utumishi wa umma kama mwalimu, Mhagama alijitosa kwenye siasa, ambako amedumu kwa zaidi ya miongo miwili, akitumikia kama mbunge na kuteuliwa kuwa waziri katika wizara tofauti.
Mwaka 2000, akiwa na umri wa miaka 33, Mhagama aligombea ubunge wa viti maalumu katika mkoa wa Ruvuma, alishinda. Katika uchaguzi wa mwaka 2005, aligombea ubunge katika jimbo la Peramiho na kufanikiwa kushinda.
Ubunge wa viti maalumu kwa miaka mitano ulimpa uzoefu na ujasiri uliomfanya ajitose katika kinyang’anyiro cha ubunge katika jimbo hilo, na kufanikiwa kumshinda marehemu Profesa Simon Mbilinyi, aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, kwenye kura za maoni za CCM.
Tangu mwaka 2005 hadi Desemba 11, 2025, umauti umemkuta, Mhagama amekuwa mbunge wa Peramiho, akishinda chaguzi zote za ndani na nje ya chama, hivyo kuendelea kuliongoza jimbo hilo kwa miaka 20.
Katika awamu ya pili ya Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, Mhagama aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, nafasi aliyoitumikia kuanzia Januari 2014 hadi 2015.
Baadaye, Kikwete alipandisha kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana na Wenye Ulemavu).
Mwaka 2015, baada ya Rais wa awamu ya tano, hayati John Magufuli kuingia madarakani, alimteua Mhagama kwenye Baraza la Mawaziri akiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, akiwa na uzoefu wa miaka 15 na kuwa mwanamke pekee aliyehudumu kama mbunge kwa muda mrefu.
Katika awamu ya pili ya Magufuli, Mhagama aliendelea kubaki katika wizara hiyo, hadi mwaka 2022 alipoteuliwa na Rais Samia kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora).
Agosti 2024, Rais Samia alimteua Mhagama kuwa Waziri wa Afya, akichukua nafasi ya Ummy Mwalimu ambaye uteuzi wake ulitenguliwa.
Katika baraza jipya la mawaziri lililotangazwa Novemba 17, 2025 na Rais Samia, jina la Mhagama halikuwemo, hivyo alihitimisha muongo mmoja aliotumikia kama waziri katika wizara tofauti.
Jina la Mhagama litabaki kuwa miongoni mwa wanasiasa wanaotambulika kutokana na juhudi zake za kukuza ushiriki wa wanawake katika siasa, ushawishi katika Bunge na uongozi wa sera zinazogusa maisha ya Watanzania wengi.
Katika salamu zake za rambirambi, Rais Samia ameandika katika ukurasa wake wa X akisema:
“Nimepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha Mbunge wa Jimbo la Peramiho, Jenista Joakim Mhagama. Ninatoa pole kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mussa Azzan Zungu, wananchi wa Jimbo la Peramiho, familia, ndugu, jamaa na marafiki.
“Kwa miaka 38, Mhagama amekuwa mwanachama mahiri wa CCM, kiongozi wa vijana, kiongozi wa wanawake, waziri katika awamu mbalimbali na mnasihi wa wengi katika siasa na maisha. Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi.”
Kiongozi mstaafu wa chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, ameeleza kusikitishwa na kuumizwa na taarifa za kifo cha Mhagama, aliyekutana naye bungeni mwaka 2005.
“Nimefanya naye kazi bungeni nilipoingia mwaka 2005 hadi 2020, ingawa Mhagama aliingia mwaka 2000. Tulikuwa wote wenyeviti wa kamati za kudumu za Bunge, tulitaniana na tulisaidiana. Mola amweke mahala pema peponi, nimeumizwa sana. Alikuwa mtu bora kwangu, nawapa pole wananchi wa Peramiho kwa msiba huu mkubwa,” amesema Zitto ambaye ni mbunge wa zamani wa Kigoma Mjini.
Mbunge wa Kasulu Mjini, Joyce Ndalichako, ambaye ni miongoni mwa waliokuwa marafiki wa karibu wa Mhagama, amesema anasikitishwa na kifo cha mbunge mwenzake waliyewahi kuhudumu wote katika Baraza la Mawaziri kwa nyakati tofauti.
“Nimepokea taarifa ya msiba huu kwa masikitiko makubwa. Mhagama alikuwa mtu wa watu, alikuwa anashirikiana na watu wote, alikuwa anayependa kusaidia. Tunamuombea kwa Mungu ampe pumziko la milele,” amesema Profesa Ndalichako.
Pia amemuelezea Mhagama kama mtu mchapakazi anayejitoa katika utekelezaji wa majukumu yake.
“Kama kuna jambo la Serikali linalotaka kufanyika basi mtakaa hata hadi asubuhi ili likamilike. Katika kazi, Jenista alikuwa mchapakazi hasa na alikuwa na wito wa kazi, daima alikuwa anaipenda kazi yake,” ameeleza Profesa Ndalichako.
Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Mugisha Nkoronko, amezungumzia Mhagama akisema alikuwa kiongozi msikivu na alipokuwa Wizara ya Afya, aliratibu udhibiti wa ugonjwa wa Mpox na Marbug.
“Alitupa ushirikiano wa hali ya juu katika mkutano wa maadhimisho ya miaka 60 ya MAT. Alipokea mawazo yetu kwa upole, kila wakati na kwa pamoja tulijadiliana namna ya kuzikabili changamoto za sekta ya afya zilizotukabili.
“Tunasikitika amefariki dunia mapema, tulitamani aendelee kuishi kwa muda mrefu. Tunatoa pole kwa familia, Spika Bunge, wapigakura wake na wananchi wote wa Peramiho,” amesema Dk Nkoronko.
