Zambia. Amsons Group, moja ya makampuni makubwa ya nishati na viwanda kutoka Tanzania, imetangaza ushirikiano mkubwa wa kimkakati na kampuni ya Exergy Africa Limited ya Zambia kwa ajili ya kuendeleza kwa pamoja miradi mipya ya uzalishaji umeme yenye jumla ya megawati 1,300.
Mradi huo wenye thamani ya Dola za Marekani 900 milioni (Sh2.2trilioni) utahusisha MW 1,000 za umeme wa jua na MW 300 za umeme unaotokana na makaa ya mawe, hatua inayotarajiwa kuleta mageuzi katika usalama wa nishati wa Zambia, kukuza viwanda, na kuimarisha ushirikiano wa nishati baina ya nchi za Kusini na Mashariki mwa Afrika.
Kwa mujibu wa pande hizo mbili, ushirikiano huo unachanganya uzoefu wa Exergy katika soko la ndani pamoja na mtandao mpana wa Amsons Group katika eneo la ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini, ili kuanzisha mkondo madhubuti wa miradi ya umeme inayoendana na mahitaji ya muda mrefu ya Zambia.
Akizungumza mjini Lusaka wakati wa hafla ya utiaji saini iliyofanyika Jumanne, Desemba 9, Mkurugenzi Mtendaji wa Amsons Group, Edha Nahdi, alisema makubaliano hayo yanadhihirisha dhamira ya kampuni hiyo kusaidia maendeleo ya kiuchumi na ya viwanda nchini Zambia.
“Zambia ni soko la kimkakati kwetu, na kupitia ushirikiano huu tunaleta miundombinu yetu ya kikanda ya nishati, uwezo wa usafirishaji, na uwekezaji katika nishati safi ili kusaidia maendeleo, uendelezaji wa viwanda, na uthabiti wa umeme nchini Zambia,” alisema.
Naye Mkurugenzi wa Exergy Africa Limited, Bi Monica Musonda, alisifu ushirikiano huo na kuuita hatua muhimu katika juhudi za Afrika kuimarisha muunganiko wa kikanda katika sekta ya nishati na kuboresha upatikanaji wa umeme wa uhakika.
“Ushirikiano huu ni dhamira kubwa kwa sekta ya umeme ya Zambia na mustakabali wa viwanda. Kwa kushirikiana na kundi linalofanya kazi katika masoko mengi Afrika, tuna nafasi ya kusonga haraka, kupunguza hatari za miradi, na kutoa umeme wa uhakika pale unapohitajika zaidi,” alisema.
Kupitia uwekezaji huo uliopangwa, washirika hao wanakusudia kuongeza uwezo wa uzalishaji wa umeme nchini Zambia, kuimarisha uthabiti wa gridi kwa sekta muhimu za viwanda, kufungua fursa mpya za uzalishaji na uchimbaji madini, na kuendeleza ajira pamoja na ustahimilivu wa kiuchumi kwa muda mrefu.
Waziri wa Nishati wa Zambia, Makozo Chikote, ambaye alishuhudia utiaji saini huo, alisifu hatua hiyo akisema inaonyesha imani ya wawekezaji katika sekta ya nishati ya nchi hiyo na inaendana na mkakati wa serikali wa vyanzo mbalimbali vya nishati unaolenga kuimarisha ushiriki wa sekta ya umma na binafsi.
“Ushirikiano huu utasaidia ongezeko la MW 500 za nishati ya jua kuongezwa kwenye gridi ndani ya miezi 18. Ndani ya miezi 24, MW 300 za makaa ya mawe pamoja na zote MW 1,000 za umeme safi wa jua zitakuwa zimewekwa, hatua itakayoiwezesha Zambia kuingia katika hadhi ya kuzalisha umeme wa ziada,” alisema.
Amsons Group kwa sasa inafanya shughuli zake Tanzania, Kenya, Msumbiji, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Zambia, ikitoa zaidi ya ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja 10,000.
Kwingineko katika nishati, kampuni hiyo ina uwezo wa kuhifadhi lita milioni 60 za mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam, biashara kubwa ya mafuta katika ukanda wa Kusini mwa Afrika, na ina moja ya misafara mikubwa ya mizigo binafsi Afrika Mashariki yenye zaidi ya malori 800.
Miundombinu hii mikubwa, kampuni inabainisha, itawezesha upatikanaji wa uhakika wa mafuta kwa ajili ya uzalishaji wa umeme, uhamasishaji wa haraka wa vifaa kwa ajili ya ujenzi wa mitambo ya umeme, na usalama wa muda mrefu wa usafirishaji wa kuvuka mipaka, sambamba na kusaidia malengo ya Zambia ya nishati safi.
Zaidi ya maendeleo ya miundombinu, ushirikiano huo pia umeundwa kuleta manufaa ya kijamii na kiuchumi kwa jamii za Zambia pamoja na faida za kibiashara.
kuelekea kwenye uendelezaji wa muda mrefu na umiliki wa miundombinu muhimu ya nishati ili kukabiliana na uhaba sugu wa umeme katika eneo hilo.
Aidha mbali na uwekezaji wake nchini Zambia Amsons Group hivi karibuni ilipeperusha bendera ya Tanzania katika sekta ya uzalishaji wa saruji baada ya kukamilisha mpango wa ununuzi wa Bamburi Cement Desemba mwaka jana kwa Ksh23.6 bilioni (Sh452.1 bilioni), kuimarisha nafasi yake katika soko la saruji la Kenya.
Kwa kuwa Bamburi Cement tayari inamiliki asilimia 12.5 ya EAPC, Munif atakuwa mnunuzi mkubwa zaidi akiwa na hisa asilimia 41.75.
