Katika mazingira ya maisha yanayobadilika kila siku, swali muhimu ambalo wazazi wengi hujiuliza ni hili: Je, tunawaandaa watoto wetu kukabiliana na changamoto za kiuchumi za kesho?
Gharama za maisha zinaongezeka, matumizi ya pesa kwa njia za kidijitali yanakuwa ya kawaida, na watu wengi hujikuta bado wanalipa madeni wakiwa watu wazima. Katika hali kama hii, elimu ya fedha imekuwa ujuzi muhimu na sio hiari tena. Watoto wanahitaji maarifa ya fedha ili waweze kustawi wanapokuwa wakubwa.
Elimu ya fedha huanza nyumbani hata kabla mtoto hajaingia darasani. Mazungumzo ya wazi kuhusu pesa, thamani ya vitu na kupanga vipaumbele yanajenga msingi wa tabia njema.
Watoto wanaojifunza mapema kwamba pesa ni matokeo ya kazi na lazima zitumike kwa nidhamu hujenga misimamo imara, heshima kwa kazi na uwezo wa kusubiri wanapohitaji kitu muhimu.
Mazungumzo haya yanapojirudia mara kwa mara huwasaidia watoto kuelewa tofauti kati ya matumizi ya lazima na yale ya anasa, na kwa njia hiyo huanza kufanya maamuzi yenye fikra pana badala ya hisia.
Mtoto anapofundishwa kuweka akiba, hata kama ni kiasi kidogo, hujenga nidhamu ya kifedha na uwezo wa kupanga malengo ya muda mrefu.
Kadiri wanavyokua, watoto hugundua kuwa akiba si adhabu bali ni njia ya kujijengea uwezo wa kupata mambo makubwa wanayoyataka baadaye. Hii huwafanya wajue kwamba matumizi mazuri ya pesa ni uamuzi wa kila siku, si tukio la bahati mbaya.
Bajeti pia ni somo muhimu kwa mtoto. Wakati mtoto anapoanza kuandika matumizi yake, kufuatilia kile anachonunua na kufikiria kabla ya kutumia, anajenga tabia ambayo itamfaa sana akiwa mtu mzima.
Mtoto anapogundua kwamba pesa haitoshi kila anapokuwa na tamaa ya kununua kitu, huanza kujifunza kutofautisha kati ya “nataka” na “nahitaji”. Hili humfundisha kupanga na kujiwekea malengo, kama vile kutunza pesa kwa muda fulani ili kupata kitabu kipya au baiskeli.
Ni muhimu kumjaribu mtoto kwa kumpatia pesa ya matumizi ya wiki na kukagua namna alivyozitumia. Ikitokea amezitumia zote ndani ya siku chache, na kukosa pesa ya kutumia siku zinazofuata huwa ni somo lenye thamani kubwa kuliko maneno yoyote ya mzazi.
Kadiri watoto wanavyokua, wazazi wanaweza kuanza kuwaelezea mambo ya msingi kama jinsi benki zinavyofanya kazi, umuhimu wa kuwa na akaunti ya akiba , na hatari za kukopa bila mpango. Unaweza ukaanza kwa kumtengenezea kibubu (saving jar) kumjengea uwezo wa nidhamu ya kuweka akiba kidogokidogo.
Ni vema pia kuwafundisha mifumo rahisi ya uwekezaji kama hati fungani za serikali au mifuko ya pamoja kwa lugha rahisi ili kuwajengea mtazamo chanya kuhusu mustakabali wao wa kifedha.
Kumfundisha mtoto nidhamu wa fedha si suala la kumpa pesa nyingi, bali ni kumjengea uwezo wa kutumia kile alicho nacho kwa hekima. Mafunzo haya hujenga tabia ya kupanga, kuwajibika, kuwa na subira na kushukuru.
Kama taifa, tukiwafundisha watoto elimu ya fedha mapema, tunatengeneza kizazi kitakachokuwa na uwezo wa kujitegemea, kuchangia uchumi na kuchangamkia fursa za baadaye bila hofu.
Elimu ya fedha si ya watu wazima pekee. Ni zawadi tunayoweza kuwapa watoto wetu leo kwa faida ya maisha yao yote.
