BAADA ya mapumziko ya wiki moja, kikosi cha Singida Black Stars kinaingia tena kambini Desemba 14, huku kocha msaidizi wa timu hiyo, David Ouma akieleza mikakati mipya, kabla ya kurejea katika mechi za ushindani kuanzia Januari mwakani.
Kikosi hicho kinarudi tena kambini ikiwa ni wiki moja imepita tangu ichapwe mabao 3-1 na TRA United zamani Tabora United katika mechi ya Ligi Kuu Bara, iliyopigwa kwenye Uwanja wa KMC Complex Mwenge jijini Dar es Salaam, Desemba 6, 2025.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ouma alisema licha ya mechi za ushindani kuwa mbali ila hawajatoa mapumziko ya muda mrefu kwa nyota wa kikosi hicho, kwa sababu lengo ni kuhakikisha wanaendelea vizuri na programu kutokana na ratiba ngumu mbeleni.
“Kuna wachezaji ambao hawako na timu za taifa zinazoshiriki Michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON), sasa tumeona ni vyema waliobaki waendelee na programu maalumu kwa sababu wenzao watakuwa na mechi nzuri na za ushindani walipo,” alisema Ouma.
Ouma alisema wataendelea na mazoezi ya kujiweka fiti kutokana na kundi la wachezaji waliopo, ingawa malengo yao makubwa ni kupata mechi nyingi za ushindani, huku wakisikiliza kama watapata nafasi ya kushiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi.
“Kama tutapata mualiko wa Kombe la Mapinduzi itakuwa jambo jema pia kwetu kwa sababu ni njia nyingine nzuri ya kucheza mechi za ushindani, kwa sasa sisi tutaendelea na maandalizi yetu kama kawaida ingawa ikitokea fursa hiyo tutashiriki.”
Mechi ya kwanza ya mashindano kwa timu hiyo, ni ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya AS Otoho ya DR Congo itakayopigwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex visiwani Zanzibar, Januari 25, 2026, huku kikosi hicho kikiwa hakijashinda hadi sasa.
Singida iliyo Kundi C la michuano hiyo msimu huu, ilianza kwa kichapo cha mabao 2-0, dhidi ya CR Belouizdad ya Algeria, kisha mechi ya pili ikashindwa kutamba nyumbani, baada ya kutoka sare ya bao 1-1 na Stellenbosch ya Afrika ya Kusini.