PEDRO Goncalves ghafla amekuwa mkombozi wa Yanga, hiyo ni baada ya mtangulizi wake, Romain Folz kuchemsha na kusitishiwa mkataba fasta na mabosi wa klabu hiyo kongwe.
Folz aliyetambulishwa Yanga Julai 2025, alisitishiwa mkataba Oktoba 2025 akiwa ameiongoza timu hiyo katika mechi sita za mashindano tofauti akishinda nne, sare moja na kupoteza moja akibeba Ngao ya Jamii. Kati ya mechi hizo, mbili za ligi akianza na ushindi kisha suluhu.
Baada ya hapo, Pedro akachukua mikoba na kuirudisha Yanga katika kicheko kwa kushinda mechi zote nne za ligi. Kimataifa pia ameanza vizuri, ameshinda moja na sare moja, Yanga ikiwa na pointi nne sawa na Al Ahly ya Misri katika Kundi B la Ligi ya Mabingwa Afrika.
Hata hivyo, Pedro anakabiliwa na msala uliowashinda makocha wawili waliomtangulia, Miloud Hamdi na Folz ulioachwa na Sead Ramovic aliyesepa baada ya mechi 10 zikiwamo sita za Ligi Kuu Bara, huku kikosi kikishindwa kuvuka makundi Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita 2024-2025.
Msala aliouacha Ramovic walioushindwa Hamdi na Folz ni ishu ya kupata ushindi mechi nyingi mfululizo za kwanza Ligi Kuu Bara.
Alichokifanya Ramovic katika mechi zake sita za kwanza akiwa Yanga, hata Miguel Gamondi alishindwa kukifanya katika msimu wake wa kwanza 2023-2024. Pia Nasreddine Nabi naye msimu wa kwanza 2021-2022 pale Yanga alishindwa.
Hata hivyo, makocha hao wameacha kumbukumbu nzuri kwa kushinda mataji na kuifikisha mbali timu kimataifa. Nabi aliifikisha Yanga fainali Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2022-2023 kwa mara ya kwanza, huku Gamondi akiipeleka timu hiyo makundi Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2023-2024 baada ya miaka 25 kupita, pia kucheza robo fainali ya michuano hiyo msimu huo.
Mechi ya juzi dhidi ya Coastal Union wakati Yanga inashinda 1-0, ulikuwa ushindi nne mfululuzo Pedro anaupata Ligi Kuu Bara tangu akabidhiwe kikosi hicho, hivyo amebakiwa na dakika 180 sawa na mechi mbili za ligi hiyo kuifikia rekodi ya Ramovic.
Ramovic alifanya hivyo katika mechi sita za ligi alizoongoza akiwa Yanga na alishinda zote msimu wa 2024-2025 alipopokea kijiti cha Gamondi akashinda dhidi ya Namungo (2-0), Mashujaa (3-2), Tanzania Prisons (4-0), Dodoma Jiji (4-0), Fountain Gate (5-0) na Kagera Sugar (4-0).
Kwa upande wa Pedro, ameshinda mechi nne za ligi hadi sasa dhidi ya Mtibwa Sugar (2-0), KMC (4-1), Fountain Gate (2-0) na Coastal Union (1-0).
Hamdi katika msimu wa 2024-2025 alipotua Yanga akichukua mikoba ya Ramovic, mechi ya kwanza alikaribishwa na suluhu dhidi ya JKT Tanzania, hata hivyo zilizofuatia akashinda zote na kutetea ubingwa wa ligi.
Folz yeye alisimamia mechi mbili tu za ligi, alianza na ushindi dhidi ya Pamba Jiji, akatoka suluhu na Mbeya City, safari ikaishia hapo.
Kwa upande wa Nabi aliyeingia Yanga Aprili 20, 2021, alikaribishwa na kichapo kutoka kwa Azam. Baadaye mambo yakakaa sawa na kuacha rekodi nzuri ya kubeba mataji yote ya ndani pia kuiongoza timu kucheza mechi 49 za Ligi bila kupoteza.
Gamondi msimu wa kwanza 2023-2024, aliiongoza Yanga kucheza mechi tatu na kushinda mfululizo dhidi ya KMC (5-0), JKT Tanzania (5-0) na Namungo (1-0), kisha akaenda kupasuka Mbarali mkoani Mbeya mbele ya Ihefu kwa mabao 2-1. Sasa hivi Ihefu inaitwa Singida Black Stars.
Msimu wake wa pili 2024-2025, Gamondi alishinda mechi nane mfululizo za ligi dhidi ya Kagera (2-0), KenGold (1-0), KMC (1-0), Pamba Jiji (4-0), Simba (1-0), JKT Tanzania (2-0), Coastal (1-0) na Singida Black Stars (1-0). Baada ya hapo, vichapo viwili mfululizo dhidi ya Azam (1-0) na Tabora United (3-1) ambayo sasa inatiwa TRA United vikahitimisha safari ya Gamondi Yanga. Ndipo akatua Ramovic aliyeacha msala huo unaomkabili Pedro kwa sasa.
KAULI YA PEDRO KWA MECHI NNE
“Tumemaliza hili kwa ushindi, tunakwenda kwenye mapumziko, baada ya hapo tunapaswa kurudi na nguvu mpya ya kumalizia msimu kwani tuna msimu mgumu sana mbele yetu.
“Kila mechi ina mbinu yake, tutaangalia ni aina gani mpinzani anakuja mbele yetu kuweka mikakati ya ushindi. Hatuhitaji kukwama kwa namna yoyote,” amesema Pedro.
