Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Tanzania limeeleza hali ya usalama inaendelea kuimarika kutokana na ushirikiano wa wananchi katika kuepuka vitendo vya uvunjifu wa amani.
Taarifa ya jeshi hilo iliyotolewa na msemaji wake, David Misime leo Alhamisi Desemba 11, 2025, imeeleza ulinzi na doria unaendelea katika maeneo mbalimbali nchini huku hali ikiendelea kuwa salama na yenye amani.
Jeshi hilo kufuatia vitisho vya maandamano yasiyo na kikomo yaliyotangazwa kwa njia ya mitandao ya kijamii kufanyika kuanzia Desemba 9, 2025, limeendelea kuimarisha ulinzi huku wananchi wakitakiwa kuchukua tahadhari za kiusalama katika maeneo yao.
Hatua hiyo imechukuliwa baada ya tukio la vurugu zilizotokana na maandamano ya Oktoba 29, 2025, ambalo lilizua taharuki na kuendeleza wasiwasi kuhusu usalama wa raia na mali zao.
Pamoja na taarifa mbalimbali ambazo zimeendelea kutolewa na jeshi hilo, katika taarifa iliyotolewa leo, msemaji wa jeshi hilo imewahakikishia wananchi, vyombo vya ulinzi na usalama vinaendelea kulinda amani, utulivu na usalama wa Taifa kwa kushirikiana nao.
Aidha, taarifa hiyo imewatoa hofu wananchi licha ya vitisho vya maandamano kutoka mitandaoni, Tanzania imeamka salama na shwari, ishara ya mafanikio ya ushirikiano kati ya raia na vyombo vya dola.
“Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama vinaendelea kulinda amani na usalama wa nchi pamoja na maisha na mali za wananchi,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Taarifa hiyo ya hakikisho la usalama inakuja ikiwa katika siku za hivi karibuni, kumekuwa na ongezeko la doria za askari katika maeneo ya masoko, vituo vya mabasi, barabara kuu na mitaa yenye mikusanyiko mikubwa ya watu.
Hatua hizo zimeelezwa ni za tahadhari dhidi ya uwezekano wa vitendo vya uvunjifu wa amani kufuatia wito wa maandamano ulioenezwa kupitia mitandao ya kijamii na baadhi ya makundi yasiyojulikana.
Hata hivyo, Jeshi la Polisi limewataka wananchi kuendelea kuzingatia kanuni za kiusalama, kutii sheria, na kukataa ushawishi wa kuchochea vurugu au kusambaza taarifa za uzushi na uchonganishi.
Aidha, limeendelea kuonya dhidi ya matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii kwa lengo la kuchafua taswira ya taifa au kueneza hofu miongoni mwa jamii.
“Tuendelee kuwakataa na kuyapinga yale yenye mwelekeo wa uchonganishi, uzushi, uongo na chuki baina yetu,” imeeleza taarifa hiyo, ikisisitiza umuhimu wa mshikamano wa kitaifa.
Sambamba na tahadhari hizo za kiusalama, hali katika maeneo mengi nchini imeendelea kuwa tulivu wananchi wameonekana kurejea katika shughuli zao za kila siku bila hofu, tangu jana Jumatano Desemba 10 2025 huku biashara zikiendelea kama kawaida.
Maeneo ya majiji na miji mikubwa yakiwemo Dar es Salaam, Arusha, Mbeya, na Mwanza shughuli za biashara, usafiri wa umma na kazi mbalimbali za watu kujipatia kipato zimeshuhudiwa kurejea kikamilifu kama ilivyokuwa awali.