Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema, amepokea kwa masikitiko kifo cha mbunge wa Peramiho (CCM), Mkoa wa Ruvuma, Jenista Mhagama kilichotokea leo Alhamisi Desemba 11, 2015 jijini Dodoma.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa umma na Kitengo cha Mawasiliano na Elimu kwa Umma, Ofisi ya Bunge, Spika wa Bunge, Mussa Zungu ametangaza kifo cha mbunge huyo kilichotokea leo jijini Dodoma.
“Kwa masikitiko makubwa naomba kutangaza kifo cha Mbunge wa Peramiho Mheshimiwa Jenister Joakim Mhagama kilichotokea leo Desemba 11, 2025 jijini Dodoma.”
Ofisi ya Bunge kwa kushirikiana na familia ya marehemu inaratibu mipango ya mazishi na taarifa zaidi zitaendelea kutolewa.
Kupitia kurasa zake za kijamii, Rais Samia ameweka picha ya Jenista na kuandika: “Nimepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha Mbunge wa Jimbo la Peramiho, Mheshimiwa Jenista Joakim Mhagama.
Ninatoa pole kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Mussa Azzan Zungu, wananchi wa Jimbo la Peramiho, familia, ndugu, jamaa na marafiki.
“Kwa miaka 38, Mheshimiwa Mhagama amekuwa mwanachama mahiri wa Chama cha Mapinduzi (CCM), kiongozi wa vijana, kiongozi wa wanawake, waziri katika awamu mbalimbali na mnasihi wa wengi katika siasa na maisha. Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi.
Jenister Mhagama, alikuwa Mbunge wa Peramiho, aliyejijengea sifa kubwa kwenye siasa za Tanzania kupitia safari yake ya kiserikali iliyojaa vyeo vyenye umuhimu wa kitaifa na kikanda.
2000 – Mbunge wa Viti Maalumu alipoteuliwa kwa mara ya kwanza.
2005 – Mhagama alichaguliwa kuwa Mbunge wa Peramiho kuwakilishwa wananchi wake katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa miaka mingi, amekuwa mstari wa mbele katika kuwakilisha masilahi ya wafuasi wake na maendeleo ya jimbo lake.
2014 – 2015 – Baada ya kuonyesha ubora katika siasa za Bunge, Mhagama aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi wadhifa uliompa nafasi ya kushirikiana na wizara katika kuboresha elimu ya ufundi nchini.
2015 – 2020 – Katika Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli (hayati), Mhagama aliteuliwa kuwa Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu. Hapa alishughulikia sera muhimu za ajira, masuala ya Bunge na masuala ya vijana na walemavu, akijitahidi kuboresha mfumo wa ajira na kushirikisha vijana katika maendeleo.
2020 – 2024 – Mhagama alihamishiwa katika Ofisi ya Rais kama Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais akilenga kuongeza uwajibikaji na uwazi wa Serikali kwa wananchi. Katika kipindi hiki, alichangia katika kuboresha utendaji wa mashirika ya umma na kufanikisha sera za uwajibikaji wa Serikali.
Agosti 2024 – Rais Samia Suluhu Hassan alimteua kuwa Waziri wa Afya, nafasi ambayo amejitahidi kuitumia kuboresha huduma za afya, kupunguza changamoto za uhaba wa madaktari na kuongeza upatikanaji wa dawa na huduma za afya kwa wananchi.
Juni 2025 – Kati ya mafanikio yake ya kikanda, Mhagama alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri wa Afya (Regional Steering Committee – ResCo) Ukanda wa Mashariki mwa Afrika, nafasi inayomuwezesha kushirikiana na mawaziri wenzake wa Kiafrika katika kuboresha sekta ya afya kieneo.
Jenista Mhagama alijipatia sifa ya kuwa kiongozi wa karibu na wananchi wake, na ni mmoja wa wanasiasa wanawake wenye ushawishi mkubwa nchini Tanzania. Safari yake inaonyesha ukuaji wa kiserikali kutoka mbunge wa jimbo hadi waziri wa afya mwenye jukumu la kikanda.