Serikali yaziwekea mkakati nafasi za masomo nje ya nchi

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Elimu imeandaa mkakati maalumu unaolenga kuhakikisha inazitumia vyema fursa za ufadhili wa masomo zinazotolewa katika nchi mbalimbali.

Mkakati huu umekuja kufuatia Tanzania kutonufaika na baadhi ya fursa nyingi zinazotolewa kutokana na kukosekana kwa taarifa au wanaopata taarifa kutokidhi vigezo vinavyopangwa katika ufadhili husika.

Akizungumzia hilo Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolfu Mkenda amesema wizara yake imeanza kutekeleza mkakati huo kuhakikisha kila nafasi ya ufadhili inayotolewa inapata mnufaika.

Mkenda ameyasema hayo muda mfupi baada ya kufanya mazungumzo na Balozi wa Saudi Arabia nchini Tanzania, Yahya Bin Ahmed Okeish yaliyojikita katika ushirikiano wa kielimu baina ya mataifa hayo.

Saudi Arabia ina mpango wa kutoa nafasi 127 za ufadhili wa masomo ikiwa ni ongezeko la nafasi 37 kutoka 90 zilizokuwa zikitolewa hapo awali.

Akizungumza baada ya mazungumzo hayo Waziri Mkenda amesema kwa sasa hakuna nafasi ya ufadhili wa masomo itakayopotea bila kuwepo watu wenye sifa za kuijaza.

Amesema; ”Kwa muda mrefu tumekuwa tukipata nafasi za ufadhili, lakini baadhi  tunashindwa kuzifikia, wakati mwingine ni kukosekana kwa taarifa au kutokidhi vigezo, tunataka kulifanyia kazi kikamilifu hili suala kwa kutengeneza vijana wetu kabla ya kuziomba hizo nafasi.

“Niliwahi kukutana na balozi wa nchi fulani akaniambia nyie Tanzania mnaziachia nafasi za ufadhili, wenzenu Kenya na Uganda wanazichangamkia hili lazima tulifanyie kazi.”

Amesema wizara yake imeanza kutekeleza programu ya kuwakusanya wahitimu wa kidato cha sita waliofanya vizuri zaidi kwenye masomo yao katika fani mbalimbali na kuwaandaa kwa ajili ya fursa za masomo nje ya nchi.

“Tumeanza na vijana 50, tuliwapata kupitia Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta), hawa tunawaandaa kwenda kusoma masuala ya teknolojia na hili litafanyika katika fani zote tukiwaweka tayari na kuwawezesha pale inapotokea, labda ufadhili unataka ajilipie mwenyewe gharama za nauli.

“Hili litatoa fursa kwa vijana wa Kitanzania waliofanya vizuri bila kujali ametoka kwenye familia duni kiasi gani, atapata nafasi ya kwenda kusoma nje ya nchi akifanikiwa kukidhi vigezo vya ufadhili tofauti na ilivyo sasa tunaona wengi wanaokwenda ni kutoka kwenye familia zenye uwezo,” amesema Profesa Mkenda.

Wakizunguzia hilo wadau wa elimu wamesema  mpango huo ni mwanzo wa mageuzi muhimu katika elimu ya Tanzania.

Wadau hao wamebainisha kuwa endapo mkakati huo utatekelezwa kwa umakini na kuhusisha ngazi zote kuanzia shule za msingi hadi vyuo vikuu Tanzania inaweza kuanza kuonekana kama Taifa linalotumia kikamilifu fursa za kimataifa, na si kuziacha zipotee kama ilivyokuwapo hapo awali.

Akizungumzia hilo Dk Fausta Lema amesema  mkakati huo unamaanisha kuweka msingi mpya wa usawa.

“Kwa miaka mingi tumeshuhudia wanaokwenda nje wakiwa hasa watoto wa familia zenye uwezo. Uamuzi wa Serikali kutengeneza mfumo wa ushindani unaotegemea uwezo wa kitaaluma na si uwezo wa kifedha utachochea morali kwa wanafunzi,” amesema Dk Lema.

Kwa upande wake Bahati Msonde ambaye ni mwalimu wa sekondari amesema  mafanikio ya mpango huo  yatahitaji maboresho ya mazingira ya kujifunzia nchini.

“Maandalizi ya vijana wasomi kwenda nje hayapaswi kuanza baada ya mtihani wa kidato cha sita pekee, bali katika hatua za chini kwa kuimarisha ufundishaji wa sayansi, lugha za kimataifa na teknolojia.

“Mfumo wa maandalizi ni mzuri, lakini lazima tuwekeze kwenye maabara, vitabu na walimu wa kutosha nchini. Bila hapo, tunaweza kuwaandaa vijana wachache tu badala ya wengi,” amesema Msonde.

Akizungumza na Mwananchi,  Ernest Masha ambaye ni mzazi licha ya kuipongeza Serikali kwa kufungua milango kwa vijana kutoka familia zisizo na uwezo amesema  bado ipo haja ya kuweka mfumo shirikishi utakaojenga uelewa mpana kuhusu fursa hizi.

“Kama changamoto ni ukosefu wa taarifa, basi Serikali ifike mpaka kwenye vijiji. Wengi tunasikia nafasi hizi zikitajwa kwenye vyombo vya habari baada ya muda kupita,” amesema Masha mkazi wa Temeke.