Taji la Cecafa lampa mzuka Eliza

NAHODHA wa timu ya taifa ya Tanzania ya wasichana, Elizabeth Chenge amesema ilikuwa lazima wanyakue ubingwa wa Mashindano ya Shule ya ‘CECAFA Zonal CAF African Schools Football Championship’ kutokana na historia ya Tanzania kwenye mashindano ya CECAFA.

Mashindano hayo ya timu za Shule yalifanyika Uganda kuanzia Desemba 6-9 na Tanzania ilipangwa Kundi B na Ethiopia, Sudan Kusini na Djibouti.

Tanzania ilinyakua ubingwa huo baada ya kuitandika Ethiopia kwa penalti 5-4 kutokana na kutoka suluhu katika muda wa kawaida, hata hivyo kwa upande wa timu ya taifa ya wavulana ikimaliza mshindi wa pili.

Akizungumza na Mwanaspoti, Chenge alisema Tanzania inapokutana na timu za ukanda wa CECAFA imekuwa ikifanya vizuri jambo lililowapa hamasa ya kupambana ili kuendeleza rekodi hiyo.

Alisema ubingwa walioubeba una maana kubwa kama mabinti wanaoanza karia ya soka la wanawake na unawapa uzoefu wa kukutana na timu ngumu za ukanda huo.

“Kwetu ni jambo kubwa kwa sababu kuna wachezaji ndio mara yao ya kwanza kucheza mashindano ya kimataifa vile vile yanatupa taswira ya tunaanzaje karia yetu ya soka,” alisema Chenge na kuongeza;

“Pia ni sehemu ya sisi kujulikana mbali na kuendeleza rekodi ya CECAFA kwa sababu hata tutakapoendelea kucheza mashindano mengine kuna mawakala waliotoka sehemu mbalimbali wanatutazama ni fursa kwetu.”