TMA: Mvua zitakazoambatana na radi kuanza leo maeneo mbalimbali nchini

Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imetangaza kuanza kwa mvua zitakazoambata na radi mikoa mbalimbali nchini kuanzia leo Desemba 11 hadi 20, 2025.

Katika taarifa yake TMA inaonesha kuwepo kwa vipindi vya mvua zilizoambatana na ngurumo za radi katika maeneo ya Ziwa Victoria, Magharibi mwa nchi na nyanda za juu Kusini-Magharibi huku maeneo machache ya pwani na nyanda za juu Kaskazini-Mashariki kupata mvua kwa kiwango kidogo.

Maeneo hayo ni Kanda ya Ziwa Victoria ambapo mikoa ya Kagera, Geita, Shinyanga, Mwanza, Simiyu na Mara, kutakuwa na mvua zinazoambatana na ngurumo za radi zikitarajiwa katika maeneo machache.

Nyanda za juu Kaskazini- Mashariki (Mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro) mvua zinatarajiwa katika maeneo machache.

Pwani ya Kaskazini (Mikoa ya Tanga, maeneo ya kaskazini mwa Morogoro, Pwani na Dar es Salaam pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba) mvua zinatarajiwa katika maeneo machache.

Huko Magharibi mwa nchi (Mikoa ya Kigoma, Katavi na Tabora): Mvua zinazoambatana na ngurumo za radi zinatarajiwa katika maeneo machache.

Aidha Kanda ya Kati (Mikoa ya Dodoma na Singida): TMA imesema mvua zinatarajiwa katika maeneo machache.

Nyanda za juu Kusini-Magharibi (Mikoa ya Rukwa, Songwe, Mbeya, Njombe na Iringa): Mvua zinazoambatana na ngurumo za radi zinatarajiwa katika maeneo machache.

Pwani ya Kusini (Mikoa ya Mtwara na Lindi), mvua zinatarajiwa katika maeneo machache. Kanda ya Kusini (Mkoa wa Ruvuma na maeneo ya Kusini mwa Morogoro mvua zinatarajiwa katika maeneo machache.

Ikitoa matarajio ya hali ya hewa kuanzia leo Desemba 11 hadi 20 mamlaka hiyo imesema katika kipindi hiki, migandamizo mikubwa ya hewa iliyopo kaskazini mwa dunia (Azore na Siberia) inatarajiwa kuendelea kuimarika wakati ile iliyopo kusini mwa dunia (St. Helena na inatarajiwa kuendelea kudhoofika.

Hali hii inatarajiwa kusababisha sehemu ya ukandamvua (ITCZ) kusogea kuelekea kusini na kuwepo katika maeneo ya ukanda wa Ziwa Victoria, magharibi mwa nchi, kati, nyanda za juu kusinimagharibi na kusini mwa nchi, hali inayotarajiwa kuimarisha mifumo isababishayo mvua katika maeneo hayo.

“Vilevile, uwepo wa upepo wenye unyevunyevu uvumao kutoka baharini kuelekea maeneo ya ukanda wa pwani ya nchi yetu unatarajiwa kuimarisha mifumo isababishayo mvua katika maeneo hayo,” imebainisha TMA.