Uhaba wa maji Dar unavyobadilisha mfumo wa maisha ya wananchi

Dar es Salaam. Changamoto ya upatikanaji wa huduma maji safi na salama imeendelea kuathiri mfumo wa maisha ya baadhi ya wakazi wa Dar es Salaam na kusababisha mabadiliko ya shughuli zao za kila siku, uchumi wa kaya na afya za wakazi.

Kwa wiki kadhaa sasa, baadhi ya maeneo yamekuwa yakikabiliwa na adha hiyo, hali inayowalazimu kubadili ratiba zao na kutumia muda mwingi kutafuta huduma hiyo muhimu.

Maeneo kama Tabata, Kariakoo, Segerea, Temeke na mengineyo, wakazi wake wamekuwa wakiamka alfajiri kusaka huduma hiyo na wengine kusubiri kwenye visima ambavyo hutoa maji kwa muda usiotabirika.

Wakizungumza na Mwananchi leo Desemba 11, 2025, wananchi  hao wamesema hali hiyo imekuwa ikiathiri shughuli zao nyingine kama kufika kazini kwa wakati, kufanya usafi wa nyumbani na uendeshaji wa biashara ndogondogo zinazohitaji maji ya kila siku.

Mirafat Juma, mkazi wa Tabata Kimanga, Mtaa wa Magufuli amesimulia namna wanavyopitia magumu baada ya kukosekana kwa huduma hiyo kwa takribani wiki tatu mfululizo, hali ambayo imeathiri maisha ya familia, biashara ndogondogo na usafi wa watoto waliopo likizo.

Juma amesema maisha yamevurugika kiasi cha kulazimika kuhamishia baadhi ya shughuli zao za msingi kwa mzazi wake anayeishi Kinyerezi ambako angalau wanapata maji ya kisima.

“Ni wiki ya tatu mfululizo hatujapata maji. Tanki langu la lita 1,000 limeisha. Tumelazimika kwenda kuoga kwa mama Kinyerezi na kuomba hata madumu mawili ya lita 20 ili tupate maji ya dharura,” amesema.

Kwa upande mwingine, watoto waliopo likizo wamejikuta wakibeba majukumu ya kutafuta maji kwenye nyumba zenye visima.

Juma amesema ndoo ya lita 10 huuzwa Sh100, lita 20 huuzwa Sh200 huku wauzaji wa mkokoteni wakiuza dumu moja la maji ya chumvi kwa Sh500.

“Hawa watoto kila asubuhi wanatoka kutafuta maji. Sio kwamba wanapenda, ni mazingira yanayowalazimu,” amesema Juma.

Amesema familia nyingi sasa zimepunguza matumizi ya maji kwa kiwango kikubwa, hawajafua kwa wiki tatu huku kuoga kukifanyika mara moja tu kwa siku ili kuokoa kiasi kilichobaki.

Juma amesema hulazimika kuagiza maji kutoka kwa wauzaji wa maboza kwa Sh17,000 kwa lita 1,000, bei inayoongezeka kutokana na umbali na uhitaji wa wateja wengi ili gari lifike.

Athari za ukosefu wa maji zimegusa pia wafanyabiashara wadogo, Maria Singael mfanyabiashara wa barafu, amedai amelazimika kusitisha shughuli zake kwa muda kutokana na kukosa majisafi ya kuzalisha barafu hizo.

“Nauzia wafanyabiashara barafu kwa ajili ya vinywaji na juisi. Sasa hivi siwezi kuuza barafu ya maji ya chumvi, lazima nisubiri maji yarudi,” amesema Singael akieleza kuwa, biashara hiyo ndiyo chanzo chake kikuu cha kipato cha kila siku.

Singael aliyekuwa akiuza barafu kwa bei kati ya Sh500 hadi Sh2,000 pamoja na ‘ice cream’ za vifuko, amesema amepoteza mapato yote kutokana na changamoto ya maji.

Jacob Mbawala, mkazi wa Mtaa wa Aman Tabata, amesema: “Bora ukose umeme kuliko maji. Huduma ya maji ni muhimu ili uende chooni au bafuni, unahitaji maji, kupika na shughuli zingine.”

Amesema wanachopitia sasa ni unyanyasaji wa haki za binadamu, wanamaliza wiki mbili sasa hawapati huduma hiyo ingawa wamekuwa wakisikia kutakuwa na mgao wa maji lakini, hakuna wanachokiona.

Hata hivyo, jana, Desemba10, 2025 akizungumza na waandishi wa habari, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso alisema operesheni wanazofanya sasa zimeanza kuleta matunda na kipaumbele chao kiwango cha uzalishaji maji kinachopatikana kigawiwe kwa usawa.

“Ni maelekezo kwa Dawasa, kiwango hiki cha maji kigawiwe kwa usawa na viongozi wajitahidi kusimamia kila eneo lifikiwe na maji kama kesho watapata hawa kesho watapata wale kwa kuzingatia kiwango kilichopo na mazingira ya sasa,” alisema.

Kwa mujibu wa maelezo ya Aweso, wananchi wanatakiwa kujenga utamaduni wa kuhifadhi maji ili yawasaidie kuvuka katika kipindi hiki cha mpito.

“Wakazi wa Dar es Salaam niwaambie hiki ni kipindi cha mpito na faraja tunayoipata baadhi ya maeneo mvua imeanza kunyesha naamini kwa mvua zilizoanza kunyesha maji yataanza kupatikana kwa wingi,” alisema.

Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Wami-Ruvu, Elibariki Mmasi alisema katika kukabiliana na tatizo hilo, kwanza wamesitisha shughuli zinazotegemea matumizi ya maji ya majumbani.

“Kinachofanyika kwa sasa kupita maeneo yote kufanya doria na kiwango cha maji kimeongezeka naamini matumizi ya maji yataanza kurudi kawaida muda si mrefu,” alisema Mmasi.

Alisema taasisi hiyo inaendelea kutoa wito kwa wananchi wanaoishi karibu na vyanzo vya maji kuwa wastamilivu katika kushirikiana kulinda vyanzo hivyo.

“Maeneo yaliyokuwa yanapoteza maji tumeyazuia na yameanza kutumika kwa matumizi ya majumbani,”alisema.

Serikali kupitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa), ilikamilisha ujenzi wa tanki jipya la kuhifadhi maji la Bangulo lenye ujazo wa lita milioni tisa, lililopo Kata ya Pugu Station, mradi uliogharimu Sh36.8 bilioni

Kazi za ujenzi huo zilijumuisha pia ujenzi wa kituo cha kusukuma maji na ulazaji wa mtandao wa kusambaza maji wenye urefu wa kilomita 108; huduma inayotarajiwa kuanza rasmi mwishoni mwa Februari 2026.

Mradi huo mkubwa umejengwa kwa lengo la kuboresha upatikanaji wa maji katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam, hususan kata za Mzinga, Kipunguni, Kitunda, Pugu Station, Kiluvya, Msigani na Kinyerezi, huku takribani wakazi 450,000 wanatarajiwa kunufaika.

Pia, utekelezaji wake ulilenga kuhakikisha wakazi wa majimbo ya Segerea, Ilala, Ubungo, Kibamba na Temeke wanapata huduma ya maji kwa uhakika na uhakika wa kudumu.

Katika kuendeleza jitihada za upatikanaji wa huduma hiyo, Serikali imeendelea kusukuma jitihada za kupanua na kuimarisha upatikanaji wa maji katika jiji hilo.

Novemba 2, 2022, aliyekuwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alizindua Mradi wa Maji Kigamboni uliolenga kuzalisha lita milioni 70 kwa siku ili kupunguza adha ya upatikanaji wa maji Kigamboni, maeneo ya katikati ya jiji pamoja na Temeke.

Mradi huo ulihusisha ujenzi wa visima saba na tanki lenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni 15, maji hayo yalitarajiwa kuunganishwa na mfumo kutoka chanzo cha Mto Ruvu.

Zaidi ya hapo, Novemba 10, 2022, Waziri Mkuu alikagua na kushuhudia kazi za usafishaji wa visima katika maeneo ya Tabata Relini na Mwananyamala Komakoma, ikiwa ni sehemu ya mwendelezo wa juhudi za Serikali kuongeza upatikanaji wa maji.

Visima hivyo ni miongoni mwa visima 197 vilivyochimbwa mkoani Dar es Salaam, wakati huo jumla ya visima 160 vilikuwa vikizalisha lita milioni 29.4 kwa siku. Maji hayo yaliunganishwa katika mfumo wa usambazaji ili kupunguza changamoto ya upatikanaji wa maji kwa wananchi.

Pamoja na jitihada hizo ambazo lengo lake lilikuwa kukabiliana na adha ya maji hususan nyakati za kiangazi, zimeshindwa kujibu na huduma ya maji imeendelea kuadimika kila uchwao.