Umelala Mhagama, kikokotoo ulipambania | Mwananchi

Dodoma. Ungekuwa ni mchezo wa mpira hapa tungeuliza, eti Zungu umepigaje hapo?

La hasha, huu si mpira, na huyu siyo Zungu bali ni Spika wa Bunge, Mussa  Zungu lakini alichofanya ni kuutangazia umma kuhusu msiba wa Mbunge wa Peramiho, Jenista Mhagama.

Masikini! Mhagama hayupo, Bunge la Januari 2026 hatutamuona mjengoni, hataonekana Peramiho na Ruvuma nzima, ewe Mungu pokea kiumbe wako.

Hivi unajua kila mtu amepewa haki ya kifo, yaani mimi na wewe tutake tusitake lazima tutakufa na hilo halina mjadala, tena katika utamaduni wa Kitanzania lazima tutachimbiwa chini, ohoo, Mungu kwa nini sasa.

Basi ndiyo kusema sisi sote tu makaburi yanayotembea lakini mwenzetu Mhagama tayari amelisogelea kaburi lake, na hatatembea bali atatembezwa kulifikia.

Huyu Jenista Mhagama kwa mara ya kwanza aliingia mjengoni miaka 25 iliyopita akiwa Mbunge Viti Maalumu lakini baadaye akadaka Jimbo hadi leo alipoitwa na Mola wake.

Ametangulia kabla hajashuhudia ndoto ya bima ya afya kwa kila Mtanzania kwani haijatimia, ametangulia kabla utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa haijatimia, lakini ametangulia akiwa amebakiza siku 20 pekee kuufuta mwaka 2025.

Halafu, hivi unajua akiwa Waziri wa Afya ndiye aliyeongoza kampeni za kumfanya Profesa Mohamed Janabi kuwa Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa Ukanda wa Afrika?

Yaani kwa maneno mafupi ni kwamba Mhagama alimsogeza mbali mtu aliyekuwa akitupunguzia Watanzania kula bata, maana kila kitu kwake kilionekana tukila itakuwa ni matatizo.

Ni kama utani vile lakini Mhagama ndiyo hayupo tena, halafu hivi unajua kwamba aliwahi kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora?

Sasa leo msiba wake umetangazwa wakati Waziri Mkuu alipokuwa kwenye mkutano na watumishi na  viongozi wa Sekretarieti ya Maadili kwa Viongozi wa Umma, ambapo Waziri wa Utumishi Ridhiwani Kikwete alikuwepo.

Lakini nikwambie kitu, huwezi kumtaja Mhagama bila kutaja vita yake na Ester Bulaya kwenye mambo ya kikokotoo.

Ni kama bungeni linakuwa jepesi usipomuona Mhagama akiingia kupitia lango C akiwa na mkoba wake mkono wa kushoto, sawa alishaachwa kwenye baraza la mawaziri, je, angeuliza maswali yepi kwa mfano?

Tembea salama wa Peramiho, Mtanzania na mzalendo kindakindaki uliyekipambania chama chako (CCM) ndani na nje ya Bunge, hasa ulipokuwa na hoja za kushindana na kambi ya upinzani nawe ukiwa Waziri wa Sera. Tutakukumbuka daima.