Nairobi. Umoja wa Mataifa (UN) umezindua kikosi kazi kitakacholenga kuhakikisha nchi tajiri kwa madini muhimu (critical minerals) zinanufaika na rasilimali hizo zinazotumika katika mpito wa nishati safi.
Hata hivyo, Tanzania imeunga mkono hatua hiyo ikitoa angalizo juhudi hizo zisigeuke kuwa vikwazo kwa maendeleo ya kiuchumi ya mataifa yenye rasilimali hizo.
Kikosi kazi hicho (global task force) kilizinduliwa Desemba 11 katika kikao cha saba cha Baraza la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEA-7) kinachoendelea jijini Nairobi nchini Kenya kikilenga kusaidia nchi zinazoendelea zinazozalisha madini kama cobalt, lithium na shaba kupata manufaa ya haki katika mnyororo wa thamani wa teknolojia za nishati safi, kidijitali na akili mnemba.
Mwenyekiti wa Jopo la Majadiliano la Afrika (AGN), Richard Muyungi, amesema hatua hiyo inakuja katika kipindi ambacho dunia inapitia mabadiliko makubwa kutoka matumizi ya nishati chafuzi kwenda nishati zisizo au zenye uharibifu mdogo kwa mazingira, na mahitaji ya madini haya yakiongezeka.
“Kwa sasa dunia inakwenda kwenye matumizi ya vyanzo vya nishati vyenye uzalishaji mdogo wa hewa ukaa au hazizalishi kabisa. Madini haya ni muhimu katika kufanikisha hilo,” amesema Muyungi, ambaye pia ni mshauri wa Rais wa Tanzania katika masuala ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi.
Akifafanua zaidi, amesema kinachohitajika si kuwekewa sheria au miongozo mipya itakayoizuia nchi kutumia madini yake, bali kujengewa uwezo ili madini hayo yachangie kuondoa umaskini na kuboresha maisha ya wananchi, kama ilivyotokea kwa nchi za Kiarabu zilizonufaika wakati dunia hapa kutoka kwenye makaa ya mawe kwenda kwenye mafuta.
Hata hivyo, ametoa tahadhari akisisitiza,“…juhudi hizi hazipaswi kuleta masharti yanayoweza kuzuia uhuru wa nchi kama Tanzania kuamua namna bora ya kutumia rasilimali zake kwa ajili ya maendeleo.”
Katibu Mkuu Msaidizi wa Umoja wa Mataifa na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEP), Inger Andersen alisema kikosi kazi hicho kitatumika kuwaongoza watunga sera katika kipindi ambacho ushindani wa kimataifa wa kupata madini muhimu unaongezeka.
Ameonya bila uratibu maalumu, dunia inaweza kuingia kwenye migogoro mipya ya rasilimali zitakazoongeza ukosefu wa usawa na kuharibu mazingira.
Andersen amesema kikosi kazi kitasaidia kuboresha uwazi, kuimarisha kanuni za uchimbaji na kuhakikisha nchi wanachama zinaongeza thamani karibu na maeneo ya uchimbaji badala ya kuendelea kuuza malighafi.
Kikosi kazi hicho kitasimamiwa kwa pamoja na UNEP, Shirika la Umoja wa Mataifa la biashara na Maendeleo (UNCTAD), na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP) na mashirika mengine ya UN, kikitekelezwa kupitia makundi ya kitaalamu yatakayojikita katika kuongeza thamani, kugawana faida kwa haki, ulinzi wa mazingira, uchumi na kuzingatia uchimbaji mdogo.
Mshauri Maalumu wa Katibu Mkuu wa UN kuhusu hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, Selwin Hart, alisema nchi tajiri kwa madini zinatakiwa kuwa katikati ya uchumi wa nishati safi, akionya mara nyingi nchi hizi zinasafirisha malighafi huku zikirudishiwa umaskini, uchafuzi wa mazingira na ajira zisizo salama.
Alisisitiza kuwa hatua hiyo mpya inalenga kutoka kwenye mapendekezo hadi matokeo huku nchi za majaribio zikitarajiwa kutangazwa karibuni.
Naibu Katibu Mkuu wa UNCTAD, Pedro Moreno, amebainisha kikosi kazi hakitaanzisha miundo mipya, bali kitaimarisha uratibu uliopo ili kuhakikisha mpito wa kijani unakuwa pia mpito wa maendeleo.
UN ilisisitiza kuwa mamlaka ya nchi juu ya rasilimali zao itaendelea kuheshimiwa, na lengo ni kusaidia serikali kujadiliana mikataba yenye maslahi mapana kwa wananchi wake.
“Hatupaswi kujenga uchumi wa nishati safi juu ya misingi ya dhuluma iliyokuwepo,” alisema Hart.