Nairobi. Kwenye kikao cha saba cha Baraza la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEA-7) kinachoendelea Nairobi nchini Kenya, viongozi na wadau wametoa wito kwa nchi za Afrika, ikiwamo Tanzania, kujifunza kutokana na urithi wa Wangari Maathai wa Kenya, ambaye alipambana kuunganisha amani, demokrasia, haki za binadamu na uhifadhi wa mazingira.
Kutokana na juhudi hizo mwaka 2004, Maathai alikuwa mwanamke wa kwanza barani Afrika kutunukiwa Tuzo ya Amani ya Nobel.
Kamati ya Nobel ilimtambua kwa mchango wake katika maendeleo endelevu na amani, ikikumbusha ulimwengu kwamba ‘amani duniani inategemea uwezo wetu wa kulinda mazingira yetu’, kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Taasisi ya Wangari Maathai, Wanjira Mathai, aliyekuwepo kwenye hafla hiyo.
Kazi yake iliyoanzia kwenye kurejesha ardhi na misitu iliyoharibika ndiyo iliyozaa Harakati za Green Belt Movement (harakati ya mazingira iliyoanzishwa na Maathai, ikilenga upandaji miti, uhifadhi wa mazingira na uwezeshaji jamii).
Mjumbe wa Tanzania katika UNEA na Mwenyekiti wa Jopo la Majadiliano la Afrika (AGN), Richard Muyungi, amesema Tanzania inaweza kujifunza kutokana na namna Maathai alivyojenga mabadiliko kupitia jamii.
“Tuitambue kwamba utunzaji wa mazingira ndio unaweza kutupa maendeleo endelevu, kama alivyokuwa anapigania Wangari Maathai,” alisema Muyungu kumuenzi Maathai aliyefariki Septemba 2011.
Pia rasilimali nyingi za Tanzania zinaweza kutumiwa kwa tija kwa manufaa ya mazingira na uchumi.
“Tunahitaji mazingira bora kwa kila tunachofanya na tunaweza kutumia rasilimali hizi vizuri kwa maendeleo… tuna bahari, misitu na maziwa. Hizi zinasaidia pia uchumi wa nchi,” alisema.
Muyungi alisema Maathai alionesha jinsi uhifadhi unavyoweza kuwa na manufaa kwa mazingira, jamii na uchumi.
“Mfano yeye ametuachia eneo linalofaa kwa utalii wa ikolojia. Hapa tunalinda mazingira na kusaidia watu kupata kipato kwa jamii,” alisema, akiongeza kuwa juhudi zake sasa zimevuka sio kwenye misitu tu bali kwenye kila eneo la ikolojia.
Hafla hiyo ilifanyika Desemba 10, siku ambayo Tuzo ya Amani ya Nobel hutolewa Oslo huko Norway. Akikumbuka tukio hilo, Mwenyekiti wa Taasisi ya Wangari Maathai, Wanjira Mathai, amesema siku hizo zilikuwa za kipekee. “Ilikuwa siku tatu za kimiujiza,” alisema.
“Mapambo, gwaride, watoto, mwanga wa mishumaa usiku, tamasha, na sherehe yenyewe… maana yake ilikuwa kubwa sana. Ni muda mrefu lakini nakumbuka kama ilikua jana.”
Alisema Kamati ya Nobel mwaka 2004 ilichukua hatua ya kihistoria kwa kuunganisha suala la amani na mazingira. “Waliona kwamba hakuna amani bila mazingira endelevu,” alisema.
“Mfumo wetu wa maisha ndio jambo la msingi tunalopaswa kulinda.”
Waziri wa Hali ya Hewa na Mazingira wa Norway, Andreas Bjelland Eriksen, alisema tuzo hiyo inaendelea kuwa dira ya kimataifa.
“Alikuwa kama sisi na alituongoza,” alisema.
Alibainisha mabadiliko ya tabianchi si suala la baadaye tena. “Leo yanatokea hapa na sasa, Afrika, Norway na duniani kote,” alisema, akisisitiza umuhimu wa uongozi wa kisiasa licha ya changamoto za majadiliano ya kimataifa.
Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP, Inger Andersen, alikumbuka ujasiri wa Maathai. Alisema alisoma kuhusu Green Belt Movement mwaka 1977 na baadaye kushuhudia ugumu aliokabiliana nao.
Andersen alieleza kuwa Maathai alitoa mwanga katika kipindi ambacho Afrika ilikabiliwa na ukame na hali ya jangwa.
Alisema jamii ya kimataifa iliifuatilia kazi yake kwa makini kwa sababu “tuliona kuwa ilikuwa inaleta mabadiliko.”
Pia alimweleza kama shujaa asiyeogopa ambaye alionesha kuwa hata hatua ndogo, “kama bawa la kipepeo” zinaweza kuleta mabadiliko makubwa.
